Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Mei 2024

14:07:39
1455918

Uturuki yasitisha biashara na Israel kulalamikia maafa ya kibinadamu Gaza

Serikali ya Uturuki imetangaza kuwa, imesitisha biashara zote na utawala ghasibu wa Israel kutokana na mashambulizi yake huko Gaza, ikitoa mfano wa "janga la kibinadamu linalozidi kuongezeka" katika ukanda huo.

Wizara ya Biashara ya Uturuki imesema katika taarifa yake kuwa, hatua hizo zitawekwa hadi Israel iruhusu "mtiririko usioingiliwa na wa kutosha" wa misaada katika Gaza.

Biashara kati ya nchi hizo mbili ilikuwa na thamani ya karibu $7bn (£5.6bn) mwaka jana (2023).

Waziri wa mambo ya nje wa Israel alimshutumu rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa kuwa "dikteta".

Israel Katz alisema kwenye X kwamba Bw Erdogan "anapuuza maslahi ya watu wa Uturuki na wafanyabiashara na kupuuza makubaliano ya biashara ya kimataifa".Hayo yanajiri katika hali ambayo, majuzi Hakan Fidan Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alisema kuwa nchi hiyo itaomba kuwa sehemu ya kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya Israel. Itakumbukwa kuwa serikali ya Afrika Kusini imefungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mauaji yake ya kimbari huko Gaza. Mwanzoni mwa mwaka huu, kimya cha namna fulani cha viongozi wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan kwa mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza kilipelekea kufanyika maandamano ya mara kwa mara nchini Uturuki katika kipindi cha takribani miezi mitatu tangu kuanza hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel huko Gaza.

342/