UTENZI WA KUKARIBISHA RAMADHANI.

  • Habari NO : 332243
  • Rejea : ABNA.ir

1.

KWA MOYO USO INADI.

NAWALETEA ZAWADI.

ITOKAYO KWA WAHIDI.

ILLAHI MOLA JALIA.

2.

ZAWADI HASA YAKINI.

IZIDISHAO IMANI.

KURUDI KWA RAHAMANI.

KUFUATA YA NABIA.

3.

ZAWADI YENYE AMANI.

IPENDEZAO MOYONI.

ZAWADI NI RAMADHANI.

WAZI NAWATANGAZIA.

4.

NI MWEZI USIO SHAKA.

NI MWEZI WENYE BARAKA.

NDIO HUNU USHAFIKA.

WAJA UMETUFIKIA.

5.

TUMSHUKURU ILLAHI.

KUTUJALIA UHAI.

KUFIKIA SAHIHI.

TENA UMETUFIKIA.

6.

WANGAPI LEO NANENA.

WALO USUBIRI SANA.

LAKINI MOLA RABANA.

RABBI HAKUWAJALIA.

7.

HAKUJALIA KUONA.

WASHARUDI KWAKE SANA.

KWENYE NJIA ILE PANA.

SOTE TUTAIPATIA.

8.

NDIO KWA YAKE HIARI.

ILLAHI MOLA KAHARI.

KWA MWEZI HUNU WA HERI.

SISI TUMEJIONEA.

9.

LAZIMA TUONE RAHA.

RAHA ISO IKIRAHA.

RAHA ILO NA FURAHA.

SISI UMETUFIKIA.

10.

NDIO NATOWA WASIA.

UPATE KUWAFIKIA.

KWA MUNAONITEGEA.

MUPATE KUZINGATIA.

11.

ZINGATIENI JAMANI.

KWA MWEZI WA RAMADHANI.

TUSIENDE MFUNGONI.

MABICHI KUJIENDEA.

12.

MFUNGO HAUNA MANA.

NI KITU HULETA LANA.

LANA ILO NA HIANA.

YA KUFANYA MAASWIA.

13.

NI MWEZI MTUKUUFU.

TUPOKE’ KWA MATUKUFU.

YAKE ILLAHI LWATIFU.

ELA SIO MAASWIYA.

14.

TUFANYE KAMA NI ADA.

TUPOKEE KWA IBADA.

ILI TUSIPATE SHIDA.

KESHO IKITUFIKIA.

15.

NI MWEZI WENYE NA HERI.

TUYAFANYE YA BASHIRI.

KUUPOKEA SI SIRI.

ATATULINDA JALIA.

16.

KWA KUSOMA KUR-ANI

KWA MWEZI WA RAMADHANI.

INAPENDEZA YAKINI.

ITAJA TUSAIDIA.

17.

TUKIFIKA KABURINI.

ITATULINDA YAKINI.

NI MAMBO HAYA AMINI.

AMEYASEMA NABIA.

18.

NA ALAFU LA ZIADA.

MWEZI HUNU WA IBADA.

QUR-ANI ISO SHIDA.

NDO’ LITEREMSHIWA.

19.

‘LITEREMSHWA QU-RANI.

KWA MWEZI WA RAMADHANI.

KWA HIVYO TUISOMENI.

ITATUFAA SIKIA.

20.

NDIO LEO NINASEMA.

NI TULALENI MAPEMA.

TUAMKENI KUISOMA.

NA KUSWALI NAO PIA.

21.

TUIFANYENI SHAUKU.

KWA KUAMKA USIKU.

KWA KUSWALI KILA SIKU.

KIYAMU-LELI SIKIA.

22.

UMUOMBE MOLA WAKO.

KWENYE YOTE YA VITUKO.

ILLAHI AKUPE HEKO.

AKUSAMEHE JALIA.

23.

USHUKURU BILA INDA.

KWENYE MEMA KUYATENDA.

TENA UZIDI KUPANDA.

MEMA ‘WEZE JIPANDIA.

24.

ILI KWENYE LAKO JASHO.

YAJE YAKUFAE KESHO.

KATIKA SIKU YA MWSIHO.

YA KIAMA KUWADIA.

25.

NDIO NAWELEZA SASA.

TUCHUKWENI HINI FURSA.

YA RAMADHANI KABISA.

TUWEZE KUITUMIA.

26.

PIA TUTOWE SADAKA.

KWA WINGI BILA YA SHAKA.

ITATUFAA HAKIKA.

SIKU ITAPOFIKIA.

27.

KATIKA ZAKO IBADA.

VYEMA KUWE NA ZIADA.

ISIWE NI KAWAIDA.

VILE ULIVYOZOEA.

28.

HINI ITAKUWA HERI.

KUENGEZA SIO SIRI.

IBADA HUTOWA SHARI.

HUSHINDWA KUKUFIKIA.

29.

NDIO LEO KWA YAKINI.

TUHESHIMU RAMADHANI.

TUSIENDE MFUNGONI.

KUYAFANYA MAASWIYA.

30.

RAMDHAN MWEZI MWEMA.

TUYASHIKE YA KARIMA.

ALIYOMPA HASHIMA.

MTUME WETU NABIA.

31.

TUSIFUATE HASARA.

KUSHIKWA YA KINASWARA.

YALE MAMBO YA KIKORA.

YAKAJA TUHARIBIA.

32.

NDIO NAELEZA WAZI.

VYEMA TUANZE ZOEZI.

LA KUYASHIKA YA MWENYEZI.

ILLAHI MOLA JALIA.

33.

NA WAVUTAJI SIGARA.

KUPUNGUZA YAWA BORA.

TUTAIKOSA HASARA.

RAMADHAN KIANZIA.

34.

NA WALAJI MAIRUNGI.

DHATI MUKIBADILISHA RANGI.

MUTAFANYA LA MSINGI.

MBALI KUYAACHILIA.

35.

NA WANYWAJI WA POMBE.

TUSIWENI KAMA NG’OMBE.

KATIKA HUNU UPAMBE.

VYEMA KUUWACHILIA.

36.

WATUMIAJI MADAWA.

MOLA AWAPE AFUWA.

AFUWA YA KUYATOWA.

MBALI KUYAACHILIA.

37.

NA LOLOTE LA HARAMU.

TULIWATE ISILAMU.

ILI SIKU ZIKITAMU.

RAMDHAN KUANZIA.

38.

TUFANYE LILILO SAWA.

KWETU IWE NDIO DAWA.

TUTAIPATA AFUWA.

KUTUHIFADHI JALIA.

39.

HAYA NILOWATUNGIA.

RAMADHAN KUIPOKEA.

HIVYO MUWEZE NGOJEA.

MWENGINE ME’WANDALIA.

40.

‘MEWANDALIA YAKINI.

UTENZI WA RAMDHANI.

HIVYO NI MUWE MAKINI.

MUWEZE KUUNGOJEA.

41.

JAMANI UNGONJEENI.

UTENZI WA RAMADHANI.

KWA SASA UKO JIKONI.

TAWAPA IKIWADIA.

42.

HUNU NI KUKARIBISHA.

JAMII KUIKUMBUSHA.

MAASWI KUJIEPUSHA.

MFUNGONI NAWAMBIA.

43.

SASA NIWEKE KHATIMA.

IWE NI BISHARA NJEMA.

KWA TULO SOTE UMMA.

MFUNGO KUTOJIENDEA.

44.

TUKARIBISHE KWA HERI.

MWEZI HUNU SIO SIRI.

KWA ILI MOLA KAHARI.

ATUHIFADHI JALIA.

45.

WATAMATI UKINGONI.

MTUNZI WA TUNGO HINI.

MTUNZI NI ALAMINI.

SIWA SOMO NAWAMBIA.

MALENGA WA MOMBASA

 


پیام رهبر انقلاب به مسلمانان جهان به مناسبت حج 1441 / 2020
We are All Zakzaky
Hatuukubali muamala wa Karni