(ABNA24.com) Mwaka wa tatu wa mvutano na mzozo baina ya Qatar na nchi nne za Kiarabu za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri ulianza Juni mwaka huu. Ilikuwa tarehe 5 Juni mwaka 2017, wakati Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilipochukua hatua ya kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa sababu ya serikali ya Doha kutofuata muelekeo wa nchi za Kiarabu zinazoongozwa na Saudia. Lakini mbali na kuiwekea vikwazo Qatar, nchi hizo ziliifungia pia Doha mipaka yao ya ardhini, baharini na angani. Licha ya mzozo huo kuingia mwaka wake wa tatu, si tu kwamba, hakuna ishara zozote za kupungua kwake, lakini hivi sasa kadhia ya Hija kwa mara nyingine tena imekuwa sababu ya kushadidi mzozo baina ya Riyadh na Doha.
Saudi Arabia na Qatar kila moja imekuwa ikiutuhumu upande wa pili kwamba, unatumia kwa maslahi ya kisiasa suala la ibada ya Hija. Qatar imetangaza kuwa, Mfalme wa Saudi Arabia anazuia raia wa Qatar kwenda Makka kutekeleza ibada ya Hija. Serikali ya Doha inataja mambo kama kuzuiwa raia wa nchi hiyo kusafiri kwa basi kwenda Saudi Arabia, kutokuweko ubalozi na Beetha ya Hija ya Qatar huko Saudia na kutokuweko safari za ndege za moja kwa moja kutoka Qatar kuelekea Saudia kuwa, miongoni mwa ukwamishaji mambo wa Riyadh wa kuwazuia raia wa Qatar kwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija.
Masuala hayo yalikuwa mjadala pia mwaka uliopita kiasi cha serikali ya Doha kufikia kutoa pendekezo la kuweko 'usimamizi wa kimataifa kwa ibada ya Hija'. Hata hivyo Adil al-Jubeir, Waziri Mshauri Katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni alilitaja ombi hilo kama ni kutangaza vita na Riyadh.
Mkabala na hilo, Mfalme wa Saudia sambamba na kukanusha tuhuma hizo za Qatar amesema kuwa, serikali ya Doha ndiyo inayolitumia kisiasa suala la Hija na kudai kwamba, Qatar ndiyo ambayo inayowazuia raia wake kwenda kutekeleza ibada ya Hija katika hali ambayo, utawala wa Riyadh una hamu na shauku kuona raia wa nchi hiyo wanaelekea Maka kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija. Serikali ya Saudi Arabia inaamini kuwa, hatua ya Qatar ya kuwazuia raia wake kwenda kutekeleza ibada ya Hija inalenga kuzihamasisha na kuzichochea fikra za waliowengi katika Ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya Saudi Arabia.
Anwar Gargash, Waziri Mshauri Katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Imarati sanjari na kutetea hatua yay Saudi Arabia, ameituhumu Qatar kwamba, inalitumia kisiasa suala la ibada ya Hija na wakati huo huo ameitaka Doha iwaruhusu raia wake wakatekeleze jukumu lao la kidini kwa kushiriki katika ibada ya Hija.
Madai hayo yamekabiliwa na radiamali ya viongozi na vyombo vya habari vya Qatar. Ahmed Al-Rumaihi, Mkuu wa Ofisi ya Habari ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Qatar akitoa radiamali yake kwa tuhuma za Saudia dhhidi ya Doha ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba:
Hivi bila ya kuweko ubalozi wa Qatar, Beetha ya Hija na kutoruhusiwa ndege za Qatar kufanya safari za moja kwa moja kuelekea Saudia, vipi tutaamini shauku na hamu ya uongo ya Riyadh na kudiriki kwamba, wana nia raia wa Qatar waende kutekeleza ibada ya Hija?
Gazeti la al-Sharq la Qatar nalo linaandika kuhusiana na jambo hili kwamba: Wizara ya Hija ya Saudi Arabia kwa upande mmoja inawakaribisha Mahujaji wa Qatar na katika upande mwingine inawachoma jambia kwa nyuma.
Nukta muhimu ni hii kwamba, katika miaka ya hivi karibuni Saudi Arabia imeshuhudiwa ikiwazuia Mahujaji wa Yemen na Syria kwenda kutekeleza ibada ya Hija. Kwa msingi huo inawezekana kusema kuwa, kuitumia ibada ya Hija kisiasa na kulifungamanisha suala hilo na uhusiano wake na nchi nyingine za Kiislamu ni jambo ambalo katika miaka ya hivi karibuni limefanywa mara kadhaa na utawala wa Saudi Arabia. Tuhuma za kila upande za Saudia na Qatar katika kadhia ya Hija nalo linaonyesha kwamba, mzozo baina ya Doha na nchi nne za Kiarabu hususan Saudi Arabia ulioanza Juni 5 mwaka 2017 ungali unaendelea.
/129