Hujjatul Islam Muhammad Hassan Abu Turabifard khatibu wa Swala ya ya Ijumaa ya wiki hii mjini Tehran ameashiria operesheni hiyo iliyopewa jina la "Ahadi ya Kweli" na kusema: Katika operesheni hiyo, Iran ilionyesha sehemu ya uwezo wake wa usimamizi wa masuala ya kijeshi na kuongeza kwamba, hii leo mafanikio ya operesheni hiyo ya ushindi yanapaswa kubainishwa.
Hujjatul Islam Muhammad Hassan Abu Turabifard ameendelea kusema kuwa Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba operesheni hii ingeweza kuwa zaidi ya ilivyokuwa, lakini ilipunguzwa ili kuenda sambamba na ukhabiti wa adui.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran ameendelea kusema: 'Kwa mtazamo wa maadui, "Operesheni ya Ahadi ya Kweli" ilikuwa pana sana na imekuwa mwanzo wa mabadiliko ya mligano wa nguvu kieneo."Ikumbukwe kuwa, Jumatatu, Aprili 1, 2024, utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus katika shambulio la kigaidi lililopelekea kuuawa shahidi washauri saba wakuu wa kijeshi wa Iran.
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran aliitaja hatua hiyo ya Israel kuwa ni shambulio dhidi ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni "utaadhibiwa".
Katika kutekeleza ahadi hiyo, Jumapili asubuhi (tarehe 14 Aprili 2024), Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilichukua hatua ya kuuadhibu utawala huo wa Kizayuni kwa kuvurumisha ndege zisizo na rubani na makombora kuelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kupitia operesheni ya kuiadhibu Israel iliyopewa jina la "Ahadi ya Kweli."
342/