Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

4 Januari 2021

09:39:27
1102943

Mkuu wa IRIB: Kamanda Suleimani alikuwa dhihirisho la imani, taqwa na kutawakali kwa Allah

Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB amesema, Luteni Jenerali Qassem Suleimani alikuwa dhihirisho la imani, taqwa na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na alifanya jitihada uhai wake wote katika kushikamana na njia ya fikra ya Imam Khomeini na Ayatullah Khamenei.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Abdulali Ali-Asgari, Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika kongamano la kielimu la "Vyombo vya Habari na Njia ya Fikra ya Suleimani" lililofanyika leo katika Ukumbi wa Makongamano ya Kimataifa wa IRIB hapa mjini Tehran.

Dakta Asgari ameongeza kuwa, Shahidi Suleimani, iwe ni wakati alipokuwa akihudumu kama kamanda shujaa, muumini na mwenye ikhlasi katika vita vya miaka minane vya Kujihami Kutakatifu, au wakati alipokuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alichukua hatua kubwa na za kistratejia kwa ajili ya Muqawama wa Kiislamu.

Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Iran amebainisha kuwa, kamanda Suleimani alikuwa muumini na alichukua hatua kivitendo kulingana na misingi ya imani yake; na Mwenyezi Mungu alimfungulia njia na kumtunukia riziki isiyokwisha.

Akihutubia washiriki wa kongamano hilo, Mkuu wa kitengo cha matangazo ya ng'ambo cha IRIB Peyman Jebeli ambaye pia ni mkuu wa kamati ya kielimu ya kongamano hilo la "Vyombo vya Habari na Njia ya Fikra ya Suleimani" amesema kamanda Qassem Suleimani alikuwa na ushujaa, ujasiri, uelewa, uwezo wa kutabiri na uono wa mbali wa mambo; na kwamba sifa hizo zina umuhimu mkubwa mno kwa mtazamo wa vyombo vya habari.

Dakta Jebeli amebainisha kuwa, IRIB ambacho ni chombo kikuu na kipana zaidi cha habari cha mhimili wa muqawama, kikiwa na majukumu ya kutekeleza kwa upande wa ndani na kimataifa imelikubali jukumu na lengo inalopaswa kulifikia la kuitangaza na kuiarifisha kupitia vyombo vya habari njia ya fikra ya Suleimani.

Katika kongamano hilo la siku mbili lililoandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha IRIB na shakhsia kadhaa wa kielimu na kiutamaduni nchini, wazungumzaji wamewasilisha makala na kuhutubia juu ya mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na Njia ya Fikra ya Suleimani na Diplomasia ya Vyombo vya Habari, Njia ya Fikra ya Suleimani na Nguvu Zisizo za Kijeshi, Njia ya Fikra ya Suleimani na Muqawama wa Vyombo vya Habari n.k.

Katika kongamano hilo kimezinduliwa pia kitabu cha maisha ya Shahidi Qassem Suleimani, alichoandika yeye mwenyewe kiitwacho "Nilikuwa Sihofu Chochote", ambacho kimepambwa kwa dibaji iliyoalifiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei...

342/