KUFUNGA MIKONO KATIKA SWALA

  • Habari NO : 400556

KUFUNGA MIKONO KATIKA SWALA NI BID'A SIO SUNNA YA MTUME (S.A.W.W).

 Waislaam wote huitekeleza ibada hiyo.Lakini tunaona kuna baadhi ya tofauti baina yao pindi wanapoitekeleza ibada  hii muhumu ambayo ni nguzo ya dini, utakuta hawa wakiswali katika hali ya  kufunga mikono yao, na wengine wakiswali katika hali ya kunyoosha mikono yao (au kuachia mikono yao).Hivyo kuna makundi mawili,la kwanza linafunga mikono katika swala,na la pili,linaachia mikono (yaani:Halifungi mikono) katika swala.Na makundi yote mawili yanadai yanajifunza kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) jinsi ya kuswali swala sahihi.!!

Je, ni kweli kwamba Mtume (s.a.w.w) aliswali katika aina hizo mbili kama wanavyoswali watu wa makundi hayo mawili,au aliswali katika aina moja wapo kati ya hizo mbili hapo juu.?!!Ni swali muhimu sana sana,itabidi kila amtu ajiulize swali hilo.Haingii akilini  Mtume (s.a.w.w) kusali mara kafunga mikono yake na wakati mwingine aswali akiwa amefungua (ameachia) mikono yake,maana akifanya hicho atakuwa anauchanganya umma wake na utashindwa kujua ni ipi swala sahihi,ile inatakiwa kufunga mikono ndani yake au inayotakiwa kuachia (na kunyosha) mikono ndani yake.??!!

Sisi twapenda sana kupita pita katika baadhi ya mitandao na tovuti mbali mbali tukitafuta faida.Alhamdulillah leo hii tumepata faida maana tumekutana na tovuti moja ya Kiislaam, katika kupekua pekua ndani ya tovuti hiyo tukakutana na mada moja iliyokuwa ikizungumzia kuhusiana na suala la Kufunga mikono katika Swala.Mhariri au muhusika katika maudhui hii amejaribu kuthibitisha kuwa Kufunga mikono ni Sunna iliyothibitika kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na kwamba Mtume (s.a.w.w) kasisitiza jambo hilo!. Kaleta Riwaya kadhaa ili kuthibitisha hilo ingawa "hakufanikiwa" kuleta riwaya hata moja inayozungumzia kuachia mikono katika swala ili kuibatilisha na hatimae kuthibitisha alichotaka kukuthibitisha. Kataja hadithi zinazoonekana kuthibitisha kufunga mikono tu katika swala,' ama zile zilizopinga kufunga mikono hajataja hata moja ili kuonyesha udhaifu wake na kuibatilisha!. Ili kuwa vizuri sana angetaja hata zile riwaya zinazosemekana zinaharamisha kufunga mikono au kupinga kufunga mikono katika swala kisha azibatilishe na baada ya kuzibatilisha kwa dalili zinazoeleweka kiakili, basi iwe  ni fursa nzuri ya kuthibitisha hadithi zake alizoshikamana nazo ili kuthibitisha kuwa jambo hilo ni Sunna ya Mtume (s.a.w.w).

Na angelikuwa amebahatika kufanya hivyo, basi Msomaji angeweza kuelewa moja kwa moja kuwa hakuna riwaya sahihi inayopinga kufunga mikono katika swala.Huwezi kuongea na mtu mwenye akili kama vile mtoto! Lazima umuheshimu walau kidogo kwamba naye ana fikra na ana uwezo wa kuelewa unachokizungumzia.! Ukifanya hivyo utakuwa umeenda sawia na Ubindamu wa Mwanadamu. Hilo ukilitambua, basi utajitahidi kuandika mambo yanayoingia akilini na hutakimbilia kusema "Hakuna hadithi sahihi" bila ya kuonyesha usahihi wa kauli yako hiyo!.

Unapotaja riwaya zinazothibitisha kufunga mikono hiyo sio dalili ya kwamba riwaya zinazopinga hilo na sahihi hakuna! Lakini dalili ni kuzitaja riwaya hizo unazoziona ni dhaifu kwa mtazamo wako au kulingana na ulivyoelewa kisha kuzibatilisha kisomi zaidi, hiyo ndio dalili ya kukataa riwaya kuwa sio sahihi na hivyo ndivyo riwaya zinavyokataliwa.Sio unaamua tu na kusema "Riwaya sahihi ya kunyoosha mikono katika swala hakuna"! Unadhani nani atakubali kauli hiyo kavu bila dalili  ?!

Kuna hadithi za kufunga mikono na hadithi zinazosema kufunga mikono ni haramu na si sunna ya Mtume (s.a.w.w) bali suala hilo limezushwa baada ya Mtume (s.a.w.w) na kunasibishwa kwake!. Kielimu na kiungwana zaidi, ukitaka kuthibitisha hadithi zinazozungumzia kufunga mikono inabidi uweke mezani hadithi zote zinazothibitisha na zinazopinga, kisha ubatilishe zile zinazopinga "kwa mtazamo wako" ili baada ya kuzibatilisha uweze kuthibitisha zile zinazothibitisha "kwa mtazamo wako". Hapo utakuwa umefanya Uadilifu Kielimu na utaeleweka kwa haraka zaidi.

Lakini mhariri wetu inaonekana Hadithi au Riwaya zinazopinga kufunga mikono katika swala hajawahi kuziona! ispokuwa alizoziona tu ni zile zinazosema kufunga mikono katika swala ni Sunna. Na ndio maana moja kwa moja akaanza kwa kusema na hapa namnukuu:

(( "Hakuna ushahidi wala dalili wala mapokezi sahihi yoyote yanayoonyesha kinyume na kufunga mikono kwenye Swalah kutoka kwake yeye Mtume wala Maswahaba zake".))  Mwisho wa kumnukuu.

Mhariri katumia "kauli hii kama ilivyonukuliwa" ili kuthibitisha anachokiitikadia yeye maana anachotaka kukithibitisha katika maudhuu hii ni kufunga mikono katika swala,ama zile riwaya zinazokataa na kupinga suala hilo na kusema limezuka baada ya Mtume (s.a.w.w), kwa upande wa mhariri zinathibitisha jambo asiloliitikadia,hivyo akaamua zote hizo kuzibatilisha kirahisi tu kwa kauli yake moja isiyokuwa na dalili na wala hoja kwa akisema:

"Hakuna ushahidi wala dalili wala mapokezi sahihi yoyote yanayoonyesha kinyume na kufunga mikono kwenye Swalah kutoka kwake yeye Mtume wala Maswahaba zake".!

Napenda kumsaidia jibu ndugu mhariri na kumuweka sawa ajue kwamba hadithi hizo alizozitaja sio sahihi bali Mtume wa Mwenyeezi Mungu (s.a.w.w) hajasema hivyo bali jambo hilo wamelinasibisha kwake ili likubalike kuwa ni sunna yake (s.a.w.w), hadithi au riwaya hizo ni dhaifu pande zote, ukija kwenye matini ya riwaya zenyewe zinatosha kuthibitisha udhaifu wake, ukija kwenye sanadi ya riwaya hizo, huko tena ndio balaa.!

Lakini kabla ya majibu yetu, hebu kwanza nikunukulie nilichokikuta kwenye Tovuti hiyo hapa chini.Katika tovuti hiyo, mhusika alianza namna hii na hapa namnukuu.

MWANZO WA KUNUKUU KTK TOVUTI YA ALHIDAAYA.COM:

Kufunga Mikono Katika Swalah

Kufunga mikono katika Swalah ni Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ni jambo alilolisisitiza sana katika Swalah na hata kuwasahihisha wale waliokuwa wakikosea kufunga mikono yao ndani ya Swalah. Isitoshe ni Sunnah sahihi iliyothibiti hata kwa Mitume waliotangulia kama anavyotujulisha mwenyewe Mtume katika Hadiyth zifuatazo hapo chini.

Hakuna ushahidi wala dalili wala mapokezi sahihi yoyote yanayoonyesha kinyume na kufunga mikono kwenye Swalah kutoka kwake yeye Mtume wala Maswahaba zake.

Hadiyth Za Kufunga Mikono

Ama Hadiyth zinazoeleza juu ya Kufunga mikono ni nyingi sana na zinapatikana katika kitabu 'Swifatu Swalaat An-Nabbiy' cha Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) kilichopo ndani ya ALHIDAAYA kwa lugha ya Kiswahili Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam). Na pia ndani ya kitabu cha 'Al-Qawl Al-Mubiyn fiy Akhtwaa Al-Muswalliyn) kilichoandikwa na Shaykh Mash-huur Hasan Salmaan na pia ndani ya kitabu cha Fiqhus Sunnah cha Sayyid Saabiq na kwenye kitabu cha Swahiyhu Fiqhus Sunnah cha Abu Maalik Kamaal kilichopo ALHIDAAYA Swahiyh Fiqhus Sunnah na ndani ya vitabu vingi sana vya Fiqh na vya Hadiyth sahihi.

Anasema 'Bahari ya elimu' Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa;
"Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;
"Sisi Mitume tumeamrishwa kuharakisha kula futari zetu na kuchelewesha kula daku letu, na kuweka mikono yetu ya kulia juu ya kushoto ndani ya Swalah." At-Twabaraaniy na Ibn Hibbaan
Na katika Sunan za Abu Daawuud Hadiyth iliyosahihishwa na Ibn Khuzaymah inasema;

"Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto."

Imepokelewa pia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona mtu mmoja akiswali huku ameweka mkono wake wa kushoto juu ya mkono wa kulia, akauondoa na kuuweka wa kulia juu ya kushoto." Ahmad na Abu Daawuud.
Na imepokelewa kutoka kwa Swahaba Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa katika Swalah ya maiti Mtume wa Mweyezi Mungu alinyanyua mikono yake juu akasema 'Allahu Akbar', kisha akauweka mkono wake wa kulia juu ya wa kushoto."
At-Tirmidhiy katika ‘Baab maa jaa fiy raf’il yadayni.’

Imepokelewa katika Swahiyh Muslim na kutoka kwa Imam Ahmad na At-Twabaraaniy kuwa:

"Na alikuwa akiuweka mkono wake wa kulia juu ya sehemu ya nyuma (mgongo) ya mkono wa kushoto."
Katika mlango huu zimepokelewa Hadiyth zaidi ya ishirini kutoka kwa Maswahaba kumi na nane pamoja na waliowafuatilia (Taabi’iyn), zote hizo zikitoka moja kwa moja  kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
Kutoka kwa Swahaba Waail bin Hujr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema;

"Kama kwamba namtazama Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) namna alivyokuwa akiswali", akasema:

"Nikamtazama! akatoa takbiyr, kisha akanyanyua mikono yake mpaka ikakaribia masikio yake, kisha akauweka wa kulia juu ya upande wa nyuma wa mkono wa kushoto."

Ibn Khuzaymah katika sahih yake na An-Nasaaiy na Abu Daawuud katika Sunan yake na Ahmad katika Musnad yake 4/318 na Ibn Maajah katika Sunan yake 1/266 na Ad-Daarimiy katika Sunan yake 1/314 na Ibnul Jaruud katika Al-Muntaqaa Hadiyth nambari 208 na katika vitabu vingi vingine".
Anasema Imaam Maalik (Allaah Amrehemu) katika kitabu cha Al-Muwattwaa, na huyu ni Imaam wa watu wa Madiynah mji alioishi na kuswali ndani yake Mtume wa Allaah zaidi ya miaka kumi, na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakaendelea kuswali hapo miaka mingi iliyofuata.
Katika ukurasa wa 122 na 123 mlango wa "Mwenye kuswali aweke mkono mmoja juu ya mwengine",  imeandikwa katika kitabu hicho cha Imaam Maalik katika Hadiyth nambari 133 kama ifuatavyo:
"Katika maneno ya Mitume ni kuwa usipokuwa na haya basi fanya utakalo, na pia (katika maneno ya Mitume) ni kuweka mkono mmoja juu ya mwengine katika Swalah."
Haya ni maneno ya Imaam Maalik ndani ya kitabu chake cha Al-Muwattwaa.
Na katika kitabu hicho hicho cha Al-Muwattwaa Imaam Maalik ameandika Hadiyth kutoka kwa Sahl bin Sa’ad Al Saa’idiy kuwa:

“Watu walikuwa wakiamrishwa kuweka mkono wao wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika Swalah."
Anasema Abu Haazim;

"Naelewa kuwa anakusudia hapa wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)". Al-Bukhaariy Juz. 1 ukurasa wa 397 Imaam Maalik katika Al-Muwattwaa na Imaam Ahmad katika Musnad.

Na katika kuisherehesha Hadiyth hiyo amesema Imaam Maalik (Allaah Amrehemu);

"Kuweka (mkono) wa kulia juu ya kushoto na kuharakisha futari na kuchelewesha daku."

Haya ameyasema katika kuisherehesha Hadiyth iliyotangulia ya Abul Mukhariq.

Baadhi ya watu wakasema kuwa katika Hadiyth iliyomo ndani ya Al-Muwattwaa yumo Abul Mukhariq na huyu anajulikana kuwa ni dhaifu katika elimu ya Hadiyth, lakini inaeleweka pia katika elimu ya Hadiyth kuwa udhaifu wa wapokezi unakhitalifiana darja, na kwamba daraja inayokubalika Hadiyth zao katika madhaifu ni wale waliodhoofishwa kwa ajili ya udhaifu wao wa kuhifadhi ikiwa wao si watu waongo wala si wenye kupenda kuongeza maneno.

Madhaifu wa aina hii anasema Dr. Muhammad Ajjaaj Al-Khatwiyb katika kitabu chake cha 'Al-Mukhtasar Al-Wajiyz fiy Uluum Al-Hadiyth kuwa;

"Mtu aliyedhoofishwa kwa ajili ya kuhifadhi kwake, au kwa ajili ya kutoweza kudhibiti maneno vizuri, ikiwa hatuhumiwa kwa ila nyingine, na ikiwa zitapokewa Hadiyth zake kwa njia nyingi, basi Hadiyth itapanda na kufikia darja ya Hadiyth 'Hasan', na kwa ajili hiyo udhaifu wake unatoweka kwa kupokelewa Hadiyth kwa njia nyingine."

Anasema Imaam Muhammad bin Al Hassan Al Shaybaniy kuwa;

"Anatuhumiwa Abul Mukhariq kwa udhaifu wake wa kuhifadhi tu."

Isitoshe ndani ya kitabu hicho cha Al-Muwattwaa ipo pia Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) na kunukuliwa pia na Maimaam Ahmad na Al-Bukhaariy na wengineo, inayosema;

"Watu (wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) walikuwa wakiamrishwa kuweka mikono yao ya kulia juu ya kushoto katika Swalah."

Je, Imaam Maalik Alikuwa Akiaachia Mikono Na Alisema Watu Waachie Mikono Kwenye Swalah?

Yaliyoandikwa ndani ya kitabu cha Bidaayatul Mujtahid si kukanusha kufunga mikono bali ni kuthibitisha, isipokuwa tu imenukuliwa ndani ya kitabu hicho kuwa Imaam Maalik amejuzisha kufunga katika Swalah ya Sunnah na hakujuzisha katika Swalah ya Fardhi akihofia watu wasiwe wanafunga kwa ajili ya kujipumzisha tu na wasidhani kuwa ni nguzo mojawapo ya Swalah na kwamba Swalah inabatilika iwapo mtu atafanya kinyume cha hivyo (hii ikiwa kweli imethibiti kuwa Imaam Maalik amesema hayo), lakini yaliyomo ndani ya kitabu chake cha Al-Muwattwaa ni kinyume na hayo yaliyoelezwa.

Na yanayofanywa na baadhi ya wafuasi wa Imaam Maalik wanaoachia mikono kwenye Swalah zao kama wafanyavyo baadhi ya watu wenye itikadi zisizo za Ahlus Sunnah wal Jama’ah, ni jambo ambalo halina dalili kwenye Sunnah ya Mtume wetu, wala Maswahaba zake wala hata Imaam Maalik mwenyewe.

Hivyo, tumeona kuwa hapana Hadiyth sahihi hata moja kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema watu waachie mikono katika Swalah au kuonyesha kuwa Mtume alikuwa akifanya kinyume na kufunga mikono kwenye Swalah, na hii ni kauli ya wengi sana katika Maswahaba na Taabi’iyna (Radhiya Allaahu ‘anhum) na haya ndiyo aliyonukuu Imaam Maalik katika Al-Muwattwaa.

Na Allaah Ni Mjuzi Zaidi.

MWISHO  WA KUNUKUU

 

JIBU LA KWANZA:

Tambua kwamba Mas'ala hii ya "kufunga mikono katika swala" au "kufungua (yaani kunyoosha au kuachia) mikono" katika swala", ni mas'ala ambayo wanazuoni wa Ahlul-sunna wamekhitilafiana.kuna baadhi yao wamesema inajuzu na wengine wakasema ni Mustahabu. ni kauli mbili tofauti,anayesema inajuzu kauli yake inatofautiana nay a yule anayesema ni mustahabu,hilo liko wazi Mfano: Maliki amesema "Inajuzu",lakini Mustahabu ni kuachia mikono katika swala ya faradhi".Hambali,Shafii Hanafi wao wakasema kufunga mikono katika swala ni mustahabu,lakini wakatofautiana sehemu ya kuiweka mikono hiyo.Hanafi akasema ni sunna kwa mwanaume aweke mikono yake baada ya kufunga chini ya kitovu chake,na mwanamke aiweke kwenye kifua chake,Shafii akasema: Ni sunna kwa mwanaume na mwanamke baada ya kufunga mikono waiweke chini ya kifua na juu ya kitovu,Ama Hambali yeye anasema jambo hilo ni sunna na bora zaidi baada ya kufunga mikono basi iwekwe chini ya kitovu.Pia wote kwa ujumla wamekubaliana na kuafikiana kuwa kufunga mikono katika Swala sio Wajibu.Hakuna mwanazuoni hata mmoja anayesema jambo hilo ni Wajibu katika swala.

Hivyo tunapozidurusu riwaya hizo hapo juu kama alivyozileta mwenye kutetea kufunga mikono, lazima tufaidike (kutoka katika riwaya hizo) na mambo mawili tu na wala hakuna la tatu:

*Lakwanza: IMma tufahamu kuwa Riwaya hizo zinathibitisha Wujub kwamba Jambo hilo ni wajibu.

*La pili: Au tufahamu Istihbaabu kwamba Riwaya hizo zinathibitisha kuwa jambo hilo ni mustahabu.

Ama jambo la kwanza tumeelewa kwamba hakuna A'limu wala mwanazuoni yeyote anayesema kufunga mikono ni mustahabu, hivyo kauli hiyo ni batili.

Ama jambo la pili,likithibiti kuwa jambo hilo ni mustahabu,basi haitakiwi na sio haki kumlaumu wala kumnyoshea kidole yule atakayenyoosha au kuachia mikono yake katika swala kwa sababu hajaacha wajibu bali kaacha mustahabu,na anayeacha mustahabu haitwi Mub'diu,yaani haitwi kuwa kafanya bid'a na kuingiza katika swala lisilokuwa ndani ya swala,ispokuwa hatapata thawabu za kufanya mustahabu.kwa hiyo hautakiwi kumuita kafiri wala kumuita mub'diu maadamu hajaingiza katika swala lisilokuwa katika swala,ingelikuwa kufunga mikono ni wajibu,kisha mtu akanyosha mikono,hapo ni haki kusema fulani kaingiza katika swala lisilokuwa ndani ya swala,hivyo hii itakuwa ni bid'a na bid'a ni haramu.Mfano:Kuweka hina katika ndevu ni mustahabu,lakini mtu akiamua kutoweka hina katika ndevu zake,hutakiwi kusema fulani kafanya bid'a na kumnyoshea kidole na kumuita kafiri kwa jambo la mustahabu,hivyo hivyo katika suala la kufunga mikono,atakayeamua kunyoosha mikono kwa kujua kuwa kufunga sio wajibu, hutakiwi kumtuhumu na kuona swala yake si sahihi.Hili ni jibu namba moja.

JIBU LA PILI:

Umesema kwamba hakuna riwaya sahihi inayokataza kufunga mikono au inayosema kunyoosha mikono ndio sahihi katika swala! Lakini tunaona katika baadhi ya wanazuoni katika Fat'wa zao wanafutu kwa kusema kunyoosha mikono ndio sahihi,nakufunga mikono si sunna bali sunna ni kunyoosha mikono,na wafuasi wao wananyoosha mikono katika swala zao,mfano mzuri ni Malik rai yake ni kunyoosha mikono na sio kufunga mikono.Sasa unaposema hakuna riwaya sahihi kinyume na kufunga mikono bali sahihi ni hizo ulizozileta au ulizozitaja hapo kuthibitisha kufunga mikono,huoni kwamba kauli yako hiyo inawadhalilisha baadhi ya wanazuoni wakubwa kwamba hawakujua kuwa hadithi sahihi ni hizo ulizozitaja na hatimae wakashikamana na hadithi nyingine zilizowalazimu kutoa Fat'wa ambayo inapingana na Sunna ya mtume (s.a.w.w)? Kwa mujibu wa kauli yako Malik ambaye hakubali kufunga mikono katika swala na ambaye alikuwea akichukizwa sana na jambo hilo, ina maana alikuwa Jahili (mjinga),alishindwa kufahamu riwaya zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) zinazosema kufunga mikono ni sunna katika swala!? Hili haikubaliki maana hakuwa mjinga kiasi hicho bali tunaheshimi rai yake maana hakutoa rai hiyo ispokuwa baada ya kuzidurusu riwaya hizo, hivyo hajakurupuka kutoa fat'wa ya kunyoosha mikono.au tuseme Malik alijua kuwa riwaya hizo zinathibitisha sunna ya Mtume (s.a.w.w) lakini amepinga kwa mapenzi yake na kuchagua kunyoosha mikono kuwa ndio sahihi?! Na ihtimaali hii ikiwa ni sahihi, basi Maalik atakuwa alifanya khiana na alikuwa na lengo la kupoteza sunna ya Mtume (s.a.w.w) kwa kwenda kwake kinyume na sunna!. Itabidi umbebeshe Maalik moja kati ya hayo mawili kwa mujibu wa kauli yako kwamba kufunga mikono katika swala ndio sahihi na hakuna riwaya sahihi kinyume chake.kiasi kwamba anayeshikama na riwaya dhaifu nakusema kunyoosha mikono katika swala ndio sahihi kama alivyosema Maalik na kama wanavyofanya wafuasi wa Maalik,basi mtu huyu atakuwa na uewewa mdogo wa kufahamu riwaya na hadithi za Mtume (s.a.w.w) au anafahamu lakini anafanya khiana.utakuwa umembebesha mzingo huo,ima yote mawili au moja wapo.

JIBU LA TATU:

 Mhariri anasema kwamba Maalik katika kitabu chake kiitwacho: Al-Muwattwaa, "Amesema" : !!

"Katika maneno ya Mitume ni kuwa usipokuwa na haya basi fanya utakalo, na pia (katika maneno ya Mitume) ni kuweka mkono mmoja juu ya mwengine katika Swalah."

Kwanza kabisa hiyo sio kauli ya Maalik bali Maalik alikuwa anapokea Riwaya, hivyo ilitakiwa useme hivi: Maalik "Amepokea" katika kitabu chake kiitwacha Al-Muwattwaa: , sio usema Maalik amesema ! Hii inamaana unanasibisha kauli hiyo kwa Maalik wakati si kauli yake bali amenukuu kauli hiyo na hivyo yuko katika hatua ya kupokea riwaya na sio kusema yeye kama yeye kwa mtazamo wake.Amepokea na Amesema ni vitu viwili au kauli mbili tofauti zenye maana tofauti!.Hiyo hadithi uliyoitaja alikuwa anapokea Riwaya inayozungumzia kufunga mikono katika swala si kwamba alikuwa anathibitisha au anatoa Fat'wa kwamba kufunga mikono ni sunna katika swala. Hilo Mosi.

Pili; Katika kitabu cha Maalik kiitwacho Al-mudawanaati, Hichi ni kitabu kilichokusanya Fat'wa za Malik, Maalik amekataa kuuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika swala, akasema kwa kauli yake na hapa namnukuu:

"Silijui jambo hilo katika Faradhi".

 Pengine utaniambia- mbona katika kitabu chake kingine kiitwacho Al-muwataa amepokea riwaya ya kukunja au kufunga mikono? najua hilo swali utakuwa nalo na utajiuliza kwanini katika kitabu hiki amepokea Riwaya ya kufunga mikono na katika kitabu chake kingine akatae jambo hilo kwa kusema ;"silijui jambo hilo katika Faradhi" ? Kwa nini Maalik alifanya hivyo ina maana alikuwa anajipinga mwenyewe?!

Hapana sio hivyo, Maalik hajajipinga bali wachache wanashindwa kuelewa tukio hilo, ukweli ni kwamba:

Kitabu cha Maalik kiitwacho Al-Muwattwa ni Kitabu cha RIWAYA, Maalik hana kitabu hicho tu, bali anacho kitabu kingine kinachoweka wazi mtazamo wake na rain a fat'wa zake kulingana na alivyoelewa na kufahamu Riwaya.Hivyo anaweza kuipokea riwaya hiyo katika Kitabu chake khaasi kwa ajili ya Riwaya lakini asiikubali riwaya hiyo wala kutoa Fat'wa kutumia Riwaya hiyo.Kupokea riwaya haimaanishi kwamba unaikubali! Na ndio maana katika kitabu chake kingine khaasi kwa aliji ya Fat'wa zake kiitwacho: Al-mudawanaati, hakuitumia riwaya hiyo alipotaka kutoa fat'wa kuhusu jambo hilo bali akaenda kinyume na Riwaya hiyo akifutu mas'ala hii kwa kutoa fat'wa ya kunyoosha mikono katika swala na sio kufunga mikono katika swala.

Hivyo utakapoona riwaya katika kitabu chake hicho cha riwaya, usihukumu moja kwa moja pasina kujua riwaya hiyo anaikubali au haikubali,kwani kuipokea katika kitabu chake haimaanishi anaikubali,inatakiwa kuangalie fat'wa zake anasemaje,maana ikiwa riwaya anaikubali basi ataitumia kutoa fat'wa na kuthibitisha mtazamo wake ambao tunauita fat'wa baada ya kupokea riwaya na kuichunguza kisomi zaidi ili kujua usahihi wake na udhaifu wake,ukiaona katika kitabu chake cha fat'wa zake hakuitumia riwaya hiyo,bali katoa fat'wa kinyume na riwaya aliyoipokea katika kitabu chake cha riwaya,basi jua kwamba huo ndio mtazamo wake na hiyo ndio fat'wa yake kulingana na alivyozidurusu na kuzifahamu riwaya zilizopokelewa kuhusu maudhuu husika.hapa nikitaza naona mhariri wetu wa Alhidaaya hajafahamu kama Maalik ana kitabu kingine kilichokusanya mtazamo wake na fat'wa zake kulingana na ijtihaadi yake aliyoifikia katika mas'ala.na ndio maana ndugu mhariri akaona kuipokea riwaya katika kitabu chake cha A-lmuwatta ni dalili ya kuonyesha kuwa anakubali na kuthibitisha jambo hilo kuwa ni sunna katika swala!! Lakini ufahamu huu ni makosa makubwa sana na sio sahihi maalik anapinga riwaya hiyo ingawa kaipokea katika kitabu chake, lakini yeye maalik hajsema popote kwamba riwaya nilizozipokea kwenye kitabu change hichi ni sahihi na nazikubali, ingelikuwa kasema hivyo mahala popote pale, basi ingelikuwa ni haki kusema maalik anakubali kufunga mikono katika swala kwa dalili ya kupokea riwaya hiyo kwenye kitabu chake.

Ndugu msomaji, Ili unielewe zaidi nikisemacho, jaribu kufuatilia kitabu cha Malik kiitwacho Al-muwatta na kile cha fat'wa kiitwacho Al-mudawanaati, utakuta kuna tofauti kubwa sana kati ya riwaya zake zilizopo katika kitabu chake al-muwatta na fat'wa zake zilizopo kwenye kitabu chake cha fat'wa Al-mudawanaati.Ukiona Fat'wa yake imepingana na riwaya aliyoipokea, basi jua riwaya hiyo haikubali na kama angelikuwa anaikubali basi fat'wa yake ilitakiwa iende sawia au ioane na riwaya aliyoipokea.Kupokea riwaya sio kutoa fat'wa,na fat'wa inaweka wazi mtazamo wako kuhusiana na riwaya hiyo.

Hivyo Maalik anaposema: "Silijui jambo hilo katika Faradhi" kauli hii inaonyesha au inajulisha kwamba Matendo ya watu wa Mji huo wa Madina ni tofauti kabisa na jambo hilo la kufunga Mikono, bali hawatendi au hawafanyi hivyo katika faradhi, katika kauli hiyo "Silijui jambo hilo katika Faradhi"

Maana inayofahamika ni kwamba Maalik halijui hilo (la kufunga mikono) kutoka katika matendo ya Maimam ambao walikuja baada ya Maswahaba na wakachukua elimu toka kwa Maswahaba.

JIBU LA NNE:

Mhusika katika Tovuti ya Alhidaaya.com ametaja riwaya ili kuthibitisha kufunga mikono kwa kusema na hapa Namnukuu:

 (("Haya ni maneno ya Imaam Maalik ndani ya kitabu chake cha Al-Muwattwaa.
Na katika kitabu hicho hicho cha Al-Muwattwaa Imaam Maalik ameandika Hadiyth kutoka kwa Sahl bin Sa’ad Al Saa’idiy kuwa:

“Watu walikuwa wakiamrishwa kuweka mkono wao wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika Swalah."
Anasema Abu Haazim;

"Naelewa kuwa anakusudia hapa wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)". Al-Bukhaariy Juz. 1 ukurasa wa 397 Imaam Maalik katika Al-Muwattwaa na Imaam Ahmad katika Musnad.)) Mwisho wa kumnukuu. 

Kabla ya kujibu hebu kwanza tuiandike riwaya hiyo kwa Lugha ya Kiarabu kama ilivyo kisha Kiswahili chake, riwaya kaipokea Bukhari namna hii:

روی البخاري عن أبي حازم عن سهل بن سعد، قال:

((کان الناس يُؤمرون أن يضعَ الرجل اليد اليمنی علی ذراعِه  اليسري في الصلاةِ))، قال حازم: لا أعلمُهُ إلا يَنمي ذلک إلی النبي (صلی الله علیه وآله وسلم ).
Bukhari amepokea kutoka kwa Haazim kutoka kwa Sahl bin Saa'd, amesema:

"Watu walikuwa wakiamrishwa kuweka mkono wao wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika swala)), Haazima akasema: "Silijui hilo ispokuwa  analinasibisha hilo kwa Mtume (s.a.w.w)."

Hii ndio maana ya riwaya kwa Kiswahili.

قال إسماعيل: لا أعلمهُ إلا يُنمي ذلک إلی النبي (صلی الله علیه وآله وسلم ).

Ismail amesema: "Silijui hilo ispokuwa 'linanasibishwa' hilo kwa Mtume (s.a.w.w)."

Ismail Hakusema: 

(  يَنمي ذلک إلی النبي (صلی الله علیه وآله وسلم ).

" ……..'Analinasibisha' hilo kwa Mtume (s.a.w.w)."

Riwaya hii inajulisha jinsi ya uwekaji wa mikono (yaani: keyfiyyatul-wadh-u) haijulishi kwamba riwaya hiyo imepokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na hakuna dalili juu ya hilo.Na ushahidi juu ya hilo kwamba riwaya haionyeshi kuwa imetoka au imepokelewa toka kwa Mtume (s.a.w.w) ni kulinga na uchambuzi huu ufuatao:

Uchambuzi namba moja: Lau ingelikuwa Mtume (s.a.w.w) ndiye aliyeamrisha Kufunga mikono katika swala, basi nini maana ya kusema: "Watu walikuwa wakiamrishwa"! Kilichomkataza Sahl bin Saa'd kusema: Mtume (s.a.w.w) "alikuwa anaamrisha" ni nini? ! Kama kweli ilikuwa ni amri ya Mtume (s.a.w.w) je, si ingelikuwa ni sahihi aseme: Mtume (s.a.w.w) "alikuwa akiamrisha watu….."?! Kuliko kusema "Watu walikuwa wakiamrishwa"?! ni kauli ipi kati za hizo mbili inayoingia akilini kwamba kauli hii inathibitisha kuwa jambo hilo kaliamrisha Mtume (s.a.w.w)?!

Kwa hakika kauli ya kwamba (Watu walikuwa wakiamrishwa…..) ni dalili tosha kwamba hukumu hiyo ya kufunga mikono katika swala ilizuka baada ya Maisha ya Mtume (s.a.w.w) kwani Makhalifa, Viongozi pamoja na Watawala wote zama hizo walikuwa wakiwamrisha Watu kufunga mikono wakidhani na kuchukulia kwamba jambo hilo linalodhidhihirisha "unyenyekevu zaidi" ,na ndio maana Bukhari akaweka Mlango makhsusi kuhusiana na hilo akauita "Mlango wa Unyenyekevu" au : (Baabul-Khushuu).Ibn Hajar yeye anasema: Hekima ya kitendo hicho (yaani kufunga mikono) ni kuonyesha kwamba Muombaji ni dhalili,na kiko karibu zaidi na unyenyekevu,Bukhari alichukua Fikra hiyo na akaweka mlango khaasi aliouita (Baabul-Khushuui) yaani "Mlango wa Unyenyekevu".

 Uchambuzi namba mbili: Chini ya Sanadi hiyo, kuna kitu au dalili inayojulisha kwamba jambo hilo la kufunga mikono katika swala, ilikuwa ni amri ya watawala (hivyo Watawala wenye kutoa amri ndio Waamrishaji na Watu ndio Waamrishwaji)  sio Mtume (s.a.w.w) mwenyewe aliyeamrisha,na hii ni kulingana na kauli ya Ismaili ((Namaanisha Ismail bin Abi Uwaysi ambaye ni Shekh wa Bukhari kama Humaydiy alivyothibitisha hilo, hebu tazama Fathul-baariy: Juzu ya 5, Ukurasa wa 325.) :        قال اسماعيل:(( لا أعلمهُ إلا يُنمي ذلک إلی النبي (صلی الله علیه وآله وسلم )   ))     ikiwa kitendo tutakisoma kwa "Swigha ya Majhuul" au "kauli ya kutendwa" ( Passive Voice).Na maana ni kwamba:Haelewi kwamba jambo hilo ni Sunna katika Swala ispokuwa suala hilo (au jambo hilo) linanasibishwa kwa Mtume (s.a.w.w), Hivyo analolipokea Sahl bin Saa'd katika Riwaya hiyo Halikubaliki.!

Ibn Hajar amesema: Mpokezi anaposema: ينميه)) Maana yake: Hilo analinasibisha kwa (na kumbambikizia) Mtume (s.a.w.w).

((Tazama: Ibn Hajar, Fathul-baariy fiy Sharhi Swahiyhul Bukhaariy, Juzu ya 2/ukurasa wa 224, katika Mlango wa "kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto")).

Hivi ndivyo riwaya hiyo inavyokuwa dhaifu ikiwa kitendo tutakisoma kwa "SWIYGHA YA MAJHUULI" au "Passive Voice", ama kitendo hicho tukikisoma katika "Swiygha ya Maaluum"  au "Kauli ya Kutenda"  (Active Voice) kama alivyosema Haazima katika Riwaya:

((يَنمي ذلک إلی النبي (صلی الله علیه وآله وسلم))

  , basi maana yake itakuwa namna hii kwamba Sahl bin Saa'd Analinasibisha hilo kwa Mtume (s.a.w.w), hivyo tukichukulia kwamba kukisoma kitendo hicho kwa Swiygha hii (Active voice) ndio sahihi na kwamba riwaya hiyo ikubalike! , bado ishkeli itabaki pale pale na riwaya itabi kuwa dhaifu, kwani kauli hii:  ((………..:(( لا أعلمهُ إلا "Silijui hilo ispokuwa…….." Inajulisha udhaifu wa kuvumisha na kunasibisha jambo hilo kwa Mtume (s.a.w.w) na kwamba jambo hilo kalisikia toka kwa mtu mwingine na "hajulikani ni nani".

Kwa mujibu wa dalili hizi mbili au uchambuzi huu namba moja na namba mbili, riwaya hii hatuwezi kushikamana nayo kuthibitisha kwamba kufunga mikono ni sunna ya Mtume (s.a.w.w) na kwamba hiyo ilikuwa amri yake (s.a.w.w).

Lakini Mhariri alipoitaja riwaya hii katika mtandao wake wa ALHIDAAYA.COM, akitoa tarjuma kwa Kiswahili alisema namna hii na  hapa namnukuu:

“Watu walikuwa wakiamrishwa kuweka mkono wao wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika Swalah."
Anasema Abu Haazim;

"Naelewa kuwa anakusudia hapa wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)". Al-Bukhaariy Juz. 1 ukurasa wa 397 Imaam Maalik katika Al-Muwattwaa na Imaam Ahmad katika Musnad.))

Mwisho wa kumnukuu.

 

 

Ndugu msomaji, riwaya hiyo nimeileta katika asili yake kwa lugha ya ki-Arab, hakuna sehemu katika riwaya hiyo Haazim anasema: "Naelewa kuwa anakusudia hapa wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)".!!  Hayo ni maneno ya mhariri sio maneno ya Haazim bali Haazima amesema:

قال حازم: لا أعلمُهُ إلا يَنمي ذلک إلی النبي (صلی الله علیه وآله وسلم ).

"Silijui hilo" ispokuwa analinasibisha hilo kwa Mtume (s.a.w.w)."

Sasa ipo wapi kauli ya Haazim anasema:"Naelewa kuwa anakusudia ……" ?!!

Kwanini Mhariri anamzuria uongo Haazim na kumvumishia ambayo hakuyasema?! Mi nadhani hali hii inaweza ikawa inatokana na ile fikra ya kwamba Ninaowaandikia hawajui, fikra hii humpelekea mtu kuandika anavyotaka yeye na kutarjumu anavyotaka maada anafikra kwamba  watu wengi hawajui lugha ya Kiarabu, na kama sio hivyo,basi kwanini useme kwamba Haazima anasema: "Naelewa kuwa anakusudia ……" wakati yeye kauli yake sio hiyo bali kasema: " Silijui hilo ispokuwa………?!! Hii kama sio udanganyifu, ulaghai, hila na Ghushi ni nini? !! Kufanya ulagha na kumbambikizia mtu asichokisema ni kosa kubwa sana na utaulizwa siku ya kiyama kwanini umemzulia mwenzio uongo?! Ni muhimu sana kila mara tukumbuke kauli za Allah (s.w) kama vile:

 فمن يعمل مثقال ذرّةٍ خيراً يره* ومن يعمل مثقال ذرّةٍ شرّاً يره* *

"Basi anayefanya wema sawa na chembe (ndogo sana) atauona*Na anayefanya uovu sawa na chembe (ndogo sana) atauona". ((Suuratuz-zilzaal-aya ya 7-8)).

JAWABU LA TANO.

Amma kuhusu riwaya au Hadithi ya Waail bin Hajar iliyopokelewa na Muslim kwamba Waail Bin Hajar: Amemuona Mtume (s.a.w.w) ananyanyua mikono yake alipoingia katika swala na kutoa Takbiiratul-Ihraam, kisha akaingiza mikono yake chini ya nguo yake na kuweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto, na kwamba alipotaka kurukuu akatoa mikono yake chini ya nguo, na kuinyanyua kisha akasema Allah Akbar na akarukuu….." ((Tazama : Sahihi Muslim, juzu ya 1/ukurasa wa 382)).

Kutoa dalili -(kwamba kitendo cha kufunga mikono katika swala ni Sunna ya Mtume (s.a.w.w)- kwa  kutumia hadithi hii itakuwa ni kutoa dalili ya kitendo (Yaani itakuwa ni kutumia kitendo hicho kama dalili ya kuthibitisha kuwa kufunga mikono katika swala ni Sunna), na dalili ya kitendo huwezi ukaitumia kama dalili ili kuthibitisha hilo ispokuwa "ikijulikana wajhi wa kitendo hicho na makusudio yake", na kwa hakika haijulikani kitendo hicho kilikuwa na lengo gani na kusudio gani maana dhahiri ya hadithi hii ni kwamba Mtume (s.a.w.w) alikusanya sehemu mbili za nguo yake na kufunika  kifua chake kwa nguo hiyo, na akaweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto, je alifanya  hivyo kwa ajili kwamba jambo hilo ni sunna katika swala au alifanya hivyo ili nguo yake isijekuanguka bali ishikamane vizuri na mwili na aweze kujihifadhi na baridi kwa nguo?, Kitendo hicho anuani yake ni Majhuul (hakijulikani wajhi wake na makusudio yake na anuani yake) , hivyo (kitedno hicho) hakiwi hoja wala dalili ispokuwa "ikijulikana na kufahamika" kwamba Mtume (s.a.w.w) kafanya hivyo kwa ajili kitendo hicho ni Sunna.

 Lakini katika kitendo hicho kuna ihtimaal mbili lazima ubatilishe ihtimaali moja ili uthibitishe iliyobaki!. Na unapobatilisha ihtimaal moja wapo ili uthibitishe ihtimaali nyingine iliyobaki, lazima uwe na dalili inayoeleweka kiakili kwamba kitedno hicho kilimaanisha kufunga mikono ni Sunna katika swala na sio ihtimaali nyingine ya pili.Ukishindwa kubatilisha ihtimaal ya pili kwa dalili zinazoeleweka kimantiki , basi haitakiwi ushikamane na kitendo hicho ili kuthibitisha kwamba kitendo hicho kilimaanisha suala la kufunga mikono katika swala ni Sunna.!!

Ndugu yangu Msomaji, hakika Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliswali pamoja na Muhajirina wa Makka na Answaar wa Madina zaidi ya miaka kumi (10), lau kama hilo (la kufunga mikono katika Swala) lingelikuwa limethibiti kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) basi jambo hilo lingenukuliwa, lingepokelewa na pia kusambazwa na maswahaba wengi zaidi walioswali nyuma ya Mtume (s.a.w.w), na sio kusambazwa au kunukuliwa au kupokelewa na Waail bin Hajar peke yake pamoja na Ihtimaal mbili zilizopo katika kitendo hicho alichokishuhudia, (maana mtu anaposhuhudia Mtume (s.a.w.w) anafanya kitendo chochote kile ,huwezi kusema moja kwa moja kuwa kitendo hicho ni Sunna maadam tafsiri ya kitendo hicho haijajulikana kilikuwa na lengo gani,ni vitendo vingapi vimeshuhudiwa Mtume (s.a.w.w) akivifanya?! Ina maana leo hii akijitokeza mtu anadai kwamba fulani kamuona Mtume (s.a.w.w) anakohoa katika swala, utashikamana na kitendo hicho kuthibitisha kuwa suala la kukohoa katika swala ni Sunna?!! ala!!

 Ikiwa mtendaji wa kitendo hicho atakwambia au kuna sehemu nyingie anasema kuwa nilifanya kitendo hicho kwa kuwa ni Sunna katika swala, hapo sawa,utakuwa na haki ya  kushikamana na kitendo hicho kuthibitisha kuwa ni sunna, ama hajakwambia na kukutafsiria au kukujulisha  lengo la kitendo hicho, wewe binafsi unahukumu tu moja kwa moja kuwa kitendo hicho ni sunna, nani alikwambia!,umejuaje! Una dalili ipi inayobatilisha ihtimaali na uwezekano wa kitendo hicho kuwa na lengo lingine tofauti na hilo! …. "Ma lakum keyfa tahkumuuna"!!

Ndio, na kubaliana na wewe ukisema hakuna kauli inayosema: ( ثم التحف بثوبه Kisha akajifunika kwa nguo yake,) kwani hadithi hii imepokelewa kwa sura nyingine pasina kuwepo kauli hiyo.

Bayhaqiy kaipokea namna hii:

روی بيهقي بسنده عن موسی بن عمير:حدثني علقمة بن وائل عن أبيه:

أن النبي (صلی الله علیه وآله وسلم )  کان إذا قام في الصلاة قبض علی شماله بيمينه ورأيت علقمة يفعله

"Bayhaqiy amepokea kwa sanadi yake kutoka kwa Musa bin Umayri anasema:

 

 "Amenihadithia Alqama bin Waail kutoka kwa Baba yake (ambaye ni Waail bin Hajar) amesema: Kwamba Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akisimama kuswali anaushika mkono wa kushoto kwa mkono wa kuli, na nilimuona (huyu ni Musa bin Umayri anasema) Alqama akifanya hivyo"))

((Tazama hadithi hii katika: Sunanil-Bayhaqiy: Juzu ya 2, Ukurasa wa 28.Hadithi hii ni dhaifu maana katika sanadi yake kuna Abdullah bin Jaafar ambaye Ibn Muiyn anasema kuwa  "sio kitu " !, na Nasaai amesema hadithi haichukuliwi (MATRUUK) .))

 Hadithi hii ina upungufu wa neno ( kisha akajifunika kwa nguo yake) ukiipima na ile hadithi ya kwanza aliyoipokea Waail bin Hajar ambayo ina ziyada ya neno hilo, hivyo hadithi hii ni pungufu na ile ni ziyada,na kanuni inasema: Ikiwa ziyada na pungufu zitakinzana, basi inachukuliwa ile ambayo ni pungufu, hii ni kanuni haina ubishi.! Hivyo hadithi hii pungufu nayo tunaichunguza kama tulivyoichunguza ile ya kwanza ambapo nayo kitendo hicho kina uwezekana na ihtimaali mbili, hivyo pia katika hadithi hii (ambayo imepungua neno hilo) kitendo hicho ni "Majhuul" anuani yake haijulikani! Kwani lau kama Mtume (s.a.w.w) alikuwa ni mwenye kudumu kufanya hivyo mara kwa mara akiswali, basi kitendo hicho kingelikuwa maarufu sana kwa watu, lakini kauli yake aliposema: ((  . ورأيت علقمة يفعله Na nilimuona Alqama akifanya hivyo)),

hii inaonyesha kwamba mpokezi au msimulizi (yaani Musa bin Umayri) ameitambua Sunna hiyo kupitia Alqama.!! Hatujui kabla ya kumuona Alqama akifanya kitendo hicho yeye binafsi alikuwa anaswali vipi?!. Musa bin Umayri angelikuwa hai tungelimuuliza swali hili!!

Pia Bayhaqiy kaipokea hadithi hii kwa Sanadi nyingine, kutoka kwa Waail bin Hajar, lakini pia ishkaal hii tuliyoitaja inadhihiri katika hadithi hiyo.Ishkaali hii iko pale pale hata kwa sanadi hii kutoka kwa Waail bin Hajar. Zaidi ya ishkaali hiyo, pia hadithi hii ni dhaifu maana katika sanadi hii kuna "Abdullah bin Rajaai". Amru bin Ali Alfalaas amesema:

Abdullah bin Rajaai alikuwa mtu ((mwenye kuchanganya mambo kwa sana na upotofu, hivyo sio hoja)).

((Hebu tazama kauli hii katika kitabu kiitwacho: Hudas-saariy: Juzu ya 1, ukursa wa 437 )).

Kwa mujibu IL-MUR-RIJAALI, sifa Kama hii aliyokuwa nayo Abdullah bin Rajaai, inadhaifisha hadithi maana sanadi ya hadithi itakuwa dhaifu, hivyo huwezi kushikamana na sanadi hiyo kuthitisha lolote.

Pia Bayhaqiy amepokea katika sanadi yake nyingie- kutoka kwa Swahaba Mkubwa wa Mtume (s.a.w.w) anayeitwa Ibn Mas-ud (r.a) kwamba:

((Siku moja alikuwa anaswali, akawa ameweka mkono wake wa kushoto juu ya mkono wa kulia,! Mtume (s.a.w.w) akamuona (akiswali katika hali hiyo), akachukua mkono wa kulia wa Ibn Mas-ud na kuuweka juu ya mkono wake wa kushoto.))

Tazama hadithi hii: ((Sunanil-Bayhaqiy: Juzu ya 2, ukurasa wa 28 .Katika mlango wa "kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto" , Hadithi namba tano (5).))

 

Hadithi hii ni dhaifu hata kabla ya kuichunguza sanadi yake, ukiiangalia kwanje tu , unajua udhaifu wake! Maana ni jambo lisilokubalika kwa Swahaba Abdullah bin Mas-ud, Swahaba mkubwa kama huyo kuwa alikuwa hajui ni lipi ambalo ni Sunna katika swala! Wakati yeye ni katika Maswahaba waliotangulia katika Uislaam!!

Ama tunapokuja upande wa sanadi ya hadithi hii, tunakuta kwamba kuna Hashiym bin Bashir, huyu alikuwa mashuhuri sana kwa kufanya (Ghushi) ulaghai, na kupotosha. Hebu tazama katika kitabu hiki ujue sifa ya mtu huyu:

((Hudas-Saariy: Juzu ya 1, ukurasa wa 449)).

Hivyo kitendo cha kufunga mikono katika swala hakina dalili sahihi na dalili zote wanazoshikamana nazo wenye kufunga mikono ni dhaifu na jambo hilo sio sunna wala Mtume (s.a.w.w) hajaliamrisha na halijui bali limezushwa tu baada ya maisha yake Matukufu na kisha kunasibishwa kwake.

Kwa ajili hiyo ndio maana Maimam Watukufu wa Ahlul-bayt (a.s) - wenye kujua sunna za Mtume (s.a.w.w) zaidi na wenye elimu zaidi ya mtu yeyote yule – walikuwa wakijiepusha na kitendo hicho cha kufunga mikono katika swala na kukiona kuwa ni kitendo cha " Majusi, hawa ndio waliokuwa wakikitenda mbele ya mfalme"!. 

Zuraara amepokea kutoka kwa Abi Jaafa (a.s) kwamba amesema:

(( وعليک بالإقبال علی صلاتک ، ولا  تکفِّر ، فإنما يصنع  ذلک المجوس))

"Inatakiwa uitilie umuhimu swala yako (uiswali kwa umakini zaidi), na usifunge mikono, kwani anayefanya hivyo ni Majusi"

((Na Swaduq amepokea kwa sanadi yake kutoka kwa Imam Ali (a.s) kwamba amesema:

(( لا يجمع المسلم يديه في صلاته وهو قائم بين يدي الله عز وجل يتشبه بأهل الکفر- يعني المجوس-))

((Muislaam asikusanye (asifunge) mikono yake katika swala yake huku akiwa amesimama mbele ya Allah (s.w), (kwani akifanya hivyo) anajifananisha na makafiri-yaani Majusi-)).

((Tazama hadithi hii katika kitabu kiitwacho: Wasaailu (cha Hurru Al-a'miliyyu) : Juzu ya 4, Mlango wa 15 katika Milango inayozungumzia vibatilishi vya swala")).

FAHAMU KWAMBA: Hii ni kauli ya Imam Ali (a.s) Imam wa Mashariki na Magharibi, tofauti na Mtume (s.a.w.w), hakuna Mwislaam yeyote (sawa sawa iwe zama hizi au zama zile za Maswahaba) ambaye anaujua Uislaam zaidi na mwenye Elimu zaidi na Mchamungu zaidi na Mwenye kumjua Mwenyeezi Mungu (s.w) na Mtume (s.a.w.w) zaidi, na Mwenye kujua sunna za Mtume (s.a.w.w) zaidi, kama Imam Ali (a.s).! Imam Ali (a.s) anasema kufunga mikono ni kitendo cha Majusi na kufanya hivyo ni kujifananisha na Majusi, ingelikuwa Jambo hilo ni  Sunna ya Mtume (s.a.w.w), basi Imam Ali (a.s) bila shaka angelitambua hilo na asingelikataza nay eye mwenye zingepokelewa riwaya zikisema ameonekana akiswali hivyo !! Maana ikiwa Musa bin Umayri anasema kamuona Alqama anaswali kwa kufunga mikono, basi zingelikuwepo pia hadithi zinazosema kwamba Imam Ali (a.s) siku moja kaonekana naye akitenda sunna hiyo katika swala, maana huwezi kuniambia kauli yako ikaniingia akilini kwamba Alqama haiwezekana akaijua vizuri sunna hiyo kuliko Imam Ali (a.s)!! . 

Kwa mujibu wa Madh-hebu ya Ahlul-bayt (a.s) ya "Shia Ithna Ashariya" wenye kuwafuaata Maimam kumi na wawili (12) (a.s) walioteuliwa na Mtume (s.a.w.w) kuwa Makhalifa wake baada yake, jambo hili si SUNNA bali ni BID'A ILIYOWAZI, kwani limeingizwa katika Uislaam baada ya Mtume (s.a.w.w) na kunasibishwa kwake kwa hadithi za uongo na dhaifu kama hizo zilizotajwa na Mhariri kwenye site ya  (alhidaaya.com).

Kuna riwaya zimepokelewa na makundi yote mawili (yaani Shia na Ahlus-sunna) zinazothibitisha kuwa swala sahihi ya Mtume (s.a.w.w) haikuwa kwa kufunga mikono si tumboni kwenye kitovu au juu ya kitovu au katika katika ya kifuna na kitovu wala karibu na shingo, bali swala sahihi aliyoiswali aliiswali kwa kunyoosha (kuachia) mikono yake.Nitataja hapa hadithi mbili, moja imepokelewa na (Shia na Ahlus-sunna) na ya pili imepokelewa na kelewa kwa njia ya Shia Ithna ashariya (Imamiyya) tu.Kupitia hadithi hizi mbili tutakuwa tumethibitisha kuwa Kufunga mikono katika swala ni Bid'a na si Sunna kama wachache walivyodhani.Nazo ni hizi zifuatazo:

  HADITHI SAHIHI ZA KUNYOOSHA (AU KUACHIA) MIKONO KATIKA SWALA.

Hadithi ya kwanza:

Hadithi ya Abu Humeid As-saidiyyu:

Hadithi hii ya Humeid As-saidiyyu, imepokelewa na Wanahadithi wengi, bahthi itakuwa ndevu sana ikiwa tutataja kila mtu alivyoipokea, lakini ngoja tuitaje kwa mujibu wa maelezo ya Bayhaqiy. Bayhaqiy amesema: Ametupa habari Abu Abdillah Al-Haafidhu: Akasema: Akasema Abu Humeidi As-saidiyyu:

"Mimi ni Mjuzi zaidi wa swala ya Mtume (s.a.w.w)" .Wakasema: Kwa nini?  Ilhali haukumfuata mara nyingi zaidi yetu na wala hukutangulia kuwa naye kabla yetu?!" Akasema, 'Ndio', wakasema "tuelezee"!.

" Akasema: Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akisimama kuswali,alikuwa akiinua mikono yake mpaka iwe sawa na mabega yake, kisha anatoa Takbira mpaka kila kiungo kiwe kitulie sehemu yake huku akiwa amenyooka.Kisha anasoma, kisha anatoa Takbira na kuinua mikono yake mpaka iwe sawa na mabega.Kisha anarukuu na kuweka viganja vyake juu ya magoti yake,kisha ananyooka bila kunyanyua kichwa chake wala kukilaza.Kisha ananyanyua kichwa chake na kusema:"(Mwenyeezi Mungu amemsikia aliyemhimidi)".Kisha ananyanyua mikono yake mpaka iwe sambamba na mabega yake mpaka kila kiungo kirudi sehemu yake huku akiwa amenyooka.Kisha anasema: "Allah Akbar".

 Kisha anaporomoka (kwenda sajda) ardhini na kuweka mikono yake pembeni mwake, kisha anainua kichwa chake na kukunja mguu wake wa kushoto na kuukalia.Na anaposujudu hufungua vidole vya miguu yake.Kisha anarudi kusujudu, kisha anainua kichwa na kusema: "Allah Akbari".Kisha anakunja mguu wake na kuukalia akiwa amenyooka mpaka kila mfupa utulie sehemu yake.Kisha anafanya hivyo katika rakaa nyingine.Kisha anaposimama toka kwenye rakaa mbili , hutoa Takbira na kuinua mikono yake mpaka iwe sawa na mabega yake kama alivyofanya pale mwanzo was ala yake alipotoa Takbira.Kisha anafanya hivyo hivyo katika Swala yake yote mpaka anapofika katika sijda ya kutoa salam( ili kumaliza swala), basi hapo huchelewesha mguu wake wa kushoto na kukaa mkao wa Tawaruki na kukaa upande wake wa kushoto (yaani: Mwili ukiwa umelemea upande wa kushoto)".

Hapo wote wakasema: "Amesema kweli" ! , hakika hivyo ndivyo alivyokuwa akiswali Mtume -(s.a.w.w)- wa Mwenyeezi Mungu -(s.w)-"

((Tazama hadithi hii: Albayhaqiy: As-sunani: Juzu ya 2, ukurasa wa 72, 72,101.102. Tazama pia: At-tirmidhiy: As-sunani: Juzu ya 2, ukurasa wa 98, katika mlango wa wasifu wa Swala.Tazama pia: Musnad Ahmad: Juzu ya 5, ukurasa wa 424.))

Katika hadithi hii kuna mambo yanayoonyesha uhakika, ukweli na usahihi wa hadithi hii, moja ya mambo hayo ni Maswahaba wote hao wakubwa kumsadikisha Abu Humeidi.Kitendo hicho cha kumsadikisha kinaonyesha nguvu ya hadithi hii na usahihi wake, na kufaa kuitanguliza kabya ya kuitanguliza dalili yoyote ile nyingine.Na miongoni mwa Maswahaba wakubwa waliomsadikisha ni, Abu Hurayra, Sahl As-saidiyyu, Abu Usaydu As-saidiyu, Abu Qatadatul Haarithu bin Rabiiyu, na Muhammad bin Maslamati.

Kwa hakika Abu Humeidi As-saidiyyu, ametoa wasifu wa swala ya Mtume (s.a.w.w) kuanzia swala za Faradhi na zile za Sunna, na hajataja kufunga mikono, na wala Maswahaba hao hawajamkosoa wala kutaja kitu kingine kinyume na alivyosema, na walikuwa na nia ya kumkosoa maana pale mwanzo hawakukubali kuwa yeye ni mjuzi zaidi wa swala ya Mtume (s.a.w.w) kuliko wao.Lakini pamoja na hali hiyo,wote walisema:Umesema kweli  hivyo ndivyo alivyokuwa akiswali Mtume (s.a.w.w).

Huwezi kusema kwamba makumi ya Maswahaba hao wote walisahau kumkumbusha kuwa amesahau kutaja kuwa Mtume (s.a.w.w) alikuwa "akifunga mikono"!. Dhana hii haikubaliki maana wote walikuwa katika hali na mazingira ya kukumbuka.

Ukija katika asili ya kuweka mikono, utakuta ni kuinyoosha, na hayo ndio maumbile ya Mwanadamu, na hadithi imetaja jambo linaloendana sawa na Maumbile ya Mwanadamu. Abu Humeidi As-saidiyyu hakutaja au kuonyesha ispokuwa hayo yalikuwa ni mafunzo, yaani: alikuwa katika hali ya kuonyesha au kutoa mafunzo kunako swala sahihi ya Bwana wetu Mtume (s.a.w.w), si kwamba alilenga kuwafundisha Maswahaba bali hilo lilikuwa ni soma kwa wengine na vizazi vijavyo tukiwemo sisi zama hizi.Hivyo sifa za swala alizozitaja ndivyo hivyo swala inavyotakiwa iswaliwe na zile sifa ambazo hakuzitaja, inamaana hazitakiwi katika swala bali hiyo sio swala ya Mtume (s.a.w.w). Kwani kitendo hicho cha kutaja sifa ilikuwa ni mafunzo, hivyo huwezi kuwambia watu wenye akili zao kwamba "hakutana jambo fulani hali ya kuwa jambo hilo ni Sunna katika swala", kwani kusema hivyo utakuwa unamaanisha Swahaba huyo (Abu Humeidi As-saidiyyu) alifanya khiyana kutotoa baadhi ya sifa, na aliyefanya khiyana si yeye tu bali hata hao Maswahaba wakubwa waliokuwa wakimsikiliza akizitaja sifa za Swala ya Mtume (s.a.w.w), nao watakuwa wamefanya khiyana maana alipomaliza kuzitaja sifa hizo na kuwaonyesha ni jinsi gani Mtume (s.a.w.w) alikiswali, walimsadikisha pasina kusema umesahau jambo la kufunga mikono!. Kama kufunga mikono ni sunna basi ilitakiwa wambie, E bwana! Tunashukuru kwa uliyoyataja lakini Umekosea, hujataja kufunga mikono!"  Na kwakuwa walimsadikisha, basi ina maana kwamba walikubaliana naye kwa zile sifa alizozitaja kuwa ndio swala sahihi aliyoiswali Mtume (s.a.w.w), na pia walikubaliana naye kwa zile sifa ambazo hakuzitaja kuwa hakika hazimo katika swala sahihi ya Bwana Mtume (s.a.w.w). Na hili la kufanya khiyana halikubaliki na liko mbali na Yeye pamoja na Maswahaba wote hao.

Hivyo ndugu Msomaji, Kwa kuwa baadhi ya Maswahaba waliokuwepo kati ya wale waliopokea hadithi za kukunja mikono, hawajapinga maelezo ya Abu Humeidi As-saidiyyu, Kwa mantiki hiyo, "kufunga mikono katika Swala" Kama ilivyo kwa Madh-hebu ya Maalik, na Alaythu bin Saad na Al-awzaiy sio Sunna katika Swala bali ni Bid'a.

Ibnu Rushdi amesema: Na sababu ya kutofautiana kwao ni kwamba zimekuja riwaya thabiti ambazo zilinukuu wasifu wa Swala ya Mtume (s.a.w.w), lakini haijanukuliwa kuwa alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto" (Tazama: Bidayatul-Mujtahid)

Pia ndugu msomaji, kama tulivyotangulia kusema kuwa Wafuasi wa Malik hawafungi mikono na Imam wao (Malik) alikataa Suala hilo.Imam Maalik anasema katika kitabu chake cha Al-Mudawanaati akikataa kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto ndani ya Swala: "Silijui jambo hilo ndani Swala ya faradhi".Hii ndio Fat-wa yake Malik na ile riwaya ya kufunga mikono katika swala aliyoipokea katika kitabu chake cha Riwaya kiitwacho: Al-Muwatta, kupokea kwake riwaya hiyo haimaanishi kwamba hiyo ni Fat'wa yake, kwani inajuzu na si jambo la ajabu mtu ukapokea riwaya na ukaipinga kulingana na ulivyoielewa na ulivyo zielewa riwaya nyingine zinazopinga jambo la kufumga mikono katika swala.Na hivi ndivyo alivyofanya Imam Maalik. 

Kwa ufupi hiyo ni hadithi iliyopokelewa na Masunni kama ilivyopokelewa na Shia Ithna Ashariyya (Imamiyya).

Na sasa tuitazame riwaya iliyopokelewa na "Shia Imamiyya".

Hadithi ya pili:

Hadithi ya Hammad bin Isa

Hammad bin Isa amepokea riwaya kutoka kwa Imam Jaafar Swadiq (a.s) kwamba amesema (au alisema):

Ni jambo baya sana Mtu kutimiza umri wa miaka Sitini (60) au Sabini (70) ilhali hajawahi kuswali "hata Swala moja kwa ukamilifu", ! Hammadi akasema: Ukanifikia udhalili katika nafsi yangu, ni kasema: Niko chini yako, "nifundishe swala". !

"Akasimama Abu Abdillah -yaani Imam Jaafar Swadiq- (a.s) huku akiwa ameelekea Qibla, akanyoosha mikono yake yote (huku akiwa ameiweka) juu ya mapaja yake ilhali kabana vidole vyake na kasogeza nyayo zake mpaka kiwango cha uwazi wa vidole vitatu, akaelekeza Qibla vidole vyake vya miguu kwa unyenyekevu pasina kuvitoa Qibla, akasema: "Allah Akbar", kisha akasoma AL-HAMDU na KULI HUWALLAH AHADU, kisha akasubiri kidogo kiwango cha kuvuta pumzi akiwa amesimama.Kisha akasema: "Allah Akbar" akiwa amesimama, kisha akarukuu na kujaza viganja vyake kwenye magoti yaliyoachana na akarudisha magoti yake nyuma mpaka mgongo wake ukanyooka kiasi kwamba hata kama tone la maji au mafuta lingedondoka juu ya mgongo wake,basi lingekaa.Akaendelea kunyoosha mgongo huku akiwa amerudisha magoti yake nyuma,akanyoosha shingo yake mbele , kisha akamsabbihi Mwenyeezi Mungu (s.w) akisema: "Ametakasika Mola wangu Mtukufu , na kila sifa njema ni zake".Kisha akasimama akiwa amenyooka na alipotulia akasema: "Mungu kamsikia aliyemhimidi  aliyemhimidi". Kisha akatoa Takbira akiwa amesimama, akainua mikono yake mkabala na uso wake na akasujudu, akatanguliza kuweka mikono yake Ardhini kabla ya kuweka magoti yake na kusema maneno haya mara tatu: "Ametakasika Mola wangu Mtukufu na kila sifa njema ni zake".Na hakuweka sehemu ya mwili wake juu ya sehemu nyingine ya mwili wake, akasujudu kwa kutumia viungo nane (8) tu:

1-Bapa la uso

2-Viganja viwili

3-Magoti yake mawili

4-Vichwa viwili vya vidole gumba vya miguu na pua

Nb: Viungo hivi saba ni wajibu, ama kuweka pua ni Sunna kwa ajili ya kujidhalilisha mbele ya Mola wako (s.w).

Kisha akainua kichwa chake toka Sajda, na alipokaa sawa akasema: "Allah Akbar" akakaa kwa kulalia (kuelemea)

Upande wake wa kushoto, akawa ameweka mgongo wa mguu wake wa kulia juu ya nyayo ya mguu wake wa kushoto, kisha akasema:

((ASTAGHFIRULLAH RABIY WA ATUUBU ILAYHI))

Namuomba Mola wangu Magh-fila na ninatubu kwake".

Kisha akatoa Takbir akiwa amekaa, kisha akasujudu Sijida ya pili, akasema kama alivyosema katika Sijida ya kwanza. Wala hakutumia sehemu ya mwili wake kuusaidia mwili wake katika Sajida yake na Rukuu yake. Na wala hakuweka dhiraa zake (za mikono) juu ya Ardhi (kama afanyavyo Simba anapokuwa amelala).

Hivyo akaswali Rakaa mbili namna hii, kisha akasema:

Ewe Hammad hivi ndivyo unavyotakiwa kuswali, wala usigeuke na usicheze kwa mikono yako na miguu yako, na usiteme mate kushoto kwako au kulia kwako au mbele yako."

((Tazama riwaya hii kwenye kitabu cha Al-wasaailu cha: Al-hurru Al-aamiliyyu: Juzu ya 4, mlango wa 1 ambai mlango wa vitendo vya swala)).

Na sasa nazungumza na msomaji!, Ndugu msomaji! , kwa hakika tunapozichunguza riwaya hizi mbili, yaani ile ya kwanza iliyopokelewa na Masunni na Shia Ithna Ashariyya(Imamiyya), na hii ya pili iliyopokelewa na Shia Imamiyya ,tunazikuta zinatufundisha Swala sahihi iliyoswaliwa na Bwana wetu Mtume (s.a.w.w) na amabayo Waislaam wote wanatakiwa kuiswali.Pia riwaya hizo mbili hakuna sehemu zimetaja jambo la kufunga mikono na vigawanyo vyake tofauti.Kama kufunga mikono ingelikuwa ni sunna, basi Imam Jaafar Swadiq (a.s) asinge sita kutenda Sunna hiyo maana kitendo chake hicho kilikuwa ni funzo kwetu sisi na kwa kila Mwislaam akitufundisha Swala sahihi ya Mbwana wetu Mtume (s.a.w.w), kwa sababu kachukua toka kwa Baba yake Imam Muhammad Baaqir (a.s),na Imam Baaqir kachukua toka kwa baba yake Imam Zainul Abidin Ali bin Hussein (a.s), na Imam Ali bin Husein (a.s) kachukua toka kwa baba yake Imam Husein (a.s), na Imam Husein (a.s) na Imam Hassan (a.s) wamechkua toka kwa Baba yao ambaye ni Imam Ali  bin Abi Twalib (a.s) , na Imam Ali (a.s) kiongozi wa Waumini wote amechukua toka kwa Mtume (s.a.w.w.).

Hivyo basi "Kufunga mikono katika Swala ni Bid'a, na Bid'a maana yake ni : "Kupandikiza jambo katika sheria wakati jambo hilo halipo katika  sheria !"

Mpaka hapo tutakuwa tumefikia mwisho wa Makala yetu kwa leo, na tulilolithibitisha katika makala yetu hii ni kuwa jambo la kunyoosha mikono katika swala ndio swala sahihi ya bwana wetu Mtume (s.a.w.w).Ama tulilolibatilisha katika makala hii ni jambo la kufunga mikono katika swala,hakika jambo hilo Bid'a na si Sunna ya Mtume (s.a.w.w) bali bali limenasibishwa kwake baada ya maisha yake matukufu, na tumegusia asili ya jambo hilo kwamba ni jambo lililokuwa likitendwa Majusi ,pia Makhalifa na Magavana walikuwa waliwamrisha watu kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika swala-si Mtume (s.a.w.w) aliyekuwa akiamrisha hivyo.Tumetoa dalili za kutosha kwa tulichokithibitisha na pia tumetoa dalili za kutosha kwa tulichokibatilisha,hatujabatilisha ispokuwa kwa kutumia dalili za kiakili na kiriwaya.Hivyo basi, kazi kubwa inabaki kwa msomaji, hakika msomaji wewe ndiye mwenye jukumu la kuchagua baada ya kuwa umeshazijua dalili wazitumiazo kutetea kufunga mikono katika swala na zile zitumikazo kwa upande wa pili kwa wale wenye kunyoosha mikono katika swala.Allah (s.w) kampa Mwanadamu akili ili kupitia akili aweze kutambua ni lipi sahihi na lipi sio sahihi.Siku ya kiyama Mwanadamu atahukumiwa kulingana na alivyoitumia akili yake kuitafuta haki, na hapo itakuwa ni bahati kubwa kwa aliyeitumia akili yake vizuri kuitambua haki iko wapi,na kinyume chake basi itakuwa ni hasara juu ya hasara.

Tunamuomba Allah (s.w) atujalie tuwe miongoni mwa wale waliopata bahati ya kuitumia akili yao waliyopewa na Mola wao ili kutajua Haki iko wapi na sio kuitambua tu, bali baada ya kuitambua wakaifuata.

Mtume (s.a.w.w) amesema: "Ali - (a.s) - yuko pamoja na Haki, na Haki iko pamoja na Ali -(a.s)-, (Haki) inamzunguka (Ali a.s) kwa vyovyote vile atakavyozunguka".

 

 


Mourining of Imam Hossein
پیام رهبر انقلاب به مسلمانان جهان به مناسبت حج 1441 / 2020
We are All Zakzaky
Hatuukubali muamala wa Karni