Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

27 Mei 2022

18:39:24
1261469

Putin: Vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia vinaziathiri nchi zenyewe za Magharibi

Rais Vladimir Vladimirovich Putin wa Russia kwa mara nyingine tena amezilaumu nchi za Magharibi kwa kuiwekea nchi yake vikwazo kwa kisingizio cha vita vya Ukraine na kusema kuwa, vikwazo hivyo vinaziathiri nchi zenyewe za Magharibi.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Rais Putin alisema hayo jana Alkhamisi katika kikao kikuu cha Baraza la Kiuchumi la Eurasia na kuongeza kuwa, vikwazo hivyo vya Magharibi dhidi ya Russia, mbali na kuziathiri nchi hizo za Magharibi, vinaziathiri pia nchi nyingine ulimwenguni.

Aidha amezilaumu vikali nchi za Magharibi kwa kujaribu kupora mali za Russia na kutaka kuzipeleka nchini Ukraine.

Hivi karibuni nchi nne wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) zilitazamiwa kuwasilisha rasmi katika umoja huo barua ya kutaka mali na fedha za Russia zilizozuiliwa na EU zitumiwe kuijenga upya Ukraine baada ya kumalizika vita.

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei, Ukraine ilifanya makadirio ya karibu dola bilioni 600 zinazohitajika kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo; na kwa kuzingatia kuendelea kwa vita, inatazamiwa kuwa kiwango hicho kitaongezeka na kuwa kikubwa zaidi.

Shirika la habari la IRNA liliripoti kuwa, katika barua yao hiyo iliyotazamiwa kuwasilishwa Jumanne wiki hii katika mkutano wa mawaziri wa fedha wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, nchi nne za Lithuania, Slovakia, Estonia na Latvia zilieleza kwamba, sehemu kubwa ya gharama za kuikarabati na kuijenga upya Ukraine ikiwemo gharama ya fidia kwa waathirika wa vita vinavyoendelea Ukraine hivi sasa inapasa igharamiwe na Russia.


342/