Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Mei 2024

14:11:32
1455923

Kuongezeka ukatili dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Marekani wanaounga mkono Palestina

Huku maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani yakiendelea kufanyika kwa lengo la kupinga jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na vilevile kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina, polisi wa nchi hiyo wameongeza hatua zao za ukandamizaji dhidi ya wanafunzi hao.

Gazeti la New York Times limeandika kwamba wanafunzi waliokamatwa na polisi ni zaidi ya elfu moja na kuwa mapigano kati yao na waandamanaji wanaounga mkono Palestina na wasimamizi wa Chuo Kikuu cha Columbia huko New York, yanaendelea kuongezeka.

Baada ya wanafunzi kudhibiti jengo la Hamilton mapema Jumanne, uongozi wa chuo iliamua kudhibiti watu wanaoingia kwenye chuo hicho. Wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina walibadilisha jina la Ukumbi wa Hamilton wa Chuo Kikuu cha Columbia na kuuita Hind's Hall katika kumkumbuka Hind Rajab, aliyeuawa kinyama pamoja na familia yake, na jeshi la utawala wa Israel miezi michache iliyopita. Uongozi wa chuo kikuu hicho wamesema watawafukuza chuoni hapo wanafunzi wote walioshiriki katika hatua hiyo. Ben Chang, Msemaji wa Chuo Kikuu cha Columbia amesema kuwa maafisa wa polisi ya New York waliingia katika majengo ya chuo hicho siku ya Jumanne jioni kwa ombi la mkuu wa Chuo, kwa ajili ya kuwakamata na kuwatawanya waandamanaji wanaounga mkono Palestina.

Wakati huo huo, Bodi ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Columbia imesema, kuingia askari wenye silaha chuoni hapo kunahatarisha maisha ya wanafunzi na watu wote walio ndani ya chuo hicho, na kuwabebesha lawama wasimamizi wote wa chuo waliosababisha kutokea hali hiyo hatari na ya kusikitisha.

Pia, polisi wa walitumia gesi ya kutoa machozi kuwakandamiza wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Florida Kusini katika mji wa Tampa. Picha za video zinaonyesha kuwa siku ya Jumatano asubuhi polisi waliwarushia vitoa machozi wanafunzi hao na kukamata wawili kati yao.

Nukta muhimu ni kwamba sambamba na kuendelea makabiliano na ukandamizaji dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, viongozi wa serikali ya Marekani pia wanataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya vuguvugu la wanafunzi wanaounga mkono Palestina. Wabunge 21 wa chama cha Democrat cha Marekani siku ya Jumatatu waliliandikia barua Baraza la Wadhamini la Chuo Kikuu cha Columbia, wakiliambia kwamba wakati ulikuwa umefika kwa ajili ya chuo kikuu hicho kuchukua hatua madhubuti, za kuondoa mahema ya waandamanaji na kuwahakikishia usalama wanafunzi wake wote. Chuck Schumer kiranja wa wabunge wa Democrat waliowengi katika Seneti alilaani na kuwakosoa kwa maneno makali waandamanaji wa Chuo Kikuu cha Columbia ambao walipeperusha bendera ya Intifada katika Ukumbi wa Hamilton. Katika upande wa pili, Jamal Bowman, mjumbe wa chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, amesema suala la chuo kikuu kufanywa kuwa medani ya kijeshi na kukamatwa mamia ya wanafunzi linapingana moja kwa moja na nafasi ya elimu.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yameibua wimbi kubwa la maandamano ya wanafunzi kuwahi kushuhudiwa tangu kufanyika maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi mwaka 2020 nchini Marekani. Mbali na wanafunzi, kwa mara ya kwanza idadi kubwa ya mahadhiri na wasimamizi wa vyuo vikuu wamejiunga na wanafunzi huko Marekani kwa ajili ya kuunga mkono Palestina, jambo linaloweza kuchukuliwa kuwa jipya katika mfumo wa kisiasa na kijamii wa nchi hiyo. Wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina, wakiwemo wanafunzi wa Kiyahudi wanaopinga vitendo vya Israel huko Gaza, wanasema wanatuhumiwa visivyo kuwa wana chuki  dhidi ya Mayahudi kwa sababu tu ya ukosoaji wao dhidi ya Israel na kuunga mkono haki za binadamu.

Maandamano makubwa na yasiyo na mfano wake yanaendelea kufanyika katika vyuo vikuu vya Marekani kwa lengo la kuwaunga mkono Wapalestina na kupinga vitendo vya jinai vya utawala wa Israel, na hivyo kuashiria mabadiliko ya kimsingi na muhimu katika mtazamo wa kizazi cha vijana wa Marekani kuhusu suala zima la Palestina. Sasa swali linaibuka hapa kuwa je, ni kwa nini kizazi cha vijana, au kwa ibara nyingine kizazi cha GenZ ni tofauti kabisa na walivyo baba zao, ambapo kinaiunga mkono Palestina na kutouthamini tena utawala wa Kizayuni? Vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na hasa Marekani vinatumia hujudi zao zote kufunika jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni na kudhihirisha kinyume cha ukweli wa mambo, kuwa unadhulumiwa.

Pamoja na propaganda hizo zote lakini mwamko wa kisiasa nchini Marekani umedhihirisha harakati kubwa ya jumuiya za wanachuo wanaotetea haki na kupinga jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel, jambo ambalo bila shaka linatuma ujumbe maalumu kwa watawala wa nchi hiyo ambao hadi sasa wamekuwa wakitumia hujuma na propaganda chafu za vyombo vya habari kuhadaa fikra za waliowengi duniani kuhusu utawala huo wa kigaidi. Raia wa  Marekani sasa wanajiuliza swali hili muhimu kwamba je, ni kwa nini nchi yao itumie gharama na pesa nyingi za walipakodi kuhudumia na kuutetea kwa hali na mali utawala ambao unatenda jinai za kivita dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, hasa watoto na wanawake?

Bila shaka, kuendelea maandamano ya wanafunzi huko Marekani kutakuwa na nafasi muhimu katika kupunguza au kuweka masharti ya uungaji mkono wa serikali ya Joe Biden kwa utawala huo wa Kizayuni na kubadilisha hatua kwa hatua misimamo kuhusu suala la Palestina nchini Marekani.


342/