Main Title

source : ParsToday
Jumatatu

17 Februari 2020

08:23:37
1011043

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumapili alizungumza na waandishi habari wa ndani ya nje ya nchi hapa mjini Tehran na kuzungumzia masuala mengi kuanzia jibu kali la Iran dhidi ya jinai ya Marekani ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, uchaguzi ujao wa Bunge la Iran na masuala mengine ya kikanda na kimataifa.

(ABNA24.com) Mazungumzo ya Rais na waandishi wa habari yamejikita zaidi katika masuala makuu matatu. Kwanza ni utambulisho wa kibeberu wa Marekani na malengo ya siri nchi hiyo ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Lengo la mashinikizo hayo ya kutaka kuharibu makubaliano ya JCPOA ni kuzidisha mashinikizo ya kiwango cha juu kwa mujibu wa mahesabu yasiyo sahihi kwamba yataifanya Iran ilegeze msimamo na kulazimika kuketi kwenye meza ya mazungumzo na serikali ya Washington, suala ambalo kamwe halitatimia.

Kuhusuana na kadhia hii, Rais Rouhani amewaambia waandishi wa habari kwamba: "Wamarekani walikuwa wakidhani kwamba, mashinikizo ya kiwango cha juu yanaweza kuiburuta Iran kwenye meza ya mazungumzo. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu imetoa kauli yake waziwazi mbele ya dunia nzima tena kwa kuweka kifua mbele, kwa uwezo na heshima na kamwe haitaburutwa kwenye meza ya mazungumzo."

Nukta ya pili katika mazungumzo ya Rais Rouhani na waandishi wa habari ni kuhusu masuala ya usalama na changamoto zilizosababishwa na Marekani kwenye eneo la magharibi mwa Asia kutokana na sera zake za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja. Kuhusu maudhui hii Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameshiria nukta kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na Mpango wa Amani wa Hormuz kwa ajili ya kuimarisha usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Tunapotupia jicho matukio ya miaka kadhaa ya hivi karibuni tunaona kuwa, mbali na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, nchi kama Saudi Arabia zimekuwa na mchango mkubwa katika kuvuruga amani na usalama wa magharibi mwa Asia. Ni kwa karibu miaka 5 sasa tangu Saudi Arabia ilipoanzisha vita na mauaji ya raia huko Yemen.

Riyadh inaendelea kung'ang'ania misimamo yake ya vita na mauaji ya raia wasio na hatia katika nchi hiyo jirani lakini ni wazi kuwa, sera hizo zisizo sahihi zinaitia ghara na hasara kubwa na kamwe haiwezi kushinda vita vya Yemen. Sasa kuna ishara za wazi za kushindwa Saudi Arabia katika vita hivyo ambavyo wahanga wake halisi ni raia wasio na hatia yoyote.

Kuhusiana na masuala haya ya usalama, Rais Rouhani amesema: Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikitilia mkazo suala la amani na usalama wa eneo la magharibi mwa Asia na shahidi Qassem Soleimani aliyeuawa kigaidi na Marekani alikuwa miongoni mwa makamanda waliofanya jitihada kubwa kuimarisha usalama huo.

Amesisitiza kuwa Shahid Soleimani aliuawa kigaidi na Wamarekani akiwa safarini nchini Iraq kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo na kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq.     

Sehemu ya tatu ya mazungumzo ya Rais Rouhani na waandishi habari ambayo ilitawaliwa na maswali na majibu, ilihusu uchaguzi wa Bunge la Iran ulipangwa kufanyika Ijumaa ijayo.

Kuhusiana na maudhui hii Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amejibu madai yaliyotolewa na Brian Hook anayehusika na meza ya Iran katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani aliyesema kuwa uchaguzi wa Iran ni wa kimaonyesho tu. Rais Rouhani amesema: Demokrasia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni halisi na ya kweli zaidi kuliko ile ya nchi nyingine duniani ziliwemo hata nchi za Magharibi na Marekani.

Ukweli huu umesisitizwa na msemaji wa Baraza la Walinzi wa Katiba, Abbas-Ali Kadkhodaei katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter akijibu madai ya Brian Hook.

Kadkhodaei amesema: "Katika hali ambayo Donald Trump angali anaandamwa na kashfa ya kuomba msaada wa madola ya kigeni kwa ajili ya kuwashinda wapinzani wake katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016, Brian Hook anajitokeza na kutoa madai yasiyo na msingi kuhusu uchaguzi wa Iran. Kiwango cha juu zaidi cha ushiriki wa wapigaji kura katika chaguzi za Bunge la Wawakilishi (Kongresi) la Marekani ni asilimia 50.4 hapo mwaka 1914! Wairani hawahitajii imla ya demokrasia ya kimarekani."

Tajiriba ya miaka 41 iliyopita inaonyesha kuwa, uchaguzi zinazofanyika kwa kushirikisha idadi kubwa ya watu nchini Iran zinawachukiza maadui wa Jamhuri ya Kiislamu. Kwa sababu hiyo Marekani daima imekuwa ikiwataka wananchi wa Iran wasishiriki kwa wingi katika chaguzi zinazofanyika hapa nchini. 

...........
340