Main Title

source : Parstoday
Jumanne

7 Mei 2024

18:51:01
1456903

Tehran: Ushirikiano wa Iran na IAEA usiathiriwe na mwenendo usio thabiti wa US

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, kwa kutilia maanani rekodi ya Marekani ya kuhalifu ahadi katika mikataba ya huko nyuma kuhusiana na mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) usiathiriwe na mtazamo na mwenendo usio thabiti na wenye migongano wa Washington.

Kwa mujibu wa IRNA, Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mkutano na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, ambaye kwa mwaliko wa Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amekuja hapa Tehran kuhudhuria Mkutano wa 30 wa Kitaifa wa Nyuklia wa Iran na mkutano wa kwanza wa kimataifa wa sayansi na teknolojia ya nyuklia, na akaongeza kuwa, kuchukua misimamo isiyo ya upendeleo na ya kitaaluma Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, mbali na kusaidia sana ushirikiano wa Iran na taasisi hiyo ya kimataifa, kutakuwa na taathira chanya pia katika kurejesha usalama na utulivu katika eneo hili. Mkuu wa chombo cha kidiplomasia cha Iran ameeleza kwamba baadhi ya vitisho vilivyotolewa na viongozi wa utawala wa Kizayuni vya kutumia mabomu ya atomiki ni tishio la wazi kwa amani na usalama wa eneo na wa kimataifa, na akasisitizia jukumu muhimu sana la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki wa kukabiliana na matamshi hatari kama hayo ya viongozi wa utawala wenye maghala ya silaha za nyuklia.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitizia umuhimu wa nafasi na mchango wa IAEA, na akaongeza kuwa, ushirikiano wa Iran na Wakala huo inapasa uendelee katika mkondo sahihi, na wakati huo huo ihisike kuwa kuna utatuzi wa mambo unaopatikana kutokana na ushirikiano huo.

 Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ameeleza kufurahishwa na ziara yake nchini Iran, na akasema, nafasi na msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu katika kuleta uthabiti na usalama endelevu wa eneo una umuhimu; na akaongeza kuwa mtazamo wa Iran wa kutambua na kuimarisha ushirikiano wenye uhakika na Wakala wa IAEA unatokana na suala hilo. Rafael Grossi amesisitiza kuwa, kuimarishwa mchakato wa ushirikiano kati ya Iran na IAEA utapelekea kushindwa pande zinazotaka kushadidisha migogoro, mivutano na makabiliano katika eneo kwa kutumia kila sababu na kisingizio. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki amegusia safari yake ya awali iliyokuwa na mafanikio aliyofanya mjini Tehran na kufikia makubaliano na Iran na akaeleza matumaini aliyonayo kwamba, katika safari hii pia makubaliano mazuri yatafikiwa ili kuimarisha ushirikiano kati ya pande mbili.../

342/