Main Title

source : parstoday
Jumamosi

9 Mei 2020

09:59:37
1034994

Kama ilivyokuwa ikitarajiwa, Rais Donald Trump wa Marekani ametumia mamlaka yake ya veto kuukataa muswada uliopitishwa na Kongresi, ambao unataka mamlaka aliyopewa ya kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya Iran yapunguzwe.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kufuatia hatua hiyo ya Trump, muswada huo sasa unahitaji theluthi mbili za kura za uungaji mkono za bunge hilo la Marekani ili uweze kuwa sheria moja kwa moja bila kuhitaji kusainiwa na rais wa nchi hiyo. Trump amesema katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House: Leo nimeupigia kura ya veto muswada ambao ulikuwa ukinipa muongozo wa kuacha kutumia vikosi vya ulinzi vya Marekani katika uhasama na Iran.

Trump amedai kuwa, amechukua uamuzi huo kutokana na kuwa, muswada huo si wa kimantiki, ni wa udhalilishaji na unaopuuza mamlaka ya Rais ya kuchukua uamuzi wa kuanzisha vita. Tarehe 14 ya mwezi uliopita wa Aprili, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi alisaini azimio la kupunguza mamlaka ya rais wa nchi hiyo ya kuanzisha vita dhidi ya Iran ambalo lilipitishwa na baraza hilo mwezi Machi.

Vitisho vya kuanzisha vita dhidi ya Iran ambavyo Rais wa Marekani Donald Trump alivitoa baada ya mauaji ya kigaidi ya Kamanda Qassem Soleimani na watu alioandamana nao yaliyofanywa na jeshi la kigaidi la Marekani, vilizidi kulitia wasiwasi bunge la nchi hiyo na kuwafanya wabunge wa chama cha Democrat wachukue hatua ili kupunguza mamlaka ya Trump yanayohusiana na kuanzisha vita dhidi ya Iran.

Itakumbukwa Ijumaa ya tarehe 3 Januari 2020, Luteni Jenerali Shahidi Qassem Soleimani, kamanda wa wakati huo wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al-Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq la Hashdu-Sha'abi pamoja na wanamuqawama wenzao kadhaa waliokuwa pamoja nao waliuawa shahidi katika shambulio la kinyama la anga lililofanywa na vikosi vya jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Iran ilitoa jibu kali kwa ugaidi huo baada ya kushambulia kwa makombora kambi ya jeshi la Marekani ya Ain al-Assad magharibi mwa Iraq ambapo zaidi ya askari 100 wa Marekani walipata madhara na matatizo ya ubongo.

Hata kama baada ya jibu hilo kali la Iran, Trump alilegeza msimamo wake wa kutaka kuvishambulia vituo 52 vya utamaduni hapa Iran, lakini hata hivyo kwa siku kadhaa kulikuwa na wasiwasi wa kutokea vita vikubwa katika eneo la Asia Magharibi. Wasiwasi huo ndio uliowasukuma akthari ya wawakilishi wa Bunge la Marekani wakiwa na lengo la kuzuia kuibuka vita vingine katika eneo, wapasishe muswada kupunguza mamlaka ya Rais.

Hata hivyo Trump kama ilivyokuwa kwa Marais wengine wa Marekani waliotangulia ambao walisimama kidete kupinga kupunguzwa mamlaka ya Rais, naye ametumia veto kuukataa muswada wa Kongresi unaotaka kumpunguzia mamlaka ya kuanzisha vita dhidi ya Iran. Trump na washauri wake wamedai kwamba, muswada huo wa Kongresi unapuuza mamlaka ya Rais wa nchi kwa ajili ya kulinda usalama wa taifa, wanajeshi wa Marekani na waitifaki wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo, katiba ya Marekani imeliweka suala la kutangaza vita au sulhu katika mamlaka ya Kongresi ya nchi hiyo. Pamoja na hayo katika kipindi cha miaka 230 iliyopita, Marais wa Marekani wamepora mamlaka ya Kongresi ya nchi hiyo kuhodhi wao.

Uporaji huo wa mamlaka ya Kongresi ukiacha vita vitano, umepelekea mamia ya vita vilivyoanzishwa na serikali ya Marekani kutokuwa na kibali cha Kongresi. Kila vita kati ya vita hivyo vimekuwa na hasara kubwa za kiroho na mali kwa wananchi wa Marekani ambapo mfano wa wazi kuhusiana na jambo hilo ni gharama ya dola trilioni 7 katika vita nchini Afghanistan na Iraq.

Ili kuzua kukaririwa maafa kama hayo, baadhi ya wawakilishi wa Bunge la Marekani (Kongresi) wanafanya juhudi za kupunguza mamlaka ya Rais na kuhakikisha yanabakia kuwa kama ilivyoanishwa katika katiba ya nchi hiyo. Hata hivyo hadi sasa hawajafanikiwa katika hilo. Kwa kuzingatia kwamba, Kongresi ya sasa haina kura za kutosha za uungaji mkono mwa kubatilisha veto ya Rais, ni jambo lililo mbali kwa muswada huo kuvuka kigingi cha Rais kwani unahitaji theluthi mbili za kura za uungaji mkono za bunge hilo la Marekani ili uweze kuwa sheria moja kwa moja bila kuhitaji kusainiwa na rais wa nchi hiyo.

342/