(ABNA24.com) Vituo vya mafuta vya shirika la mafuta la Aramco katika viwanda vya kusafisha mafuta vya Abqaiq na Khurais vilivyoko mashariki ya Saudi Arabia vimeteketezwa na moto mkubwa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imetangaza kuwa chanzo cha moto huo ni shambulio lililofanywa na ndege zisizo na rubani za droni.
Kikosi cha droni cha jeshi na wapiganaji wa kujitolea wa Yemen kimetangaza kuwa ndicho kilichohusika na shambulio hilo lililolenga vituo vya mafuta vya Saudi Arabia.
Mwezi wa 54 wa vita vilivyoanzishwa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen unakaribia kumalizika. Saudi Arabia, ambayo ilitarajia kuwa ingeshinda vita hivyo katika muda wa chini ya mwezi mmoja na kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansur Hadi, baada ya muda kupita ilibaini kwamba kumrejesha madarakani Mansur Hadi ni kazi ngumu mno. Utawala wa Aal Saud ulisababisha maafa na uharibifu mkubwa katika vita hivyo kwa nia ya kuisambaratisha harakati ya Ansarullah na waitifaki wake, lakini sasa watawala wa Riyadh wameng'amua kwamba utumiaji mbinu hiyo katika vita dhidi ya Yemen haujaweza kuwa na tija kwao, kwa sababu ni harakati ya Ansarullah na waitifaki wake ndio waliopata ukomavu kutokana na maafa na uharibifu uliofanywa na Saudia kwa kuweza kujiimarisha kiulinzi na kiushambuliaji na kutoa kipigo sambamba na kusababisha maafa makubwa kwa madola vamizi ya Saudi Arabia na Imarati. Shambulio kali dhidi ya vituo vya Aramco lililofanywa mwezi uliopita na ndege kadhaa zisizo na rubani, na shambulio la jana la droni 10 dhidi ya vituo vingine vya shirika hilo la mafuta ni miongoni mwa hatua za kujibu mapigo zilizochukuliwa na Ansarullah na waitifaki wake.
Mashambulio yote hayo yanaonyesha kuwa Ansarullah na jeshi la Yemen zimeamua kuilenga sekta ya mafuta ya Saudia. Kwa kuvishambulia vituo vya mafuta vya shirika la Aramco, harakati ya Ansarullah na jeshi la Yemen zinaonyesha kuwa lengo lao ni kuuhasiri uchumi wa Saudi Arabia ni kuubebesha mzigo mzito zaidi wa gharama za vita utawala wa Aal Saud; kwa sababu Saudia ndiyo mzalishaji na muuzaji mkubwa zaidi wa mafuta duniani; na mafuta ndio chanzo kikuu cha mapato ya fedha ya nchi hiyo. Vituo vya mafuta vya Aramco vilivyoko mkoani Abqaiq, ambavyo vimeshambuliwa na ndege zisizo na rubani za Yemen vinahifadhi kiwango kikubwa zaidi cha akiba ya mafuta ya Saudia cha mapipa bilioni moja.
Nukta nyingine ya ujumbe uliomo katika mashambulio yaliyofanywa na droni za Yemen, likiwemo shambulio la jana katika vituo vya Aramco vya viwanda vya kusafisha mafuta huko Abqaiq na Khurais, ni kwamba, jeshi na wapiganaji wa kujitolea wa Yemen hawana nia ya kuendeleza vita, bali wanafanya mashambulio hayo kwa madhumuni ya kujihami tu na kuzuia hujuma dhidi ya nchi yao. Kwa hakika lengo lao hasa na kuizidishia Saudia mzigo wa gharama za vita, na kwa njia hiyo kuilazmisha ikomeshe vita hivyo vya kinyama ilivyoanzisha dhidi ya Yemen.
Kuhusiana na nukta hiyo, kufuatia shambulio la jana la wanamuqawama wa Yemen dhidi ya vituo vya shirika la mafuta la Aramco lililosababisha moto katika vituo hivyo sambamba na kukiri utawala wa Aal Saud kuhusu chanzo cha moto huo, Muhammad al Bukhayti, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah, amefanyiwa mahojiano na kanali ya televisheni ya Aljazeera ya Qatar, ambapo sambamba na kuashiria yote hayo ametishia kwamba, ikiwa Saudi Arabia haitakomesha uvamizi na hujuma zake dhidi ya Yemen, wapiganaji wa nchi hiyo wataelekeza mashambulio yao mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Kwa kuzingatia yote hayo, kinachotarajiwa ni kuiona Saudia ikibadilisha stratejia yake katika vita ilivyoanzisha dhidi ya Yemen. Kuendelea vita vinavyoandamana na maafa na uharibifu hakuwezi kudhamini maslahi ya Saudia. Linalopasa kufanywa hivi sasa na nchi hiyo ni kufanya kila njia ili kuhitimisha vita ilivyoanzisha, na kujitoa kwenye mkwamo wa kinamasi wa vita hivyo, kwa sababu kuendelea kwake kunaweza kuusababishia maafa na kushindwa kubaya zaidi utawala wa Aal Saud.../
/129
source : Pars Today
Jumatatu
16 Septemba 2019
08:15:51
975883
Vituo vya mafuta vya shirika la mafuta la Aramco katika viwanda vya kusafisha mafuta vya Abqaiq na Khurais vilivyoko mashariki ya Saudi Arabia vimeteketezwa na moto mkubwa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imetangaza kuwa chanzo cha moto huo ni shambulio lililofanywa na ndege zisizo na rubani za droni.