Main Title

source : ParsToday
Jumatatu

17 Februari 2020

08:23:36
1011042

Katika marasimu ya kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Fatwimat Zahra (as) Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutana na maelfu ya wasomaji wa kasida na mashairi ya kuwasifu Ahlul-Bayt wa Mtume (as).

(ABNA24.com) Katika kikao hicho Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema moja ya majukumu muhimu iliyonayo jamii ya wasomaji hao wa kasida na mashairi ni kueneza utamaduni na kuimarisha maarifa ya kidini katika matabaka yote na hasa tabaka la vijana.

Amesema: "Hii leo moja ya mahitaji muhimu ya nchi ni kuwaandaa vijana kwa silaha za vita laini ambazo ni kuinua na kuimarisha uwezo wa kiroho, kifikra na kimaanawi wa vijana na kuelewa vyema mafundisho ya Bibi Fatwimat na ya Ahlubayti wa Mtume (as)."

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kuashiria njama za vituo na uenezaji wa propaganda za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kwa ajili ya kulihadaa taifa la Iran lisikabiliana na Marekani amesema: "Taifa la Iran kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu hadi sasa limeendelea kusimama imara, na pia litaendelea kusimama imara.

Hata hivyo kusimama imara huku kunahitaji uenezaji endelevu wa umaanawi katika jamii." Mtazamo wa pamoja wa maadui katika kukabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu mwanzo wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, unaonyesha hali ya kuwa na nguvu, kubakia imara na mapinduzi haya kutowaogopa maadui. Wananchi wa Iran kwa kusimama imara mbele ya mabeberu wameweza kufikia ushindi mkubwa katika nyanja tofauti na wameonyesha kwamba hakuna dola lolote linaloweza kuliletea madhara taifa hili la Kiislamu.

Hii leo pia kusimama huko imara mbele ya kambi ya adui ni katika vipaumbele muhimu vya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Vipaumbele hivyo ni matokeo ya uvumilivu, muqawama na kufungamana na matukufu ya kidini na utamaduni halisi wa Uislamu.

Tajriba ya miaka yote hii inaonyesha kuwa itikadi na kuamini misingi ya dini katika mazingira magumu daima imewafanya wananchi Waislamu wa Iran kuweza kujiamini katika kukabiliana na hali ngumu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana vipaumbele hivyo vikawa na nafasi isiyopingika katika mapinduzi ya taifa la Iran katika kukabiliana na madola ya kibeberu na ya uistikbari wa dunia.

Kuhusiana na suala hilo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kuashiria ushiriki mkubwa wa raia wanamapambano wa Iran katika maandamano ya tarehe 22 Bahman (11 Februari) na kadhalika ushiriki wao katika mazishi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC alisisitiza kuwa, ustahmilivu wa raia wa Iran mbele ya mashinikizo ya kutisha ya Marekani, umewastaajabisha mno walimwengu.

Ukweli ni kwamba msimamo wa raia wa Iran mbele ya madola ya kibeberu unatokana na mafundisho ya Mapinduzi na maelekezo ya dini ya Uislamu. Nukta hizo ndizo zinadhamini ushindi wa Iran mbele ya madola ya kibeberu na ya uistikbari wa dunia.Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu, wananachi wa Iran wamekuwa wakishiriki kwa kishindo katika masuala yote yanayohitajia hamasa ya ushiriki wa wananchi.

Aidha katika kipindi chote cha miongo minne ya uhai wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu taifa hili sambamba na kufungamana na misingi ya kusimama kidete mbele ya mfumo wa kibeberu na kwa muono wa kimapinduzi, limeonyesha kwamba madamu bado kuna moyo wa hamasa, hakuna taifa lolote litakaloweza kuiletea madhara Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa miaka yote 41 iliyopita kipaumbele cha siasa za serikali ya Marekani kimekuwa ni kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu, ili kwa njia hiyo iweze kuusambaratisha mfumo wa Kiislamu nchini hapa kama inavyoota. Katika uwanja huo, Washington imepanga na kutekeleza njama nyingi hata hivyo haijaweza kusimamisha harakati kubwa ya Mapinduzi wala wimbi la mwamko wa Kiislamu.

Licha ya njama zote hizo, wimbi la matukio ya kieneo katika uga wa muqawama wa wananchi limezidi kushika kasi na harakati hiyo kubwa imekuwa sababu ya kuleta mabadiliko ya kistratijia katika mlingano wa kieneo. Matokeo ya mabadiliko hayo ni kushindwa mtawalia kwa Marekani na utawala haramu wa Kizayuni mbele ya kambi ya muqawama wa Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi.

Kama alivyosisitiza awali Kiongozi Muadhamu, ahadi ya Mwenyezi Mungu, ni kwamba  bila shaka adui atashindwa tu.

...........
340