(ABNA24.com) Kufuatia kuongezeka mashambulizi ya ugaidi katika nchi za Kiafrika, hususan eneo la Sahel, viongozi wa eneo la magharibi mwa bara hilo, wametenga kiasi cha Dola bilioni moja kwa ajili ya kukabiliana na tishio linaloongezeka la harakati za makundi yenye kufurutu ada katika eneo.
Kwa muda sasa harakati za makundi ya kigaidi zimekuwa ni daghadagha kuu kwa nchi za Kiafrika. Shughuli za makundi ya kigaidi kama vile ash-Shabab katika eneo la mashariki mwa Afrika hususan nchini Somalia na Boko Haram huko magharibi mwa bara hilo hususan Nigeria na nchi majirani na taifa hilo, kwa muda sasa zimekuwa zikichafua usalama wa nchi za bara hilo. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, zaidi ya magaidi elfu 10 kutoka makundi mawili ya kigaidi ya Daesh (ISIS) na al-Qaidah, wako katika nchi za Afrika. Hali hiyo imepelekea hata sehemu kubwa ya bajeti na suhula za nchi za Kiafrika, kutumika katika mapambano tu dhidi ya makundi hayo ya kigaidi. Hii ni katika hali ambayo, katika upande wa utendaji pia, mapambano hayo hayajakuwa na natija yoyote, huku makundi hayo yakiendelea kuwafanya mamia ya watu katika nchi za bara hilo kuwa wahanga wa hujuma zao. Wakati hadi sasa mapambano dhidi ya makundi hayo hayajakuwa na mafanikio ya maana, ripoti mpya zinaonyesha kwamba, katika miezi iliyopita, makundi yenye mahusiano na magenge ya al-Qaidah na Daesh (ISIS) pia yalipiga kambi katika eneo lote la Sahel ya Afrika na hivyo kugeuka kuwa tishio kubwa kwa nchi za bara hilo. Ukweli ni kwamba makundi ya kigaidi, si tu yanaitumia jografia, ukubwa wa ardhi na utajiri wa nchi za Kiafrika kwa ajili ya malengo yao, lakini pia kutokana na bara hilo kuwa na hali mbaya ya kiuchumi na umasikini na vile vile jamii kubwa ya vijana, yanahisi nchi za Afrika ni eneo zuri kwa ajili ya kuvutia na kulea wapiganaji wa kigaidi, kiasi kwamba akthari ya makundi hayo yameweza kuwashawishi vijana wengi wa bara hilo kujiunga nayo kwa kutumia kiasi kidogo tu cha fedha na ahadi za kuwaboreshea hali zao za maisha.
Katika uwanja huo, Julai mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulitangaza kwamba, mashambulizi ya makundi yenye kufurutu ada yanaongezeka kwa kasi magharibi mwa Afrika, na kwamba eneo hilo lifikirie kuchukua madhubuti zaidi kuliko juhudi za kijeshi zinazofanywa hivi sasa. Kwa upande mwingine ni kwamba, mgogoro wa kisiasa nchini Libya, mazingira yasiyo ya kuridhisha ya baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika, halikadhalika kushindwa kwa genge la Daesh (ISIS) nchini Syria na Iraq, ni mambo ambayo yameyafanya makundi ya kigaidi yaaamue kuanzisha ngome mpya na mashambulio dhidi ya nchi mbali mbali za Afrika zikiwemo za eneo la Sahel. Japokuwa baada ya kutambua hatari ya ugaidi, mwaka 2017 nchi tano za eneo hilo, ambazo ni Burkina Faso, Niger, Mali, Mauritania na Chad, ziliunda kikosi cha operesheni maalumu cha 'G 5' kupitia ahadi na uungaji mkono wa Ufaransa na msaada wake wa kifedha, kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya wanamgambo, lakini kikosi hicho hakijaweza kufanya kazi yake kutokana na serikali ya Paris kutotekeleza ahadi zake katika suala la utoaji fedha. António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameashiria jinsi mgogoro wa kigaidi ulivyoathiri familia na uthabiti wa eneo lote la Afrika na akasisitiza kuwa, haipasi kuruhusu ugaidi udhoofishe mwenendo wa ustawi wa bara la Afrika, na kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni, kuna udharura wa jamii ya kimataifa kuziunga mkono nchi za Kiafrika.
Hivi sasa nchi 15 wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) na marais wa Chad na Mauritania wamekutana Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso katika kikao cha dharura chenye lengo la kujadili ongezeko la machafuko barani humo. Katika kikao hicho viongozi hao, kupitia fremu ya ushirikiano wa kieneo, wamejadili njia za kudhamini msaada wa kifedha wa kiasi cha Dola bilioni moja. Naye Jean-Claude Brou, Mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) amesema kuwa, kamisheni ya jumuiya hiyo imechukua uamuzi wa kutenga kiasi cha Dola bilioni moja kupitia ushiriki wa kifedha, kama ambavyo kutafanyika juhudi shirikishi za haraka kwa ajili ya kupambana na ugaidi. Inaonekana kwamba katika kuziba ombwe na uingiliaji na ahadi za nchi za kigeni, viongozi wa Afrika wanafanya juhudi kwa ushirikiano wa pamoja waweze kupiga hatua ya kivitendo katika kupambana na ugaidi na pia kuimarisha usalama katika nchi tofauti za bara hilo, hata kama njia hiyo inakabiliwa na vizingiti vigumu.
/129
source : Pars Today
Jumatatu
16 Septemba 2019
08:21:48
975893
Kufuatia kuongezeka mashambulizi ya ugaidi katika nchi za Kiafrika, hususan eneo la Sahel, viongozi wa eneo la magharibi mwa bara hilo, wametenga kiasi cha Dola bilioni moja kwa ajili ya kukabiliana na tishio linaloongezeka la harakati za makundi yenye kufurutu ada katika eneo.