Main Title

source : ParsToday
Jumapili

19 Januari 2020

10:20:24
1003613

Hotuba za Kiongozi Muadhamu Katika Sala ya Ijumaa Tehran; ubainishaji wa nguvu na adhama ya Iran

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba zake za Sala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran, alisema: "Kushiriki kimuujiza taifa la Iran katika mazishi ya shahidi mtoharifu Qassem Soleimani na wenzake na pia jibu kali la IRGC lililotolewa kwa kushambulia kituo cha Ainul Assad cha Jeshi la Marekani (nchini Iraq) ni siku mbili ambazo zinaweza kutajwa kuwa Siku za Mwenyezi Mungu (Ayamullah). Siku hizi zimejaa somo na ibra na ni za kuainisha hatima."

(ABNA24.com) Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa, kwa kujitokeza kwa wingi, taifa la Iran limeonyesha batini yake, ambayo ni kusimama kidete mbele ya mashetani. Aidha kujitokeza huko ni ishara kuwa njia pekee ya kufuatwa katika mkondo wa kupata izza ni kuimarika na kupata nguvu Iran katika nyuga zote.

Katika kipindi cha miaka 41 iliyopita, taifa la Iran limepita katika siku nyeti na zenye kuainisha hatima. Kila moja ya siku hizo kubwa ilikuwa ya kihistoria na ambayo athari zake zimedumu.

Katika kipindi kigumu cha kujihami kutakatifu (kipindi cha miaka minane ya uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran), taifa la Iran liliweza kupata ushindi na kubadilisha vitisho kuwa fursa. Si tu kuwa Iran imeweza kupata mafanikio katika sekta ya ulinzi na uwezo wa kumzuia adui, bali pia imepata mafanikio makubwa katika nyuga mbali mbali kuanzia uchaguzi hadi kupata ustawi wa aina yake katika sekta ya sayansi na teknolojia.

Taifa la Iran pia limeweza kupitia mitihani mikubwa ya kisiasa na hali kadhalika limeweza kupata mafanikio katika kukabiliana na mashinikizo na njama za maadui.

Nukta muhimu katika hotuba za Ijumaa za Kiongozi Muadhamu ni sisitizo lake kuhusu 'kutegemea uwezo wa taifa la Iran katika kukabiliana na adui.'

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua kuhusu nukta hiyo na kuashiria moja ya Siku za Mwenyezi Mungu katika wiki za hivi karibuni yaani, jibu lenye nguvu la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Wamarekani na kusisitiza kuwa: "Jibu hili lenye nguvu lilikuwa pigo lenye athari ya kijeshi lakini muhimu zaidi ya pigo hilo la kijeshi ni pigo kwa haiba ya dola kubwa la Marekani."

Uzoefu unaonyesha kuwa, katika kusimama kidete kukabiliana na adui na njama zake, ni lazima kuwa na nguvu katika nyanja zote ziwe ni za kijeshi, kiusalama, kiuchumi, kisayansi na kiintaneti. Aidha kuna haja ya kuwa na tadibiri na ushujaa katika kukabiliana na adui.

Ni wazi kuwa, kama ambavyo Kiongozi Muadhamu aliwahi kusema katika siku za nyuma, uadui uliopo dhidi ya Iran si wa msimu au muda maalumu bali ni uadui wa kudumu. Aidha Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, ni kosa la kistratijia kudhani kuwa uhasama wa Marekani na Iran utamalizika. Kwa hakika uwepo wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi hasa kutuma wanajeshi wake vamizi katika nchi kama vile Iraq na Afghanistan ni chimbuko la matatizo mengi katika eneo.

Kuhusiana na nukta hiyo, Ayatullah Khamenei aliashiria nafasi ya  Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na majeshi yote ya Iran yaani IRGC, Jeshi, vikosi vya kujitolea vya wananchi, ambapo msingi wa kifikra wa majeshi hayo ni imani kwa Mwenyezi Mungu na kusema: "Kikosi cha Quds, kikiwa kikosi cha nje ya mipaka ya Iran, iwapo kitahitajika kitasaidia mataifa ya eneo na kitalinda heshima ya waliodhoofishwa na kutumia uwezo wake wote kulinda matukufu na maeneo matakatifu."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema moja ya kazi muhimu za Kikosi cha Quds ni kuizuia Iran kukumbwa na vita, ugaidi na uharibifu. Ameongeza kuwa: "Sehemu kubwa ya Usalama wa Iran imetokakana na jitihada za vijana waumini ambao kwa miaka mingi wamekuwa chini ya kamanda Haj Qassem azizi katika medani ya jihadi na kujitolea muhanga."

Leo katika moja ya matokeo ya jitihada hizo, kumeshuhudiwa mabadiliko katika hali ya eneo hasa mlingano wa kisiasa na kijeshi na sasa mataifa na serikali  haziwezi kuvumilia tena uwepo wa majeshi ya Marekani Asia Magharibi. Nukta hiyo inaashiria mabadiliko muhimu na ya kistratijia katika uga wa eneo na hata uga wa kimataifa. Mabadiliko hayo yanaonyesha kuwa zama za shari, uvamizi na ubeberu wa utawala fisadi wa Marekani zinaelekea kufika ukingoni katika eneo.

Hakuna shaka kuwa njia pekee ya kukabiliana na njama za maadui ni kuhifadhi umoja wa kitaifa, kuwa na tadibiri, ushujaa na kutoogopa vitisho vya adui. Ni kwa msingi huo ndio Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sehemu ya mwisho ya hotuba zake akayahutubu mataifa ya Waislamu katika eneo kwa kusema: "Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuanzisha safu mpya na hisia zilizoamka katika nyoyo za waumini ziamshe ile hisia ya kujiamini miongoni mwa mataifa na wote wafahamu kuwa njia pekee ya kukombolewa mataifa ni kuwa na tadibiri, kusimama kidete na kutomuogopa adui."

...........
340