Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

25 Desemba 2020

19:10:23
1099507

Ujumbe wanaokusudia kuufikisha Wairaqi kwa maandalizi ya kukumbuka kuuawa shahidi Kamanda Qassem Suleimani

Wananchi na makundi mbalimbali ya Wairaqi wanajiandaa kwa hauli na maadhimisho ya mwaka wa kwanza tangu alipouliwa shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani na Abu Mahdi Al-Muhandis.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Usiku wa kuamkia tarehe 3 Januari 2020, utawala wa kigaidi wa Marekani ulitenda jinai ya kinyama karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq ya kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Abu Mahdi Al-Muhandis, Naibu Mkuu wa vikosi vya Al-Hashdu-Sha'abi pamoja na wenzao wengine wanane. Hivi sasa wakati unakaribia kutimia mwaka mmoja tangu Kamanda Suleimani na Al-Muhandis walipouliwa shahidi, wananchi na makundi tofauti ya Wairaqi wamekuwa wakifanya hafla mbalimbali za kuwakumbuka na kuwaenzi mashahidi hao, sambamba na kufanya maandalizi makubwa kwa ajili ya maadhimisho ya kuuawa shahidi makamanda na majemadari hao wa muqawama.

Suali muhimu linaloulizwa ni, ratiba na hafla zinazoandaliwa na wananchi na makundi ya Wairaqi kwa ajili ya kumuenzi Luteni jenerali Qassem Suleimani zinakusudia kufikisha ujumbe gani?

Inavyoonekana, ujumbe mmoja muhimu sana uliokusudiwa kufikishwa na hafla hizo pamoja na maandalizi ya hauli ya mashahidi hao, ni imani ya moyoni na uelewa wa dhati walionao wananchi na makundi ya Wairaqi kwa mchango usio na kifani uliotolewa na Shahid Qassem Suleimani na Abu Mahdi Al-Muhandis kwa mhimili wa muqawama na hasa kwa taifa la Iraq. Baada ya uvamizi ulioandaliwa kimkakati na mashambulio yaliyoratibiwa na kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) dhidi ya Iraq, wakati madola makubwa yakiwemo hata yale yanayojigamba kuwa yanapambana na ugaidi yaliamua kuiacha mkono na kutoipa msaada wowote Iraq, Kamanda Qasem Soleimani na vikosi vilivyokuwa chini ya uongozi wake walielekea haraka na bila ajizi huko Iraq; na kwa kushirikiana na vikosi vya Al-Hashdu-Sha'abi na makamanda wake wakatoa mchango mkubwa kwa ajili ya kulinda ardhi yote ya nchi hiyo.

Ujumbe mwengine muhimu ni wa uungaji mkono wa sehemu kubwa ya jamii ya Wairaqi na mirengo mbalimbali ya nchi hiyo kwa njia na harakati ya muqawama ndani ya nchi hiyo na katika eneo. Maadhimisho ya kumuenzi shahid Qassem Suleimani yanayofanywa na wananchi wa Iraq yanathibitisha msimamo na sisitizo la wananchi hao la kuendeleza njia ya muqawama; na kwamba kuuliwa shahidi makamanda na majemadari wa muqawama, si tu hakujakwamisha wala kusimamisha harakati hiyo, lakini kumezidisha pia hamasa na hamu ya kuendeleza njia hiyo.

Fadhil Jabir al-Fatlawi, mbunge wa Iraq wa mrengo wa al-Fat-h ameashiria hafla ya kuwaenzi makamanda hao wa muqawma iliyofanywa Jumamosi iliyopita na bunge la nchi hiyo na kueleza kwamba, ujumbe muhimu uliofikishwa na hafla hiyo ni kuisistizia Marekani kwamba, sisi tungali tumeshikamana na njia ya jihadi iliyoanzishwa na shahid Qassem Suleimani na shahid Abu Mahdi Al-Muhandis pamoja na makamnada wenzao.

Ujumbe mwingine wanaokusudia kufikisha wananchi wa Iraq kwa kuadhimisha kuuawa shahidi Kamanda Qassem Suleimani na Abdu Mahdi Al-Muhandis ni kwamba, wananchi na mirengo mbalimbali nchini Iraq wangali wanafuatilia suala la kuondoka wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo. Marekani ilikiuka uhuru na mamlaka ya kujitawala ya Iraq kwa kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Wairaqi; na kwa kumuua shahidi Abu Mahdi Al-Muhandis, ambaye alikuwa mmoja wa makamanda wa muqawama wa Iraq. Ijapokuwa mnamo tarehe 5 Januari 2020 bunge la Iraq lilipitisha mpango wa kuwataka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo, lakini kwa sababu tofauti, mpango huo haujafuatiliwa na serikali ya Iraq kwa uzito unaostahiki.

Hivi sasa wananchi wa Iraq wanawaadhimisha mashahidi hao wa muqawama huku wakitilia mkazo tena takwa lao la kutaka askari vamizi wa jeshi la kigaidi la Marekani waondoke nchini mwao. Abu Dhiyaa As-Saghir, mkuu wa ofisi za Al-Hashdu-Sha'abi katika mikoa ya Iraq anasema hivi kuhusiana na suala hilo: "Jumbe zinazokusudiwa kufikishwa katika maadhimisho ya kutimia mwaka mmoja wa kuuawa shahidi makamanda wa ushindi dhidi ya ugaidi, ambayo yatajumuisha pia maandamano ya mamilioni ya watu yatakayofanyika mnamo siku zijazo mjini Baghdad, ni kusisitiza tena takwa la kuwataka askari wa Marekani waondoke haraka katika ardhi ya Iraq.

Nukta nyingine muhimu na ya kuzingatiwa ni kwamba, wananchi na makundi ya Iraq wameamua kutumia kaulimbiu ya "Kufa Shahidi na Kujitawala"  kwa ajili ya maadhimisho ya kuwaenzi shahid Qassem Suleimani na shahid Abu Mahdi Al-Muhandis, kaulimbiu ambayo inatilia mkazo ulazima wa kuwatimua wavamizi na wakaliaji kwa mabavu wa ardhi ya Iraq na kurejesha mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo.../

342/