Main Title

source : Pars Today
Jumapili

28 Julai 2019

07:43:45
965216

Kuaga dunia rais wa Tunisia na matukio ya usoni

Kufutia kifo cha Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia, Mohamed Ennaceur (an-Nasir) spika wa bunge la nchi hiyo, ameteuliwa kushikilia kwa muda nafasi hiyo.

(ABNA24.com) Essebsi, ambaye amekuwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Tunisia, ameaga dunia baada ya kupitisha muda fulani akitibiwa katika hospitali moja ya kijeshi mjini Tunis. Amekuwa rais wa Tunisia tokea mwaka 2014 ambapo kabla ya hapo aliwahi kuhudumia nafasi za waziri mkuu na spika wa bunge la Tunisia kati ya mwaka 1990 na 2011. Alichaguliwa kidemokrasia kuwa rais wa nchi hiyo kufuatia mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa bara la Afrika.

Habari ya kuaga dunia Essebsi imetangazwa katika hali ambayo Tunisia imekuwa ikishuhudia matukio muhimu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika miaka ya hivi karibuni. Kuhusiana na suala hilo wataalamu wengi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Essebsi amekuwa na nafasi muhimu na chanya katika mkondo wa masuala ya kisiasa ya nchi hiyo na sasa wana wasiwasi kuwa huenda kutokuwepo kwake kukavuruga mkondo huo.

Rashid al-Ghanushi, mwenyekiti wa chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha an-Nahdha cha nchini Tunisia, anasema: Baadhi ya watu wanaamini kwamba Essebsi amekuwa nguzo kuu ya mfumo wa kidemokrasia nchini Tunisia hivyo dhana ya kuwa wapinzani wa demokrasia ndio waliopanga njama ya kumuua haiko mbali na ukweli.

Kwa mtazamo wa kijamii na kiuchumi, Tunisia ingali inakabiliwa na matatizo mengi kama vile mgogoro wa kiuchumi na ufisadi na tofauti ya matabaka ya kijamii. Hasi sasa viongozi wa nchi hiyo hawajafanikiwa kutatua matatizo ya kiuchumi ambayo yaliwapelekea wananchi wa nchi hiyo kufanya maaandamano makubwa yaliyopelekea kupinduliwa serikali ya wakati huo mwaka 2011. Kwa msingi huo ughali wa maisha bado ni wa kiwango cha juu nchini Tunisia na wala marehemu Essebsi hakufakiwa kulitatua suala hilo katika kipindi cha uongozi wake kwa kadiri kwamba Shirika la Kimataifa la Fedha IMF limesema kwamba kuna udharura wa kupunguzwa kiwango cha ughali wa maisha nchini humo kwa asilimia 7 na kwamba ahadi ya kuimarishwa ukuaji uchumi wa asilimia 2 pekee haitoshi.

Katika mtazamo wa kijeshi na usalama wa nchi, serikali ya Tunisia katika miaka ya hivi karibuni imefanikiwa kuimarisha kwa kiwango fulani usalama wa maeneo mengi ya nchi hiyo, na imeweza kudhibiti usalama wa mpakani licha ya kuwa nchi hiyo inapakana na Libya ambayo inakabiliwa na mapigano ya ndani na kuwepo hatari ya kupenya makundi ya kigaidi na kuingia katika ardhi ya Tunisia.

Katika siasa za nje pia, Essebsi alijulikana kwa misimamo yake mikali dhidi ya utawala haramu wa Israel na akifahamika kuwa mmoja wa wapinzani sugu wa kuimarishwa uhusiano wa Waarabu na utawala huo ghasibu.

Kwa mujibu wa katiba ya Tunisia inayosema kuwa iwapo rais wa nchi ataaga dunia akiwa ofisini ni spika wa bunge ndiye atachukua kwa muda nafasi hiyo, Mohamed Ennaceur amepewa nafasi ya kuhudumu kwa muda katika nafasi hiyo ili kuandaa uchaguzi mkuu katika kipindi cha siku 45 hadi 90. Kuhusiana na suala hilo, Mohamed Ennaceur amesema: Matunda ya Tunisa yatalindwa katika fremu ya demokrasia na uchaguzi wa rais wa nchi utafanyika kwa mujibu wa sheria na katika wakati uliopangwa.

Kwa msingi huo, katika miezi kadhaa ijayo, Tunisia itashuhudia matukio mawili muhimu ya kisiasa yaani ya kufanyika chaguzi mbili za rais na bunge, ambazo zina umuhimu mkubwa katika matukio ya baadaye ya nchi hiyo. Wachambuzi wengi wa mambo wana wasiwasi kuwa huenda kifo cha Essebsi kikaathiri vibaya chaguzi mbili hizo. Tume ya uchaguzi ya Tunisia imetangaza kuwa badala ya tarehe 17 Novemba, sasa uchaguzi wa rais utafanyika tarehe 15 Septemba mwaka huu. Inaonekana kuwa tarehe hiyo mpya imetangazwa kwa ajili ya kutuliza hali ya kisiasa ya nchi hiyo na kusaidia kuudwa serikali ijayo kwa msingi wa demokrasia.

Mohamed Ennaceur, rais wa muda wa Tunisia ameahidi kwamba uchaguzi ujao wa rais utafanyika kwa msingi wa sheria na katika wakati uliopangwa ambapo amewataka Watunisia wote, mashirika na vyama vya siasa vishirikiane na serikali ili kufanikisha uchaguzi huo. Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa hivi sasa Watunisia wanapitia siku muhimu za kuanisha mustakbali wa kisiasa na kulinda demokrasia ya nchi yao.



/129