Main Title

source : Parstoday
Jumatano

9 Novemba 2022

18:24:14
1321770

Iran: Majibu yetu kwa uvamizi wa maadui yatakuwa makali sana

Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu la Iran ametoa onyo kali kwa maadui na kuwaambia: Mnapaswa kuelewa vyema kwamba iwapo mtafanya kosa lolote dhidi ya Iran ya Kiislamu, basi majibu mtakayopata yatakuwa makali sana.

Brigedia Jenerali Kioumars Heydari alisema hayo jana Jumanne wakati alipokuwa anakagua eneo la mpakani la Taybad la mashariki mwa Iran na kuongeza kuwa, magenge ya wahalifu ambayo baadhi ya wakati yanashirikiana na baadhi ya watu wa nchi jirani yalifanya uhalifu huko nyuma na kupata majibu makali kutoka kwa Iran.

Kamanda huyo wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu la Iran pia amesema, kupelekwa jeshi mpakani hakuwezi kuhesabiwa kuwa ni tishio bali lengo lake ni kuimarisha usalama na kukabiliana vilivyo na magenge ya wahalifu.

Brigedia Jenerali Heydari aidha amesema, brigedi za kikosi cha 77 cha Khurasan ndizo zilizoko kwenye mipaka ya mashariki mwa Iran na zimejiandaa vilivyo kukabiliana na uadui wowote ule kutoka nje.

Mkoa wa Khorasan Razavi wa kaskazini mashariki mwa Iran una mpaka wa zaidi ya kilomita 300 na Afghanistan.

Kilomita 90 za mpaka huo ziko kwenye wilaya ya Tayybad iliyokaguliwa jana Jumanne na Brigedia Jenerali  Kioumars Heydari, Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

342/