Mafunzo ya jamii

MADHARA YA MIRUNGI- Sehemu ya Pili

  • Habari NO : 382539
  • Rejea : ABNA

Madhara Ya Kiafya

Matatizo na madhara ya Mirungi yalielezwa mwanzo wa mwaka 1935 na League Of Nations, Mwaka 1970 taasisi ya tiba ikaitenga madhara ya cathinone yanayopatikana katika Mirungi ambayo kikemikali inafanana na amphetamine, na hivyo katika mwaka 1971 ikaorodheshwa na United Nation kua ni miongoni mwa madawa ya kulevya. 

Bw.Mathew Bryden aliyekuwa akifanya kazi na mashirika ya msaada kwa miaka mitatu huko Somalia alisema: “Watumiaji wengi wa Mirungi wamejikuta wakipambana na msisimko wake ili waweze kupata usingizi au hata kufanya kazi kisawasawa. Wanaelekea kwenye pombe au madawa ili kupata mapumziko au kupunguza hali ya wasiwasi. “Hali ilivyo Mogadishu ni watu kutawaliwa na nguvu za Mirungi, madawa au pombe,” Bw.Bryden akiendelea: “Unakuwa umevurugikiwa kabisa,  Ima uharibikiwe kikamilifu au upoteze mwelekeo wa hali halisi.”

Utumiaji wa Mirungi husababisha madhara mbalimbali kiafya kama:

1- Magonjwa ya vidonda vya tumbo (ulcers).

 2- Ukosefu wa haja kubwa (constipation).

 3- Utumiaji wa muda mrefu husababisha kuharibu utendaji kazi wa ini, na pia kusababisha ubadilikaji rangi meno, kudhoofika, na fizi kuuma na harufu ya mdomo.

 4- Upungufu wa msukumo wa kufanya jimaa (sex drive). Na pia kuwahi kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu.

 5- Kupatwa na ugonjwa wa futuru/futuri/bawasiri/baasili - nyama inayoota kwenye utupu wa nyuma.

 6- Upungufu wa usingizi.

7- Humpelekea mlaji kutawaliwa nayo (Addiction);

 8- Walaji wengi huvuta na sigara, hata yule aliyekuwa havuti kabla ya kuanza kula Mirungi, hujikuta akizama kwenye uvutaji, na madhara huwa maradufu.

 9- Madhara ambayo bado kinamama walaji Mirungi hawajagundua ni kwamba mtoto anayezaliwa na mama mlaji Mirungi mara nyingi hukataa kunyonya titi la mama yake kwa sababu ladha ya maziwa inabadilika kwa ajili ya utumiaji wa madawa (pesticides) unaotumiwa na wakulima wa Mirungi kama inavyoeleza utafiti uliofanyika na Chuo Kikuu Cha Aden (Aden University). Utafiti huo unazidi kueleza ya kwamba aina ya madawa yanayotumiwa na wakulima ni zaidi ya 118 (na nyingi katika hizo ni katika zile zilizokatazwa kisheria [illegal pesticides]) na ambazo zinasababisha asilimia 70 ya ugonjwa wa saratani (cancer) huko Yemen.

10- Utafiti mwengine kule Ethiopia unatueleza ya kuwa mtoto wa mama mwenye kula Mirungi kwa wingi huwa hana uzito wa kawaida wakati wa kuzaliwa.

11- Ukosefu wa hamu ya kula chakula na mengi mengine.

Madhara Ya Kiuchumi Na Kijamii

1-Kuwa na taifa la wavivu wapenda starehe wasiotumika.

2- Jamii ya Kiislamu iliyo chafu kimaadili na isiyosimamisha Ibada.

 Harakati za kunyanyua uchumi kua duni, harakati na juhudi zinazopatikana huwa ni za kuwazika na kutajika tu. Anapokuwa mtu amesha weka fundo lake la Mrungi kwenye shavu lake linalovimba kama pulizo kwa kujaa, hapo atakuwa anatoa mipango na mikakati mizito mizito ya kujenga maghorofa, kuanzisha miradi ya mamilioni..lakini yooote ni mipango inayopangwa na ‘Handas’ baada ya kutemwa gomba, mipango yote iliyokuwa ikipangwa huyeyuka na kuwa kama ngano za Alinacha….hapo tena husubiriwa siku ya pili ya kusagwa na mipango yake mingine ya mamilioni.

3- Kulala mchana kutwa na kukosekana harakati na michakato ya utafutaji riziki.

4- Kuzidi kwa omba omba, Bila shaka ikiwa watu hulala mchana mzima na hawahangaiki kufanya kazi, kinachotarajiwa ni kuzidi kwa wanyanyua mikono na wainamisha vichwa wanaoongea kwa huzuni kama waliofiwa wakati wanatupa makombora yao ya maombi.

5- Vijana wa mjini hawataki kuajiriwa kwa sababu wajiona kua  ni ma-alwatan, kwa mantiki hii haiwezekani kwao kutumwa au kuajiriwa! Matokeo yake uchumi wa wakazi wa mjini kuporomoka na mwisho wake ni wao kukodisha nyumba zao kwa wageni kwa wenye kuwa nazo,  Na hatima yake hufikia kuuza hizo nyumba ambazo wamerithi kutoka kwa wazee wao waliokuwa wakihangaika na kuchapa kazi, Na kwa wasokua na nyumba hulazimika kulala kwa majamaa na kua walalahoi.

6- Huwapelekea baadhi yao kujidunisha na kuwatumikia mabwana wakubwa si kwa lingine ila kwa ajili ya kilo ya Mirungi.

Kwa mantiki hii kutokana na maelezo na madhara ya Mirungi, Mirungi ni haramu katika Dini kwa sababu Mirungi inamadhara na kila kichokua na madhara Uislamu umekiharamisha.


پیام رهبر انقلاب به مسلمانان جهان به مناسبت حج 1441 / 2020
We are All Zakzaky
Hatuukubali muamala wa Karni