Main Title

source : Parstoday
Jumatano

9 Novemba 2022

18:25:58
1321773

Syria: Tutaendelea na mapambano dhidi ya ugaidi hadi tutakapoisafisha ardhi yetu yote

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetangaza kuwa, mapambano dhidi ya magenge ya kigaidi huko kaskazini na kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu yataendelea hadi kila shibri ya ardhi ya Syria itakaposafishwa kikamilifu.

Hayo yamekuja baada ya jeshi la Syria kusambaratisha kambi za mafunzo za magenge ya kigaidi katika mkoa wa Idlib wa kaskazini mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la SANA liliripoti habari hiyo jana Jumanne na kunukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ikisema kuwa, kushambulia maficho ya magenge ya kigaidi huko kaskazini magharibi na kusini mwa Syria ni haki na ni wajibu wa jeshi la nchi hiyo ambalo jukumu lake kuu ni kulinda usalama wa nchi na raia.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetamka wazi kuwa, uongo wa aina yoyote ile unaonezwa na mataifa yanayojifanya kupambana na ugaidi ya Marekani na Magharibi pamoja na mamluki wao chini ya mwavuli wa mashirika ya kimataifa, hauwezi kulizuia taifa la Syria kuendelea na mapambano yake hadi litakapokomboa kila shibri ya ardhi ya nchi hiyo. 

Genge la kigaidi la Daesh (ISIS) na magenge mengine mengi ya kigaidi na ukufurishaji yalisambaratishwa mwaka 2017 baada ya miaka minne ya ukatili na ugaidi wao wa kuchupa mipaka katika nchi mbili za Iraq na Syria na kuteka maeneo mengi muhimu ya nchi hizo mbili za Kiarabu. 

Lakini pamoja na hayo, wako baadhi ya magaidi wamejificha ndani ya jamii huko Iraq na Syria na huwa baadhi ya wakati wanashambulia raia na maafisa usalama ili kujionesha kuwa bado wapo.

342/