Main Title

source : Parstoday
Jumapili

5 Mei 2024

19:26:58
1456372

Meli ya kivita ya Iran yaelekea ncha ya kusini ya sayari ya dunia

Meli ya kivita ya iliyoundwa ndani ya nchi na wataalamu Wairani inayomilikiwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) imevuka mstari wa latitudo nyuzi sifuri, Ikweta, na kuelekea katika ncha ya kusini ya sayari ya dunia.

Manowari ya Shahid Mahdavi, ambayo ina uwezo wa kutekeleza majukumu kadhaa kwa ajili ya shughuli za masafa marefu, ilisajili mafanikio hayo siku ya Ijumaa ikiwa ni katika jitihada za vikosi vya wanamaji vya Iran kupanua wigo wa uwepo wao katika maji ya kimataifa na bahari kuu.

Meli hiyo ya kivita yenye uzito wa tani 2,100, ina urefu wa mita 240 na upana wa mita 27, na ilijiunga na kikosi cha majini cha IRGC mnamo Machi 2023.

Manowari hiyo ina rada ya muundo wa 3D, inasheheni makombora kutoka bahari hadi bahari na bahari hadi angani, na mifumo ya kisasa ya mawasiliano kwa ajili ya vita vya kielektroniki.

Manowari ya Shahid Mahdavi ina uwezo wa kubeba aina mbalimbali za helikopta za mashambulizi, ndege za kivita  zisizo na rubani pamoja na boti za mashambulizi ya haraka.

Mnamo Februari 2024, Jeshi la Wanamaji la IRGC lilizindua makombora mawili ya balestiki kutoka ndani ya kontena mbili kwenye meli ya kivita.

Wataalamu na wahandisi wa kijeshi wa Iran katika miaka ya hivi karibuni wamefikia mafanikio ya ajabu katika utengenezaji wa aina mbalimbali za zana kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi na kufanya majeshi ya Iran yajitosheleza katika zana za kivita na hata kuuza nje zana hizo katika soko la kimataifa.

Ikumbukwe kuwa Mwezi Mei 2023, Msafara wa 86 wa Meli za Kivita za Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulirejea nchini baada ya safari ya kuzunguka dunia kama sehemu ya juhudi za Jamhuri ya Kiislamu za kupanua uwepo wake kijeshi katika bahari za mbali.

Msafara huo wa Jeshi la Wanamaji la Iran, ulijumuisha meli ya kivita ya Dena iliyotengenezwa nchini ambayo ina uwezo mkubwa wa kuharibu manowari za adui na hali kadhalika meli ya kivita ya Makran inayosheheni zana za kivita na vifaa vingine muhimu vinavyotumika katika oparesheni za kijeshi majini.

Msafara huo wa 86 wa Manowari za Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambao ulianza safari ya kuzunguka dunia katika jiji la bandari la kusini mwa Iran wa Bandar Abbas mnamo Septemba 20, 2022, ulisimama kwa mara ya kwanza kwenye bandari ya Mumbai, India, na kisha kutia nanga Jakarta, mji mkuu wa Indonesia baada ya kupita katika Ghuba ya Bengal na Mlango-Bahari wa Malaka.