(ABNA24.com) Sheikh Khalid Ahmad Aal Khalifa amedai kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Mashambulio ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya nchi tatu za Iraq, Syria na Lebanon ni aina mojawapo ya kujihami. Akijengea hoja madai yake hayo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain ametumia kipengee cha 51 cha hati ya Umoja wa Mataifa ambacho kinahusiana na uhalali na haki ya kujihami.
Kwa hakika, haki ya kujihami iliyozungumziwa na kipengee cha 51 cha hati ya Umoja wa Mataifa inapata nguvu pale inapotokea kwamba, nchi fulani imeshambuliwa na nchi nyingine. Katika hali hiyo, nchi iliyoshambuliwa ina haki ya kujihami dhidi ya hujuma na mashambulio. Kwa muktadha huo, madai na hatua ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain ya kutumia kipengee hicho kuhalalisha mashambulio ya Israel si sahihi, kwani Israel haijashambuliwa na nchi yoyote ile bali yenyewe ndio iliyochukua hatua ya kuzishambulia nchi za Iraq, Syria na Lebanon.
Kuhusiana na suala hilo, Barham Salih, Adil Abdul-Mahdi na Mohamed al-Halbousi, Rais, Waziri Mkuu na Spika wa Bunge la Iraq wamesisitiza kuwa, mashambulio ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya ngome za Hashdu al-Shaabi, ni sawa kabisa na kushambuulia mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.
Nukta nyingine inahusiana na sababu ya kutolewa matamshi kama hayo na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain dhidi ya mamlaka ya kujitawala nchi nyingine ya Kiarabu na kuunga mkono jinai za utawala dhalimu wa Israel. Katika miezi ya hivi karibuni, utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain umechukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuanzisha uhusiano rasmi na utawala huo ghasibu kama vile kuwa mwenyeji wa mkutano wa Manama uliokuwa na lengo la kuzinduliwa mpango wa 'Muamala wa Karne' ambapo waziri huyo alitoa matamshi mengi kuhusiana na suala hilo.
Sheikh Khalid Ahmad Aal Khalifa alinukuliwa mwezi Juni mwaka huu akiitaja hatua ya Wapalestina ya kutoshiriki katika mkutano wa Manama kwamba ni kosa na kutetea mashambulio ya Israel dhidi ya Syria akidai kwamba, utawala huo wa Kizayuni una haki ya kujihami. Kwa hakika kutolewa matamshi kama hayo na kuonyesha waziwazi Manama kwamba, ina hamu na shauku ya kuanzisha uhusiano rasmi na Israel, chimbuko lake ni himaya na uungaji mkono wa Tel Aviv kwa utawala wa Bahrain kwa ajili ya kukandamiza harakati za wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Katika upande mwingine utawala wa Aal Khalifa unafanya juhudi kupitia kuwa pamoja na Israel ili upate uungaji mkono zaidi wa Marekani dhidi ya wapinzani wa ndani, kwani utawala huo, unakabiliwa na upinzani mkali kabisa wa ndani ulioanza tangu Februari 14 mwaka 2011. Licha ya ukandamizaji mkubwa wa vyombo vya usalama vya Bahrain dhidi ya wapinzani, lakini hadi sasa upinzani na malalamiko ya wananchi dhidi ya utawala wa Manama yangali yanaendelea katika nchi hiyo.
Utawala wa Bahrain unaunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nchi za Kiarabu katika hali ambayo Iraq, Syria na Lebanon ni nchi za Kiarabu na Kiislamu. Licha ya kuwa, kuna mgongano wa utambulisho wa kisiasa baina ya utawala wa Aal Khalifa na nchi hizo tatu za Kiarabu, lakini kwa uchache nchi hizo zinashirikiana katika mambo mawili na Bahrain ambayo ni kuwa kwao za Kiarabu na Kiislamu. Kwa hakika mwenendo huu wa Bahrain unaibua swali hili kwamba, je viongozi wa utawala wa Aal Khaliifa wana utambulisho wa Kiarabu au Kiebrania?
/129