Main Title

source : ParsToday
Jumatatu

10 Februari 2020

08:07:53
1009191

Kuandaliwa mazingira ya kuwakutanisha Netanyahu na Bin Salman; njama ya kuuhalalisha 'Muamala wa Karne'

Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu anafanya kila njia ili akutane na kufanya mazungumzo na Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia.

(ABNA24.com) Tarehe 28 Januari, Rais Donald Trump wa Marekani alizindua mpango wa ubaguzi wa kimbari wa Muamala wa Karne katika hafla iliyohudhuriwa na Netanyahu na mabalozi wa nchi tatu za Kiarabu. Netanyahu na Marekani wamedhamiria kuutekeleza mpango huo, licha ya kupingwa na kulaani vikali kila pembe ya dunia.

Moja ya kampeni kubwa zinazofanywa na Netanyahu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ni kutafuta njia ya kuuhalalisha mpango wa Muamala wa Karne. Kampeni hiyo inaendeshwa ili zaidi kuhakikisha kuwa, mpango huo wa kihaini unakubaliwa na nchi za Kiarabu. Na ndio maana mabalozi wa Oman, Imarati na Bahrain walihudhuria hafla ya uzinduzi wake iliyofanyika mjini Washington.

Hivi sasa, na katika hatua inayofuata, waziri wa mambo ya nje wa Marekani anajaribu kutafuta na kutangaza hadharani ridhaa ya nchi zingine za Kiarabu kwa mpango wa Muamala wa Karne, ambapo moja ya nchi zenye umuhimu zaidi kati ya nchi hizo ni Saudi Arabia. Ijapokuwa balozi wa Saudia hakuhudhuria hafla ya uzinduzi wa mpango wa kidhalimu wa Muamala wa Karne, lakini watawala wa Riyadh hawajatoa kauli yoyote ya kuupinga. Saudi Arabia inachelea kuunga mkono hadharani mpango huo wa kibaguzi na wa dhulma dhidi ya Wapalestina ili isije ikajiharibia jina lake la kuonekana kidhahiri kuwa ni mtetezi na muungaji mkono wa nchi za Kiislamu na hasa Palestina.

Pamoja na hayo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, anajaribu kujifanya msuluhishi kati ya Tel Aviv na Riyadh na kuandaa mazingira ya kuwakutanisha Netanyahu na Mohammad bin Salman. Kuhusiana na suala hilo, tovuti ya gazeti la Kizayuni la Israel Hayom imezinukuu duru za kidiplomasia za Kiarabu na kuripoti kuwa, mashauriano makubwa yanaendelea kufanywa baina ya Marekani, Israel, Saudi Arabia na Misri ili kuhakikisha mkutano kati ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu na mrithi wa ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman unafanyika mjini Cairo, Misri ndani ya wiki kadhaa zijazo. Mazungumzo baina ya wawili hao yamepangwa kufanyika kupitia kikao kitakachowakutanisha viongozi wa Marekani, Imarati, Sudan, Bahrain, Oman, Saudi Arabia na Israel katika mji mkuu huo wa Misri.

Inavyoonekana, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, kwa upande mmoja anaitumia hulka ya kupenda kufanya mambo makubwa na ya kuvunja miiko aliyonayo Bin Salman kwa ajili ya kufanikisha kufanyika kwa mkutano huo; na kwa upande mwingine, Bin Salman mwenyewe inabidi alipe fadhila kwa Marekani baada ya Washington kumvua na kesi ya kuhusika na jinai ya mauaji ya Jamal Khashoggi. Tunaweza hata kusema kuwa, kuunga mkono mpango wa Muamala wa Karne, lilikuwa ndilo sharti ambalo Marekani ilimpa mrithi huyo wa ufalme wa Saudia kwa ajili ya kumkingia kifua na kumuokoa na kashfa ya mauaji ya kinyama ya Khashoggi.

Nukta muhimu hapa ni kuwa, Muamala wa Karne umedhihirisha wazi mpasuko uliopo na kugawanyika pande mbili Ulimwengu wa Kiarabu katika kadhia ya Palestina. Saudi Arabia, Imarati, Jordan, Bahrain, Oman na Misri zimejiweka upande mmoja, kwa kuonyesha dhahiri shahiri au kiishara uungaji mkono wao kwa mpango huo; na nchi zingine, ikiwemo Iraq, Lebanon, Syria, Tunisia, Kuwait na Palestina yenyewe, zimejiweka katika upande mwingine, ambapo mbali na kuupinga, zinauita mpango huo 'Uongo wa Karne' au 'Usaliti wa Karne' inaofanyiwa Palestina.
Spika wa Bunge la Kuwait, Marzouq al-Ghanim akiwa ameshikilia nakala ya mpango wa 'Muamala wa Karne'

Kuhusiana na suala hilo, wakati inaendelea kusikika minong'ono kuhusu uwezekano wa kufanyika mkutano wa mazungumzo kati ya mrithi wa ufalme wa Saudia na waziri mkuu wa Israel, katika kikao cha dharura cha Umoja wa Mabunge ya Nchi za Kiarabu kilichofanyika siku ya Jumamosi tarehe 8 Februari mjini Amman, Jordan kwa anuani ya "Msukumo na Uungaji Mkono kwa Ndugu wa Palestina katika Suala lao la Haki", Spika wa Bunge la Kuwait Marzouq al-Ghanim alikosoa vikali kile kiitwacho "Muamala wa Karne" na hata akafika mbali zaidi kwa kuikunjakunja na kuitia kwenye debe la taka nakala ya mpango huo uliopendekezwa na serikali ya Marekani. Al-Ghanim alimalizia kwa kusema: "Mahala halisi na panapofaa kwa ajili ya mpango huu ni kwenye debe la taka la historia.".

............
340