Main Title

source : parstoday
Jumatano

8 Julai 2020

10:42:05
1053450

Sisitizo la Umoja wa Mataifa la kukiuka sheria mauaji dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani

Mnamo Januari 3 mwaka huu, jeshi la kigaidi la Marekani kwa amri ya Rais wa nchi hiyo Donald Trump lilitenda jinai kwa kumuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran akiwa uraiani nchini Iraq tena akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Baghdad.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Katika jinai hiyo aliuawa shahidii pia Abu Mahdi al-Mohandes, Naibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hashdu al-Shaabi pamoja na watu waliokuwa wamendamana nao. Tukio hilo lilitokea jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Jinai hiyo ya Marekani ilikabiliwa na ukosoaji mkubwa na kulaaniwa kimataifa. 

Katika radiamali ya hivi karibuni karibuni kuhusiana na kadhia hiyo, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda shahidi wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) yalikiuka sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa. Agnès Callamard amesema hayo katika ripoti yake juu ya mauaji hayo ya kigaidi na kubainisha kuwa, Marekani imeshindwa kutoa ushahidi wa kutosha wa kuyapa nguvu madai yake kwamba Jenerali Soleimani alikuwa tishio kwa taifa hilo. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka kuwajibishwa Marekani kutokana na mauaji ya kuratibiwa na yenye malengo maalumu ya ndege za kijeshi na kuwekwa sheria kali za silaha.

Mtaalamu huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "dunia hivi sasa ipo katika kipindi nyeti cha kutizamwa upya matumizi ya droni. Hata hivyo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijachukua hatua yoyote huku jamii ya kimataifa kwa kujua au kutojua imeendelea kunyamaza kimya."

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa ambaye Alkhamisi ijayo anapaswa kuwasilisha faili la mauaji hayo mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ili nchi wanachama waijadili ameeleza kwamba, "mauaji ya kigaidi dhidi ya Jenerali Qassem Soleimani yalikanyaga kikamilifu vigezo vinavyohusiana na nchi kutumia nguvu za kijeshi nje ya mipaka yake."

Miaka miwili iliyopita Marekani ilijitoa katika baraza hilo la haki za binadamu ikilalamikia misimamo iliyo dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ndani ya baraza hilo.

Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon amri ya kuuawa Luteni Jenerali Qassem Soleimani na watu alioandamana nao ilitolewa na Rais Donald Trump. Kisingizio cha Trump cha kutekeleza jinai hiyo kilielezwa kuwa, Luteni Jenerali Soleiman alielekea Iraq kwa ajili ya kupanga mipango ya kutekeleza mashambulio dhidi ya Marekani na vituo vyake vya kijeshi nchini Iraq na kwamba, shambulio hilo la anga dhidi ya kamanda huyo lilikuwa ni hatua ya kujikinga na kuzuia mashambulio dhidi yake. Hata hivyo madai hayo ya Trump yamepingwa bvikali na viongozi wa Iraq.

Adil Abdul-Mahdi, aliyekuwa Waziri Mkuu wa muda wa wakati huyo wa Iraq Januari 5 mwaka huu alitangaza katika kikao cha Bunge kwamba, Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa ameelekea Baghdad kwa ajili ya kupeleka ujumbe wa Iran na jibu la Tehran kwa barua ya Saudi Arabia, barua ambayo iliifikia Tehran kupitia kwa serikali ya Baghdad. Kwa msingi huo inafahamika wazi kwamba, madai ya Washington ni uongo mtupu, kwani baadaye ilikuja kufahamika pia kwamba, takribani mwaka mmoja na nusu kabla serikali ya Trump ilikuwa na nia ya kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Ukweli ni kuwa, ushahdi mpya na matamshi ya viongozi wa ngazi za juu wa Marekani yanaonyesha kuwa, serikali ya Washington ilikuwa imechukua uamuzi wa kumuua Qassem Soleimani miezi kadhaa nyuma na ilichokuwa inasubiri ni muda mwafaka tu wa kutekeleza mpango wake huo wa kijinai. Kanali ya Televisheni ya NBC ya Marekani, tarehe 13 Januari mwaka huu iliripoti kwamba, Juni mwaka jana 2019 yaani miezi saba kabla, Trump alitoa agizo lenye masharti la kuuawa Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Baada ya Iran kuitungua ndege ya kijasusi ya Marekani aina ya Global Hawk, Trump alitoa maagizo yasemayo: Kama mashambulio ya vikosi vya Iran au makundi yenye mfungamano na taifa hilo yatapelekea kuuawa wabnajeshi au raia wa marekani, basi Qassem Soleimani alengwe na kuuawa. Baada ya jenerali huyo kuuawa Trump alitoa madai yasiyo na ushahidi wala nyaraka akisema kuwa, sababu ya kufanywa mauaji hayo tishio la karibu na tarajiwa la kamanda huyo dhidi ya vikosi vya Marekani na kwamba, eti alikuwa akiandaa mipango ya kushambulia balozi nne za Marekani. Hii ni katika hali ambayo, matamshi ya viongozi wa Marekani n ahata ripoti rasmi ya ikulu ya White House inakinzana wazi na madai hayo ya Trump.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kwa mtazamo wa washauri wa kijeshi na kiusalama wa Trump ni kwamba, kuwepo kwa wakati mmoja Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Mohandes mjini Baghdad wakiwa makamanda wawili muhimu wa Kiirani na Kiiraqi ambao walikuwa na nafasi muhimu katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na wakati huo huo ni kizingiti kikuu cha Marekani kufikia malengo yake katika eneo la Asia Magharibi, ni fursa ambayo Washington isingeweza kuipoteza. Kwa muktadha huo, Marekani ilitenda jinai kubwa na ya kidhulma kwa kulishambulia kwa bomu gari lililokuwa limembeba Qassem Soleimani pamoja na watu aliokuwa ameandamana nao.

Kwa msimamo wa Agnès Callamard ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kukiuka sheria mauaji dhidi ya Qassem Soleimani yaliyofanywa na Marekani, hakubakii shaka yoyote kwamba, serikali ya Trump ni mkiukaji mkuu wa sheria za kimataifa na ikiwa na lengo la kusukuma mbele gurudumu la malengo ya siasa zake za utumiaji mabavu haiheshimu wala kuzingatia sheria au kanuni yoyote ile.

342/