Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Mei 2024

14:13:18
1455926

Wanajeshi wa Russia waingia kambi ya wanajeshi wa Marekani nchini Niger

Wanajeshi wa Russia wameingia katika kambi ya Jeshi la Anga la Niger ambayo pia ina wanajeshi wa Marekani baada ya serikali ya Niger kuamuru vikosi vya jeshi la Marekani kuondoka nchini humo.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amethibitisha tukio hilo leo Ijumaa huku akisema kuwa hakuna wasiwasi mkubwa kwani wanajeshi wa Russia hawatawafikia wanajeshi wa Marekani wala vifaa vyao.

Siku ya Alhamisi, afisa mwandamizi wa kijeshi wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe alifichua kwamba wanajeshi wa Russia tayari walikuwa kwenye Kituo cha Jeshi la Anga cha 101 karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani huko Niamey, mji mkuu wa Niger, lakini hawakuwa wakiingiliana na vikosi vya Marekani.

Taarifa za kutumwa askari wa Russia kwenye kambi hiyo ya jeshi la anga la Russia ziliibuka baada ya Niger kuifahamisha Marekani mwezi Machi kwamba inapaswa kuwaondoa haraka iwezekanavyo wanajeshi wake 1,000 walioko nchini humo.

Tukio hilo linawafanya wanajeshi wa Marekani na Russia kukaribiana sana na hivyo kuzidisha taharuki katika uhusiano wa kijeshi na kidiplomasia ambao umedorora kati ya nchi hizo mbili hasimu kutokana na mzozo unaoendelea nchini Ukraine.

Wanajeshi wa Marekani ambao wanatazamiwa kuondoka Niger hivi karibuni, tayari wametakiwa na serikali ya Chad kuondoka nchini humo mara moja, huku jeshi la Ufaransa likifukuzwa pia kutoka Mali na Burkina Faso katika miezi ya hivi karibuni.

Mnamo Machi, serikali ya Niger ilisema kwamba ilibatilisha makubaliano ya kijeshi na Marekani ambayo yaliruhusu wanajeshi wa Marekani kuwa kwenye ardhi yake.

342/