Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Mei 2024

14:08:28
1455919

Kukatwa kikamilifu uhusiano wa Colombia na utawala wa Kizayuni; kuendelea kutengwa Tel Aviv kimataifa

Rais Gustavo Petro wa Colombia alisema siku ya Jumatano tarehe Mosi Mei katika hotuba yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kuwa kuanzia Alhamisi amekata kikamilifu uhusiano wa nchi hiyo na utawala wa Kizayuni kwa sababu ya jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo huko Ukanda wa Gaza.

Petro amesisitiza hilo kwa kusema: "Akiwa hapa mbele yenu, Rais wa serikali ya mabadiliko anatangaza kuwa kuanzia kesho (Alkhamisi) tutakata kikamilifu uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Israel kwa sababu utawala huo na Waziri Mkuu wake Benjamin Netanyahu wamehusika na mauaji ya kimbari huko Gaza." Rais wa Colombia awali alitishia kuwa angevunja uhusiano wa nchi yake na utawala wa Kizayuni na kusema: "Ikitubidi kuvunja uhusiano na Israeli, tutafanya hivyo." Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) jana asubuhi ilitoa taarifa ikiunga mkono hatua ya  Colombia ya kukata kikamilifu uhusiano wake na Israel. Hamas ilitangaza katika taarifa yake hiyo kwamba inaunga mkono msimamo wa Rais Gustavo Petro wa Colombia wa kuvunja uhusiano wa kidplomasia na utawala ghasibu wa Kizayuni kutokana na kuendelea vita vya jeshi ghasibu la Kinazi dhidi ya raia wa Kipalestina huko Ukanda wa Gaza. Hamas imesema uamuzi huo wa Rais wa Colombia ni ushindi kutokana na kujitolea kwa watu wao katika kupigania malengo ya kiadilifu."

Hatua ya Colombia ya kuvunja uhusiano na utawala wa Kizayuni ni pigo jingine kwa utawala huo, na ni hatua itakayopelekea kutengwa zaidi Tel Aviv duniani. Tangu kuanza vita dhidi ya Gaza Oktoba mwaka jana, nchi za Latini Amerika zimedhihirisha misimamo ya kupinga jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza hasa mauaji ya kimbari yaayofanywa dhidi ya Wapalestina, kutumiwa utawala huo silaha nzito na kuwasababishia njaa wakazi wa eneo hilo. Nchi hizo pia zimelaani jinai za utawala wa Kizayuni na kuchukua hatua ya kuvunja au kupunguza uhusiano wao na utawala huo na hata kufikia hatua ya kuushtaki katika taasisi za kisheria za kimataifa.  Katika uwanja huo, mwishoni mwa Oktoba mwaka jana baada ya Bolivia kuchukua uamuzi madhubuti na wa wazi wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni; wakuu wa nchi mbalimbali za Amerika ya Latini zikiwemo Colombia, Brazil, Chile na Venezuela pia walilaani mahambulizi ya Israel dhidi ya kambi kubwa zaidi ya wakimbizi huko Ukanda wa Gaza na kusema kuna uwezekano nchi nyingine za eneo hilo zikafuata mkondo na kuchukua uamuzi sawa na uliochukuliwa na Bolivia mkabala wa utawala wa Kizayuni. 

Kati ya wakuu hao wa nchi ni Marais wa Colombia na Chile yaani Gustavo Petro na Gabriel Boric ambao walitangaza kupinga mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Israel dhidi ya Gaza na kusema wamewaita nyumbani mabalozi wao kutoka katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) ili kutathmini umuhimu wa kudumisha mazungumzo ya kidiplomasia na utawala wa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo wa kibaguzi. Rais Gabriel Boric wa Chile wakati huo aliandika katika ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Chile inalaani vikali matendo ya Israel na inafuatilia kwa wasiwasi mkubwa oparesheni ya kijeshi inayotekelezwa na Israel ya kuwaadhibu kwa umati raia wa Kipalestina huko Gaza, isiyoheshimu kanuni wala sheria za kimataifa."

Hii ni katika hali ambayo Rais Daniel Ortega wa Nicaragua pia amehoji uwezo wa Umoja wa Mataifa wa kuondoa vizuizi ili kuhitimisha mzingiro wa Marekani dhidi ya Cuba na vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza na kusema taasisi hiyo imekuwa wenzo tu unaotumiwa na mabeberu na haina manufaa yoyote kwa jamii ya wanadamu. 

Bila shaka, Venezuela ambayo inahesabiwa kama kiongozi wa nchi za kimapinduzi huko  Amerika ya Latini ilikata uhusiano wake na Israel kitambo nyuma. Katika vita vya Israel na Lebanon mwaka 2006, Venezuela ilimwita nyumbani balozi wake mdogo kama ishara ya kupinga uvamizi wa Israel. 

Kwa utaratibu huo, inatupasa kusema kuwa nchi za Amerika ya Latini zimedhihirisha misimamo mikali zaidi kimataifa miongoni mwa nchi zisizo za Kiislamu dhidi ya Israel na jinai zake za kutisha huko Gaza. Wakati huo huo zimeanzisha kampeni kubwa dhidi ya utawala huo wa Kizayuni kwa kupunguza, au kukata uhusiano wao na Tel Aviv na vile vile kuishtaki na kuunga mkono kesi dhidi ya Israel zilizofunguliwa na nchi nyingine kama Afrika Kusini kwa tuhuma za mauaji ya kimbari. Nchi za Amerika ya Latini zimechukua hatua nyingine sasa, kufuatia Colombia kuvunja kikamilifu uhusiano wake wa kidiplomasia na Israel.  



342/