Main Title

source : ParsToday
Jumatano

15 Januari 2020

07:14:36
1002534

Zarif: Hatua ya nchi za Ulaya ya kuanzisha mchakato wa kutatua hitilafu JCPOA ni kosa la kiistratijia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo Jumatano ameonana na Niels Anne, Waziri Mshauri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Shirikisho ya Ujerumani mjini New Delhi, India na kusema kuwa, hatua ya nchi tatu za Ulaya ya kuanzisha mchakato wa kutatua hitilafu ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni kosa la kiistratijia.

(ABNA24.com) Shirika la habari la IRNA limemnukuu Dk Mohammad Javad Zarif akizilaumu nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa uamuzi wao usio na sababu wa kuanzisha mchakato wa kutatua hitilafu ndani ya JCPOA baada ya nchi hizo kushindwa kutekeleza ahadi zao kutokana na mashinikizo ya Marekani na kusema kuwa, hoja zilizotolewa na nchi hizo katika hatua yao hiyo hazina mashiko ya kisheria, na ni kosa la kiistratijia katika upande wa kisiasa.

Kwa upande wake, Niels Annen, Waziri Mshauri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Shirikisho ya Ujerumani amesema katika mazungumzo hayo kwamba, kuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muhimu sana kwa nchi za Ulaya. Aidha amesema, msimamo wa Umoja wa Ulaya ni kuyalinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kwamba tamko lililotolewa na nchi hizo tatu za Ulaya halina nia ya kuharibu makubaliano hayo.

Kwa mujibu wa mchakato wa kutatua hitilafu za JCPOA, iwapo nchi yoyote kati ya zilizofikia makubaliano hayo itadai kuwa upande fulani umekanyaga mapatano hayo, suala hilo hutakiwa kupitia hatua takriban ndefu za kuchunguza madai hayo na mwishowe kuchukuliwa uamuzi unaofaa.

Nchi za Ulaya zinadai kuwa, hatua ya Iran ya kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA ni kukiuka mapatano hayo, wakati Iran inasema kuwa, nchi za Ulaya zimeshindwa kutekeleza ahadi zao baada ya Marekani kujitoa na wala hazikabiliani na vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Iran na Marekani. Tehran inasema,  kupunguza ahadi zake katika JCPOA kumefanyika kwa mujibu wa sheria na wala si kukiuka vipengee vya mapatano hayo.

...........
340