Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

12 Novemba 2022

20:20:15
1322531

Jenerali Salami: Iran haitafumbia macho jinai za maadui

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haitoacha jinai za maadui zipite hivi hivi bila ya kupewa majibu makali.

Brigedia Jenerali Hossein Salami alisema hayo jana Ijumaa hapa Tehran akihutubia marasimu ya kumbukumbu ya kufa shahidi Jenerali Hassan Tehrani-Moghaddam, 'Baba wa sekta ya makombora ya Iran' miaka 11 iliyopita.

Brigedia Jenerali Salami ameeleza bayana kuwa, maadui wameunda mrengo wa pamoja wakidhani watalifungia njia zote taifa hili, lakini jitihada zao hizo zimefeli na kugonga mwamba. Amesema kamwe maadui wa Iran hawawezi kufikia malengo yao batili kwa kuwa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu wamesimama kidete na wala hawatetereshwa na njama hizo za maadui.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kuwa, "Maadui wanataka kuishughulisha Iran na masuala ya ndani ya nchi, ili nchi hii ya Kiislamu iachane na malengo yake ya juu na maono yake ya mbali."

Kamanda Salami amesema licha ya njama hizo za maadui, lakini Jamhuri ya Kiislamu karibuni ilifanikiwa kuvikabilia vikosi vilivyo dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu katika eneo la Kurdistan ya Iraq, mbali na kufanya luteka ya kijeshi karibu na Mto Aras.

Aidha amebainisha kuwa, Iran imefanikiwa kurusha satalaiti katika anga za mbali, imefanyia majaribio mfumo wa makombora ya Bavar 373, na hivi karibuni kabisa imeunda kombora la balestiki la Hypersonic lisiloweza kutunguliwa na mfumo wowote wa ulinzi.

Amesisitiza kuwa, machafuko ya hivi karibuni ya nchini Iran yamechochewa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, maadui hao wamehamaki kutokana na kushindwa vibaya na taifa la Iran tangu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Kamanda Mkuu wa  Jeshi la SEPAH la Iran ameongeza kuwa, taifa la Iran limebadilisha mahesabu ya maadui waliotaka kuwatumia vibaya baadhi ya vijana wa Kiirani waliowapotosha, wakiwa na ndoto za kukabiliana na mapinduzi ya kimataifa.

342/