Mafunzo ya jamii

Historia ya Mirungi

  • Habari NO : 390341

Inaaminika kuwa Ethiopia ndio asli yake kuanzia karne ya 15, na ikaenea katika milima ya Afrika Mashariki na Yemen. Ingawa vilevile kuna wanaoamini kuwa ilianzia Yemen katika karne ya 13 kabla ya kuenea hadi Ethiopia na nchi za jirani.

Kutoka Ethiopia na Yemen, mti au mmea huo ulienea sehemu mbalimbali, Somalia, Sudan, Kenya, Tanzania, Uganda. Congo, Malawi, Zimbabwe, Zambia hadi Afrika ya Kusini.

Baadhi hudai kuwa matumizi yake yanarejea miaka ya nyuma sana tokea wakati wa Wamisri wa kale ambao inasemekana walikuwa wakiitumia kama madawa ya jadi kwa baadhi ya magonjwa.

Anaeleza mwandishi wa Kimalaysia ‘Abdullaah bin ‘Abdil-Qaadir kuwa alipokuwa Yemen mwaka 1854, aliona ada na tabia ya utafunaji Mirungi huko Al-Hudaydah. Anaeleza: “Niliona jambo la ajabu katika mji huu –kila mtu anatafuna majani kama mbuzi anavyokula akameza na kisha kucheua kisha hutafuna tena kile alichokicheua. Kuna aina ya tawi, si pana sana kiasi cha urefu wa vidole viwili, ngumu kiasi, watu hutumia aina hii ya tawi au jani na kutia mdomoni na hutumiwa na viambatanishio vingine kuila, tawi hili hutiwa lote mdomoni na kutafunwa. Wanapokuwa wengi na kula kwa pamoja, utaona mabaki ya majani hayo yamerundikana mbele yao. Wanapotema mate, mate yao huwa ya rangi ya kijani. Kisha nikawauliza kuhusu hicho wanachokula: ‘Ni faida gani mnayopata kwa kula majani hayo?’ Wakajibu, ‘Hakuna chochote, ni jambo tulilolizoea lenye kutugharimu ambalo tumekulia nalo’. Wale wanaokula majani haya inawabidi watumie sana mafuta na asali, kwani wasipofanya hivyo wanaweza kuugua. Hayo majani hujulikana kama Kad (Mirungi).”

Wasifu Na Kilimo Chake

Mirungi ni mti unaoota polepole ambao unakuwa kwa urefu wa mita 1.5 hadi mita 20, kutegemea na eneo kijiografia na pia hali ya mvua ya eneo. Likiwa na majani ya kijani yaliyokoza ambayo yana urefu wa sentimeta 5 hadi 10 na upana wa sentimeta 1 hadi 4.

Ina ladha ya uchachu mkali na utamu wa mbali kwa wakati mmoja. Hufungwa katika majani ya migomba ili kuhifadhi ubichi wake. Kawaida huvunwa asubuhi sana na kuuzwa mchana wake au usiku wake, kila inavyokaa sana hupunguza ubora wake kwa walaji na thamani yake. Na kwa sababu walaji wa Tanzania hutegemea zaidi Mirungi kutoka Kenya, huwa hawapati ule ubora unaotakikana kutokana na umbali na kutofika kwa haraka; ingawa walaji wa Arusha hupata haraka zaidi kwa ukaribu wake na Nairobi kuliko wale wa Dar na Zanzibar au miji ya bara ya mbali kama Mwanza na kwengineko.

Kwa hivyo, majani ya Mirungi yanapoanza kukauka, kemikali ile kali ya aina ya cathinone inakauka pia na inabakia ile ambayo sio kali: cathine, na ndio maana mirungi inaposafirishwa inawekwa katika mifuko maalum ya plastiki au kufunikwa na majani ya migomba ya ndizi ili ihifadhike vizuri.

Mirungi ni zao lenye kuwaingizia wakulima Yemen kipato kikubwa na ndio maana wengi wameanza kuacha kilimo cha kahawa, na hutumika asilimia 40 ya matumizi ya maji ya nchi nzima kwa kilimo chake, pamoja na uzalishaji wake kuongezeka kiasi cha asilimia 10 hadi 15 kila mwaka. Matumizi ya maji yamekuwa makubwa kiasi cha hifadhi ya maji ya San’aa mji mkuu wa Yemen kupungua na ikiendelea namna hii basi baada ya miaka kumi tu maji yatakauka na kwa hali hiyo imefikia serikali kugawa maeneo kwa kuwahamisha wakazi wa San’aa kwenda kuishi maeneo ya pwani ya Bahari nyekundu.

Matumizi ya Mirungi aghlabu hutumika katika maeneo yanayolimwa zaidi na maeneo ya jirani na yale ambayo hufika Mirungi haraka ingali bado mpya mbichi na safi kwa sababu ya mzimuo wake. Kila inavyokaa mzimuo wake na upandishaji wa ‘handasi’/ ‘nakhwa’ yake hupungua.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ya kwamba zaidi ya masaa 14.6 milioni yanapotezwa kila siku katika ulaji wa Mirungi huko Yemen. Ripoti hiyo, iliotolewa katika tovuti ya WHO, inaonyesha ya kwamba asilimia 80 ya watu wazima (male adults) wanatafuna Mirungi kila siku kwa muda wa masaa matatu mpaka manne hadi matano wakati ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wamo pia katika tabia hii yenye hatari.

Mirungi ni kileo kinachotumika sana kama ‘mkusanyiko wa kijamii’ katika maeneo mengi, na huwajumuisha zaidi wanaume ingawa baadhi ya sehemu na kwa miaka ya karibuni wanawake wamevamia sana uraibu huo haswa maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki kama Mombasa, Tanga na Dar-es-Salaam na mji kama Arusha ambao pia umekumbwa na ugonjwa huo kwa vijana wengi wa mjini. Na hupendelewa na madereva wa magari makubwa wanaosafiri safari ndefu, madereva wa abiria na hata wa magari ya kukodishwa kwa kuamini kuwa inawafanya wawe macho na makini. Vilevile hutumiwa na wanafunzi wakiamini kuwa inawafanya wasome muda mrefu na kukesha, kadhalika walinzi wa usiku huona inawasaidia kuwa macho usiku. Na baadhi ya watu hutumia kwa kisingizio cha kukesha kwa ajili ya kufanya ‘Ibaadah za usiku.

Nchi kama Tanzania, imepigwa marufuku lakini serikali kwa kutofuatilia kwa karibu kumefanya kuwe kunaliwa hadharani na bila woga wowote. Hufuatwa sheria pale maaskari wanapotaka kupata chochote kutoka kwa walaji na ni nadra kusikia mla Mirungi katiwa ndani, na akitiwa ndani basi hutolewa mara moja bila kufikishwa mahakamani.

Huko Somalia, waliposhika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na kuleta amani ambayo haikuwahi kuonekana Somalia, Baraza La Juu La Mahkama Ya Kiislam, walipiga marufuku kuliwa mwezi wa Ramadhaan na kusababisha maandamano na upinzani huko Kismayo. Na mwaka huo huo katika mwezi wa Novemba, Kenya ilipiga marufuku ndege kwenda Somalia wakitaja ni sababu za kiusalama, hali ambayo ilisababisha upinzani kutoka kwa walimaji Mirungi. Mbunge wa Ntonyiri, Meru ambayo ndio eneo lenye kutegemewa sana Afrika Mashariki kwa ulimaji wa Mirungi, alieleza kuwa imetengwa ardhi maalum ya kulimia Mirungi, ambapo tani 20 zenye thamani ya Dola Laki 8 ($800, 000) husafirishwa kila siku kuelekea Somalia na hivyo kizuizi cha serikali kitailetea taifa madhara ya kiuchumi na kipato kama hicho kwa siku.

Aina Zake

Alenle (yenye majani mapana mengi, na ni ghali) – Yemen, Ethiopia na Kenya

Kangeta – Kenya

Giza (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ndogo) – Kenya

Mbaga (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ya aina duni ambayo aghlabu ni ya bei ya chini -japo kuna baadhi ya mashamba machache sana hutoa aina yenye afadhali- na huliwa na wasiomudu kununua aina za ghali) – Tanzania

Majina yake

MIRUNGI, QAAT, KHAT, GHAT, GATI, MIRAA, GOMBA, MBAGA, VEVE, MTI, KIJITI, MAJANI, MAUA …

Mirungi au kama inavyojulikana kama Qaat au Qaadka huko Somalia, na Yemen huitwa au Al-Qaat القات ; ingawa kwa matamshi ya huko hutamkwa ‘Gaat’, Kadhalika Kenya kulingana na miji yake hujulikana kama; Miraa, Veve, Kijiti, Gomba n.k., na Tanzania ni maarufu kwa majina; Mirungi, Gomba, Gati, Miti, Majani n.k. kulingana na kila eneo na jina lake.

Mirungi au (Catha edulis) Ni mmea au mti unaoota au kuoteshwa kwa wingi sana huko Ethiopia, Yemen na Kenya.

Jani hilo ambalo Maulamaa wameeleza kua kulingana na madhara yake ni Haraam, Mirungi ni jani lenye madhara mengi katika siha ya mwanadamu na lenye kusababisha mengi katika madhara na maangamizi ya kimaadili na kijamii.

Matumizi ya mmea huo ambao hakika kwa masikitiko makubwa, yameenea zaidi katika jamii za Kiislamu na haswa maeneo ya mijini na zaidi kwa wanaojulikana kama ‘Waswahili.’

Ingawa neno ‘Waswahili’ asli yake ni neno la Kiarabu ‘Saahil’ ساحل pwani, mwambao na ‘Saahiliy’ -ya pwani, au mkaazi wa pwani au mwambao, ila neno hilo au jina hilo hivi sasa limegeuka kimatumizi na kuashiria zaidi kwa wale watu zaidi wa mtaani, wasiopenda kutumika; kufanya kazi, wasio wakweli, wapenda starehe, wasio na elimu, wazembe n.k. Kwa wasio Waislamu wao wanatumia jina hilo kuwaita nalo Waislamu, na zaidi wakikusudia sifa hizo tulizozitaja hapo nyuma. Na kadhalika Waislam kadhaa huwaita wenzao hivyo wakimaanisha, wasio na ahadi, wasemao uongo, wasioaminika, wajanja wajanja, wajuaji, na wenye maneno mengi wasioshindika.

Mirungi inakusanya ndani yake alkaloid iitwayo cathinone, amphetamine kama kichangamsho (stimulant) ambayo inasemekana husababisha msisimko, uchangamfu, kuwa na aina ya furaha ya kuwazika –kuhandasika- na huondosha hamu ya kula na kusababisha ukosefu wa usingizi.

Mnamo mwaka 1980 WHO (Shirika la Afya Duniani) liliiweka Mirungi katika fungu la madawa ya kulevya ambayo inasababisha nafsi kutawaliwa nayo au kuwa na uraibu (addiction) kwa daraja ya kati hadi ile yenye nguvu.

Mti huo umekuwa ukiandamwa na mashirika yenye kupinga madawa ya kulevya kama shirika liitwalo DEA (Drug Enforcement Administration). Shirika hilo katika mwaka 2006 Julai tarehe 26, shirika hilo katika operesheni iliyokuwa ikijulikana kama ‘Somalia Express’ ambayo katika upelelezi wake uliodumu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu ambao ulihusisha wanachama 44 wa kundi lililokuwa likisafirisha tani 25 za Mirungi ambazo zilikuwa na thamani ya Dola milioni 10 za Kimarekani kutoka Somalia kupelekwa Marekani. Shitaka (Kosa) hilo lilihusisha utoroshaji mkubwa kabisa wa Mirungi katika Historia ya Marekani.


پیام رهبر انقلاب به مسلمانان جهان به مناسبت حج 1441 / 2020
We are All Zakzaky
Hatuukubali muamala wa Karni