Main Title

source : ParsToday
Jumatano

12 Februari 2020

09:27:29
1009733

Mamilioni ya wananchi wa Iran wamejitokeza mabarabarani katika miji na vijiji vya nchi hii kushiriki matembezi ya Bahman 22, kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 41 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

(ABNA24.com) Licha ya baridi kali, wananchi wa Iran katika mji mkuu Tehran wameshiriki matembezi hayo katika barabara mbalimbali kabla ya kujumuika pamoja katika Medani ya Azadi, ambayo ilitumika kama kitovu cha maandamano mengi ya kupinga utawala wa kidikteta wa Pahlavi, uliokuwa ukiungwa mkono na Marekani kabla ya kuangushwa mwaka 1979.

Matembezi ya maadhimisho ya mwaka wa 41 yamefanyika katika miji 1000 na vijiji 4, 200 nchini Iran, huku waandishi wa habari 6000 wa Iran na wa kigeni wakifuatilia na kuakisi maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya Bahman 22 ya mwaka huu yamesadifiana na Arubaini ya Mashahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Abu Mahdi al-Mahandes, aliyekuwa naibu mkuu wa harakati ya kujitolea wananchi ya Hashdu Shaabi ya Iraq pamoja na wafuasi wao waliouawa kigaidi mapema mwezi uliopita katika shambulio la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq.

Wananchi wa Iran wamesikika wakipiga takbir "Allahu Akbar" pamoja na nara za "mauti kwa Marekani" na "mauti kwa Israel" wakati wa matembezi hayo ya Bahman 22.

Aidha walikuwa wamebeba bendera za Iran na mabango yenye picha zinazowaonyesha Imam Khomeini MA, Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, Jenerali Soleimani, Abu Mahdi al-Muhandes na Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, miongoni mwa shakhsia wengine.

Kadhalika wananchi Waislamu wa Iran wametumia jukwaa la matembezi ya Bahman 22 hii leo kulaani njama za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Wapalestina zilizopewa jina la "Muamala wa Karne" ambapo wameteketeza moto bendera za Marekani na utawala haramu wa Israel, huku wakichoma moto na kuharibu picha, sanamu na vikaragosi vya Trump.

...........
340