Barua hiyo ya ukurasa mmoja iliyopatikana na tovuti ya habari ya mtandaoni ya Zeteo, imetumwa kwa Mwendesha Mashtaka wa ICC Karim Khan ikimhutubu ya kwamba "vibali vyovyote vya kukamatwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na maafisa wengine wakuu wa Israel si halali na havina msingi wa kisheria, na endapo vitatekelezwa vitasababisha vikwazo vikali dhidi yako na taasisi yako". "Mkiiandama Israel tutakuandameni," wameeleza maseneta hao 12 wa Marekani katika barua yao hiyo ya vitisho wakiendelea kusema: "ili kuweka wazi ni kwamba, hakuna usawa wa kimaadili kulinganisha ugaidi wa Hamas na jibu halali la Israel". Waliotia saini barua hiyo ni pamoja na Tom Cotton, Mitch McConnell, Rick Scott, Tim Scott, Ted Cruz, na Marco Rubio. Vikwazo vinavyotishiwa na maseneta hao vitawalenga wafanyakazi wa ICC na washirika wao na vitajumuisha vikwazo vya viza kwa familia za wafanyakazi wa mahakama hiyo.Hata hivyo Seneta wa chama cha Democratic Chris Van Hollen amewashutumu maseneta wenzake wa chama cha Republican kwa kujihusisha na alichokiita "ujambazi" dhidi ya mahakama kuu ya kimataifa.
Uvumi umeenea kwamba mahakama hiyo inaweza kutoa hati za kukamatwa maafisa wakuu wa Israel kwa kuhusika na jinai za kivita katika vita ulivyoanzisha utawala huo ghasibu huko Ghaza tangu Oktoba 7, 2023 ambavyo hadi sasa vimeua karibu Wapalestina 35,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao kuna uwezekano wakakabiliwa na agizo la kukamatwa ni pamoja na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri wa Vita Yoav Gallant, na Mkuu wa majeshi Herzi Halevi.../
342/