Main Title

source : ParsToday
Alhamisi

23 Januari 2020

07:39:51
1004748

Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman mjini Tehran na udiplomasia wa kieneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif jana Jumanne alikutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na mwenzake wa Oman, Yusuf bin Alawi kuhusu matukio ya karibuni katika eneo la magharibi mwa Asia.

(ABNA24.com) Hii ni safari ya pili kufanywa na Bin Alawi Tehran katika kipindi cha wiki mbili za karibuni. Ziara hii imefanyika katika hali ambayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ijumaa iliyopita akiwa njiani kutoka katika ziara yake ya kidiplomasia huko India, alisimama kwa muda mjini Muscat na kufanya mazungumzo na waziri mwenzake wa Canada na vilevile Yusuf bin Alawi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman.

Mchango muhimu wa Oman katika eneo la magharibi mwa Asia umeifanya nchi hiyo itambuliwe kuwa upande wa kutegemewa katika mashauriano ya kieneo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Oman imekuwa na mchango katika mchakato wa mazungumzo ya nyuklia na kufikiwa mapatano ya JCPOA na zaidi ya yote nchi hiyo imekuwa moja ya pande zinazoshauriana na Iran kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda. Kwa msingi huo uhusiasno wa kisiasa wa nchi mbili hizi upo katika kiwango cha juu zaidi.

Hivi sasa kuna kadhia mbili zilizozidisha umuhimu wa mazungumzo ya Tehran na Muscat.

Kadhia ya kwanza ni: Kuongezeka mivutano katika eneo hili la magharibi mwa Asia kutokana na hatua ya kigaidi ya Marekani huko Iraq. Tarehe 3 mwezi huu wa Januari Marekani ilikiuka mamlaka ya kujitawala ya Iraq ilipofanya shambulio la kigaidi  karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al Muhandes kiongozi wa ngazi za juu wa harakati ya kujitolea ya wa wananchi wa Iraq ya al hashdu Shaab na wanajihadi wenzao.

Marekani ilifanya ugaidi huo wakati Kamanda Soleimani alipokuwa ziarani nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo. Kufuatia shambulio hilo la kigaidi, Iran ilijibu mapigo kwa kuishambulia kwa makombora kambi kubwa zaidi na muhimu ya Marekani ya Ain al Asad huko Iraq.  

Kadhia ya pili ni mustakbali wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, misimamo ya kindumakuwili na hatua zisizo za kimantiki za Troika ya Ulaya kwa maslahi ya Marekani ili kusambaratisha kikamilifu  mapatano hayo.

Kuhusu suala la kujitoa Marekani katika JCPOA, Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman imetoa taarifa kadhaa na ikiziarifu nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kwamba: Oman inafuatilia matukio yanayojiri baada ya uamuzi  huo wa Marekani na daima itaendeleza uhusiano wa kirafiki kwa ajili ya kudumisha usalama katika eneo la magharibi mwa Asia."   

Kwa kuzingatia masuala yote haya mazungumzo ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Oman hapa Tehran ni mwendelezo wa mashauriano ya kisiasa katika fremu ya maslahi ya pamoja na kulinda amani na usalama wa jamii katika eneo hili. Masuala ya kieneo yanaonyesha kuwa, sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani zinapingana na mikakati ya kuimarisha amani katika eneo hili. Mienendo ya aina hii na kuwepo majeshi ya Marekani katika eneo hili ni jambo lisilokubalika. Hii ni kwa sababu hatua hizo zina madhara kwa nchi zote za eneo la magharibi mwa Asia. Katika mazingira kama hayo, Muscat inafanya kila iwezalo kupitia diplomasia ya pande kadhaa kwa ajili ya kusaidia jitihada za kuipatia ufumbuzi migogoro ya kieneo.

Kabla ya hapo pia, marehemu Sultan Qaboos wa Oman katika ziara yake hapa Tehran mwezi Machi mwaka jana alitoa pendekezo la kufanyika mkutano utakaozishirikisha nchi zote zenye maslahi ya pamoja. Mchango huo wa Oman kwa mtazamo wa Iran, unatathminiwa kama hatua chanya na ya kuwajibika.

Hussein Nush-Abadi, balozi wa zamani wa Iran nchini Oman ameashiria uhusiano wa karibu kati ya Tehran na Muscat na taathira ya mahusiano hayo kwa amani ya kieneo na kueleza kuwa: "Oman imekuwa na nafasi muhimu ya upatanishi katika masuala ya kieneo na mashauriano ya kisiasa na Iran. Katika miongo minne iliyopita Oman ilifanya kila iwezalo kwa ajili ya kupunguza mizozo na mivutano katika eneo hili la magharibi mwa Asia hususan katika Ghuba ya Uajemi.  

Hivi sasa pia Oman inafanya jitihada kuzuia hali ya mivutano katika kanda hii. Kiwango hiki cha uhusiano na juhudi za kulinda amani na utulivu ni ishara ya uelewa mkubwa wa Tehran na Muscat kuhusu diplomasia na kuitumia kwa ajili ya kutimiza maslahi ya pamoja.

...........
340