(ABNA24.com) Katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani, siasa za upande mmoja za Washington dhidi ya nchi tofauti zinazopinga ubeberu na kupenda makubwa kwa Marekani, ikiwemo Venezuela , zimebadilika kuwa moja ya tofauti za msingi kati ya serikali ya Moscow na Washington.
Licha ya kwamba serikali ya Washington inawaunga mkono wazi wazi wapinzani wa Venezuela wanaoongozwa Juan Guaidó kwa lengo la kumuondoa madarakani Nicolás Maduro, rais halali wa nchi hiyo, lakini wakati huo huo kupitia siasa zake za undumakuwili hairidhii kuona Russia ikiiunga mkono serikali halali na rais huyo wa Venezuela. Kufuatia hatua ya kufuatiliwa ndege ya ujasusi ya EP-3 ya kikosi cha baharini cha jeshi la Marekani iliyofanywa na kamandi ya operesheni ya kistratijia ya Venezuela, Washington imeituhumu Moscow kuwa inatoa uungaji mkono usio wa kuwajibika kwa serikali ya Caracas. Jumapili iliyopita kikosi cha kamandi ya kusini mwa Marekani kilionyesha video ya kufuatiliwa ndege hiyo ya ujasusi ya Marekani na ndege ya kivita aina ya Sukhoi Su-30 ya Russia kitendo kilichofanywa na jeshi la anga la Venezuela. Jeshi la Marekani limetangaza kwamba tukio hilo lilijiri tarehe 19 ya mwezi huu na kwamba ndege hiyo ya ujasusi ilikuwa ikiruka katika bahari ya Caribbean, lakini pamoja na hayo halikuashiria kwa namna yoyote ukaribiaji wa ndege hiyo kwenye mipaka ya Venezuela. Kama kawaida, jeshi hilo la Marekani lilidai kwamba, ndege yake hiyo ilikuwa ikiruka kwenye anga ya kimataifa. Pia kamandi ya kusini mwa Marekani imeongeza kwamba hatua ya Venezuela ya kufuatilia ndege yake ya ujasusi ilihatarisha usalama wa ndege hiyo na watu waliokuwa ndani yake na kuongeza kuwa, ndege hiyo ya Venezuela ilikaribia kiwango cha kuhatarisha usalama wa ndege hiyo ya Marekani.
Mkabala wake Vladimir Padrino López, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amesema kuwa, kamandi ya operesheni ya kistratijia ya nchi hiyo iliifuatilia ndege hiyo ya ujasusi ya EP-3 yenye zana za kunasa taarifa na ujasusi wa kielektroniki na uwezo wa kufuatilia pia nyambizi katika eneo hilo la kiuchumi kwa msingi wa sheria zake. Kwa kuzingatia kuwa ndege ya kivita ya Sukhoi Su-30 ilitengenezwa na Russia, hivyo jeshi la Marekani linaituhumu Moscow kuwa inaiunga mkono serikali ya Caracas. Katika uwanja huo kamandi ya kusini mwa Marekani imedai kwamba: "Uungaji mkono huo wa kijeshi usio wa kuwajibika" wa Russia kwa serikali ya Venezuela na hatua ya Rais Nicolás Maduro ya kudhoofisha juhudi za kukabiliana na magendo, ni jambo lisilokubalika." Ukweli ni kwamba Wamarekani wanadai kuwa ndege yake ya ujasusi ilikuwa inatekeleza operesheni za kufuatilia magendo katika bahari ya Caribbean, katika hali ambayo jeshi la baharini la Marekani lina mazoea ya muda mrefu ya kufanya ujasusi kwa kutumia ndege zake dhidi ya Venezuela. Wakati huo huo, madai ya Marekani kuhusu uungaji mkono usio wa uwajibikaji wa Russia kwa Venezuela, ni ya kushangaza sana. Hii ni kwa kuwa katika kipindi cha utawala wa Hugo Chávez, rais wa zamani wa Venezuela, serikali ya Moscow iliwekeana saini na Caracas makubaliano ya mauzo ya silaha katika muongo wa 2000 ambapo ndege za kivita za Sukhoi Su-30, zilikuwa sehemu ya mauziano hayo.
Hivyo hatua ya sasa ya Washington ya kuilaumu Moscow kwa kuiuzia ndege hizo Venezuela na kuitaja kuwa ni uungaji mkono usio wa kuwajibika, ni jambo la kushangaza sana. Mbali na hayo idadi kadhaa ya askari wa Russia wapo nchini Venezuela kwa ajili ya kuisaidia serikali ya Caracas kukabiliana na changamoto zinazoikabili. Kuhusiana na suala hilo, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ambaye amesafari nchini Venezuela alisema siku ya Jumapili mbele ya waandishi wa habari mjini Caracas kuwa, uwepo wa wataalamu wa kijeshi wa Russia nchini Venezuela, unatokana na ombi la viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa Ryabkov: "Wataalamu wa kijeshi wa Russia, tayari wametekeleza majukumu yao lakini iwapo nchi hiyo ya Amerika ya Latini itahitajia tena huduma zao, basi wanaweza kubakia nchini humo kwa muda mrefu zaidi." Russia kama moja ya nchi zenye uwezo mkubwa wa kijeshi kimataifa na inayoshindana na Marekani, kwa mara kadhaa imekuwa ikipinga wazi mienendo na hatua za Marekani dhidi ya Venezuela sambamba na kutangaza uungaji mkono wake kwa serikali na rais halali wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Trump imeshadidisha hatua zake za kimabavu kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya mrengo wa kushoto ya Rais Nicolás Maduro. Hii ni katika hali ambayo kwa upande wake, Moscow imekuwa ikisisitiza juu ya ulazima wa kutatuliwa mzozo wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini kwa njia ya amani, sambamba na kukaribisha mazungumzo ya serikali na wapinzani wa Venezuela kwa upatanishi wa Norway.
/129