Main Title

source : Pars Today
Jumatatu

22 Julai 2019

06:09:27
963359

Kutumwa askari wa Marekani nchini Saudia, hatua mpya ya kuzidisha mvutano katika eneo

Hatua za kichochezi za serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani katika eneo, hususan ya kuongeza uwezo na harakati zake za kijeshi katika eneo la Ghuba ya Uajemi, imekabiliwa na radiamali kali na athirifu ya Iran.

(ABNA24.com) Pamoja na hayo mwenendo wa hali ya mambo unaonyesha kwamba Washington katika fremu ya siasa zake za mabavu, inakusudia kuzidisha idadi ya askari na zana zake za kijeshi  katika eneo. Katika uwanja huo Jumamosi asubuhi Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilitangaza kwamba, Mark Esper, Kaimu Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo ametoa kibali cha kutumwa askari na zana za kijeshi nchini Saudia. Katika taarifa hiyo Pentagon imedai kwamba kutumwa akari wa Marekani nchini Saudia kunaweza kuzidisha uwezo wa kuzuia mashambulio ya adui. Kwa hakika kutumwa askari wapya wa Marekani nchini Saudia kuna maana ya kuwarejesha tena askari wa nchi hiyo ndani ya ardhi ya Saudia ikiwa ni baada ya kupita miaka 16. Afisa mmoja katika Wizara ya Ulinzi ya Marekani amenukuliwa akisema kuwa Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia naye ameridhia pendekezo hilo la Washington la kutumwa askari hao nchini humo. Tangazo la utayarifu wa Riyadh la kuwapokea askari hao wa Marekani limekuja baada ya uamuzi wa Marekani wa kutuma askari wapya 500 kwenda kambi ya kikosi cha anga ya Prince Sultan mashariki mwa Riyadh, mji mkuu wa Saudia. Mwezi uliopita pia Marekani ilitangaza kwamba itatuma askari 1000 zaidi Asia Magharibi, ingawa haikuweka wazi ni mahala gani itawatuma askari wake hao. Ijumaa iliyopita, afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kwamba, serikali ya Washington haijalitaarifu bunge la Kongresi kuhusiana na uamuzi wake wa kutuma askari zaidi nchini Saudia. Suala hilo linapata uzito ikizangatiwa kuwa limetekelezwa baada ya Kongresi kupitisha hivi karibuni muswada wa kupinga mauzo makubwa ya silaha kwa Saudia na Imarati.

Kuongezeka uwepo wa askari wa Marekani katika eneo hususan katika Ghuba ya Uajemi katika miezi ya hivi karibuni, kumejiri baada ya kubatilishwa na Washington kibali cha kuziruhusu nchi mbalimbali kuendelea kununua mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kadhalika Marekani kuongeza vikwazo vyake vya mafuta  dhidi ya nchi hii. Hii ni kusema kuwa Marekani katika kutekeleza siasa zake za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran, si tu kwamba imeiwekea Tehran vikwazo vikali ambavyo havijawahi kushuhudiwa, bali sambamba na kuzidisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Ghuba ya Uajemi na katika maji yanayolizunguka eneo hilo kwa kisingizio cha kukabiliana na vitisho vya Iran, imeandaa uwanja wa kuzidisha machafuko na ukosefu wa amani katika eneo. Makabiliano ya Marekani na Iran katika miezi ya hivi karibuni yameshika kasi baada ya kujiri matukio kadhaa yaliyozihusisha meli za kubeba mafuta katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman. Serikali ya Rais Donald Trump inaituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba inahusika na matukio hayo, tuhuma ambazo zinapingwa vikali na serikali ya Tehran. Mvutano kati ya nchi mbili hizi iliongezeka baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kutungua ndege ya kijasusi na ya kisasa kabisa ya Marekani baada ya ndege hiyo kukiuka anga ya Iran ambapo dakika chache baadaye, Trump alitoa madai ya kutoa amri ya kushambuliwa baadhi ya maeneo ya Iran lakini eti akalazimika kuifutilia mbali muda mfupi kabla ya kutekelezwa mashambulio hayo. Pamoja na hayo Iran inaamini kwamba uwezo wake wa kijeshi, ndio ulioifanya Marekani kushindwa kutekeleza mashambulizi yoyote ya ulipizaji kisasi dhidi yake.

Ni wazi kuwa Washington inajaribu kushadidisha mzozo katika eneo hili kupitia madai bandia na habari za uongo. Katika uwanja huo Alkhamisi usiku Trump alidai kwamba meli ya kivita ya Marekani ilitungua ndege isiyo na rubani ya Iran katika eneo la Lango Bahari la Hormuz. Kwa mujibu wa rais huyo, meli ya kivita ya Marekani ya USS BOXER ilichukua hatua hiyo baada ya ndege hiyo kutozingatia maonyo iliyopewa baada ya kukaribia meli hiyo. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia picha zilizochukuliwa na ndege hiyo kwenye meli ya Marekani, imekadhibisha madai hayo na hivyo ikawa imefichua uongo mwingine wa Wamarekani kwa dunia. Inaonekana kwamba baada ya ndege ya thamani kubwa ya ujasusi ya Marekani aina ya Global Hawk kutunguliwa na Iran, sasa Trump anajitahidi kuibua vita vya kisaikolojia na madai bandia dhidi ya Iran ili kuwaridhisha Wamarekani. Baadhi ya duru za habari zimearifu kwamba ndege iliyotangazwa kutunguliwa na Marekani hivi karibuni ni ya Imarati. Iwapo habari hiyo itakuwa na ukweli, si tu kwamba itapelekea kutiliwa shaka uwezo wa Marekani katika kutambua zana za kijeshi za marafiki na maadui wake, bali udhaifu huo utakuwa na taathira hasi kwa Saudia na Imarati ambazo zinadhani kuwa uwepo wa Wamarekani katika eneo ni kwa ajili ya kuwadhaminia usalama wao.



/129