Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Mei 2024

14:09:39
1455921

Iran: Palestina inapaswa kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa

Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza udharura wa kukubaliwa Palestina kama mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

 Amir Saeid Iravani, ambaye alikuwa akihutubia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika mjini New York kwa ajili ya kujadili kura ya veto ya Marekani ya kupinga ombi la uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, ametangaza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa uanachama kamili wa  Palestina katika Umoja wa Mataifa na kusema, kura ya kufedhehesha ya veto ya Marekani, ambayo ilikwenda kinyume na matakwa ya jamii ya kimataifa, ilionyesha kwa mara nyingine tena kwamba nchi hiyo (Marekani) ndio kikwazo pekee katika kutimiza lengo kuu la watu wa Palestina.

Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa pia amebainisha jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel tangu tarehe 7 Oktoba 2023 na kueleza wasiwasi wake kuhusu habari za mashambulizi ya Israel dhidi ya eneo la Rafah katika Ukanda wa Gaza na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.Iravani amefafanua kuwa, kwa mtazamo wa Iran, suluhisho kamili la suala la Palestina litapatikana tu kupitia njia ya kulipa taifa la Palestina haki yake ya kujiamulia mambo yake na kuanzishwa nchi huru ya Palestina katika ardhi zote za Palestina, mji wake mkuu ukiwa Quds Tukufu.

Itakumbukwa kuwa, Aprili 18, wanachama 12 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Russia na China, walipiga kura ya kuunga mkono azimio la kukubali uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa. Marekani ilipinga azimio hilo kwa kulipigia kura ya veto.



342/