Main Title

source : Parstoday
Jumapili

30 Oktoba 2022

19:33:24
1318878

Kushindwa kwa mradi wa Marekani wa "kuangamiza Iran"

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Wizara ya Intelijensia ya Iran na Shirika la Upelelezi la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imeweka wazi nafasi ya Marekani katika machafuko ya hivi karibuni hapa nchini.

Taarifa hiyo ya pamoja imesisitiza kuwa: Nyaraka zilizopo za kijasusi zinaonyesha kuwa, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa ushirikiano na mashirika ya kijasusi ya washirika na vibaraka wake, walipanga kuzusha machafuko na pia kutayarisha uwanja wa kuzidishwa mashinikizo ya kigeni dhidi ya Iran.

Taarifa za kiintelijensia zinaonesha kuwa, CIA imekuwa na ushirikiano wa karibu na Idara ya Ujasusi wa Kigeni ya Uingereza (MI6), shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD), Idara ya Ujasusi wa Kigeni wa Saudia na nchi nyingine kadhaa katika kutekeleza mpango huo. 

Ushahidi na tajiriba ya kihistoria vinaonyesha kuwa serikali ya Marekani imekuwa mojawapo ya waungaji mkono wakuu wa machafuko na ghasia za mitaani nchini Iran katika miongo kadhaa iliyopita na kwa uchache katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mfano, kufuatia mabadiliko yaliyofanyika katika mfumo wa utoaji wa ruzuku ya petroli na urekebishaji wa bei ya bidhaa hiyo tarehe 15 Novemba 2019, kulifanyika maandamano na mikusanyiko katika baadhi ya miji ya Irani, na baadaye serikali ya Marekani ilikiri kwamba ilihusika katika kuchochea machafuko hayo. Brian Hook, aliyekuwa akihusika na masuala ya Iran katika Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya zamani ya Marekani alikiri waziwazi na kutangaza kuwa: "Tulitoa zana za mawasiliano kwa wafanya ghasia nchini Iran, kwa kadiri kwamba waliendeleza mawasiliano yao hata baada ya kukatwa mawasiliano ya intaneti nchini humo." 

Matukio na machafuko ya wiki chache zilizopita nchini Iran pia yanaonesha kuwa, maadui ikiwemo Marekani, wanatumia masuala kama vile haki za binadamu na haki za wanawake kama fursa ya kuibua machafuko, mifarakano na kuzusha migawanyiko katika jamii ya Iran na wamewekeza tangu hapo kabla kwa ajili ya njama hiyo. Uchunguzi wa vyombo vya habari na mipango ya baadhi ya vituo vya kifikra vya Marekani pia unathibitisha kwamba, serikali ya nchi hiyo imekuwa ikifanya mikakati ya kuzusha hali ya kutoridhika baina ya wananchi nchini Iran kwa malengo maalumu. Kwa mfano, taasisi ya wanafikra ya Marekani "Foundation for Defense of Democracies, FDD kwa kifupi, ambayo ina jukumu muhimu katika kuunda sera ya nje ya Washington kuhusiana na Iran, Mei 23, mwaka huu wa 2022 yaani karibu miezi minne kabla ya machafuko ya hivi karibuni na katika hali ambayo kulikuwapo baadhi ya maandamano ya hapa na pale ya kupinga ongezeko la bei ya baadhi ya bidhaa nchini Iran, iliandika ripoti iliyopewa kichwa maneno: "Maandamano Yapamba Moto Nchini Iran, Serikali ya Joe Biden Inaweza Kusaidia" na kuishauri serikali na maafisa wa Marekani kuyapa uzito na kuyaunga mkono maandamano kama hayo.

Miongoni mwa mapendekeo yaliyotolewa na taasisi ya FDD ambayo yamefanyiwa kazi na maafisa wa serikali ya Washington ni pamoja na kusimamisha mchakato wa mazungumzo ya nyuklia ya Vienna, kuunga mkono maandamano hayo kwa kiasi kikubwa, kuibua suala la ukiukaji wa haki za binadamu na kutoa huduma ya intaneti ya Starlink kwa Iran.

Katika taarifa ya hivi karibuni ya mashirika ya ujasusi ya Iran, pia imetajwa kuwa idara za kijasusi za Magharibi na Kizayuni zinatoa kozi za mafunzo ya pamoja ya wakufunzi wa "vita mseto" (Hybrid warfare) kwa idadi kubwa ya vibara wao ambao wamewapa jukumu la kuhamisha mafunzo hayo kwa wengine na kisha kuyatekeleza kivitendo katika sura ya makundi. Vita mseto (Hybrid Warfare) ni mkakati wa kijeshi ambao ni mchanganyiko wa vita vya kisiasa, vita vya kitamaduni, vita vya mtandaoni, kueneneza habari za uwongo, vita vya diplomasia, vita vya mahakama, kuingilia chaguzi za nchi za kigeni, kuvuruga muundo wa idadi ya watu, kuwapa hifadhi wakimbizi wa nchi husika, kuzusha hitilafu na migongano ya kidini na kadhalika. Mdhamini na msimamizi wa kozi hizo ni Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ambayo hutumia CIA na taasisi zinazoitwa "zisizo za kiserikali na vituo vya wanafikra" kutekeleza mpango huo.

Uwanja mwingine mkuu wa harakati za idara za ujasusi za adui kwa ajili ya kuzusha au kuchochea machafuko nchini Iran ni kijaribu kuathiri matabaka tofauti kama vile walimu, wafanyakazi na wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kuunda makundi bandia na maovu na kuongoza au kuelekeza harakati za kuyatumia vibaya matabaka hayo. Kwa mfano tu, kwa mujibu wa ufuatiliaji uliofanyika katika mtandao wa kijamii wa Twitter, kati ya tarehe 11 Septemba 2022 na 12 Oktoba 2022 pekee, zaidi ya watumiaji elfu hamsini wa lugha ya Kifarsi wenye utambulisho bandia waliundwa kwenye mtandao huo wa Twitter kufanya harakati za mtandaoni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika suala hili, Kit Klarenberg, mtaalamu wa Uingereza na aliyebobea katika uwanja wa kuchambua nafasi ya vifaa vya upelelezi katika kuunda mtazamo wa umma, aliandika makala kwenye tovuti ya uchambuzi wa habari ya The Cradle kwamba: "Mkakati muhimu" wa wanasaikolojia walioajiriwa na Pentagon ni kuzindua na kuelekeza vyombo vya habari bandia vinavyotengeneza maudhui kwa lugha ya Kifarsi. Shughuli hizi dhidi ya Irani hufanyika kwenye majukwaa maarufu ya mtandaoni kama vile "Twitter", "Facebook", "Instagram", "YouTube" na hata "Telegram"."

Mwandishi wa makala hiyo ameongeza kuwa, katika baadhi ya matukio, "waandishi wa habari na wataalamu feki" huonekana kwenye mitandao ya kijamii wakiwa na wafuasi (followers) wengi na hata picha zao za "profile" zinaundwa kwa kutumia akili mashine (artificial intelligence).

Kwa hakika, licha ya hatua zote hizi na mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na ya vyombo vya habari ya maadui wa mhimili wa Kimagharibi, Kiebrania na Kiarabu unaoongozwa na Marekani, umakini wa taifa na jamii ya vyombo vya kijasusi ya Iran, mara hii kama ilivyokuwa huko nyuma, imezuia kufikiwa kwa malengo ya maadui.

Wizara ya Intelijensia na Shirika la Ujasusi la Jeshi la IRGC pia wamesisitiza kwamba: "Mradi wa Kuangamizi Iran" umeshindwa kwa fedheha; Mradi huo ndio uleule uliotekeleza hapo awali huko Afghanistan, Iraqi, Syria, Yemen na Libya, lakini umefeli na mushindwa katika Iran yenye nguvu.