Main Title

source : Parstoday
Jumapili

13 Novemba 2022

15:55:27
1322834

Mashinikizo mapya ya Magharibi dhidi ya Iran baada ya kushindwa mradi wa kuibua ghasia

Nchi za Magharibi baada ya kushindwa mradi wao wa kuibua ghasia nchini Iran sasa zinatafuta njia nyingine mpya mbadala ili kuiwekea mashinikizo Tehran. Katika uwanja huo, nchi za Magharibi khususan za Ulaya mbali na kuratibu vikwazo vipya zimejielekeza katika kutoa taarifa na maazimio dhidi ya Iran sambamba na kushadidisha mashinikizo ya kisiasa dhidi ya nchi hii.

Kuhusiana na hilo,Troika ya Ulaya inayoundwa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani imetoa taarifa ya pamoja ikidhihirisha misimamo yake iliyo dhidi ya Iran. Taarifa hiyo imedai kuwa: "tunalaani harakati za uvurugaji za Iran Mashariki ya Kati na katika eneo; na tumedhamiria kukabiliana nazo. Tutahakikisha kuwa Iran haitamiliki silaha za nyuklia. Tunatiwa wasiwasi na hatua ya Iran ya kutoshirikiana ipasavyo na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyukilia (IAEA)." 

Katika hatua nyingine dhidi ya Iran, Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimetayarisha rasimu ya azimio dhidi ya Iran kwa ajili ya kuliwasilisha kwa Umoja wa Mataifa. Rasimu hiyo aidha imesema kuwa kuna udharura wa kufanyika haraka kikao cha bodi ya usimamizi wa nyuklia ya Iran ili kubainisha taathira za urani inayodaiwa kupatikana katika maeneo matatu ya Iran. Uamuzi huu umechukuliwa kabla ya kufanyika kikao cha msimu cha Bodi ya Magavana ya IAEA. Katika kikao hicho, serikali za Magharibi zinataraji kuitaka Iran isaini azimio la kuzidisha ushirikiano wake katika masuala ya nyuklia. Aidha rasimu hiyo tajwa ya azimio imesambazwa miongoni mwa wanachama wa Bodi ya Magavana; ambapo Tehran imekubali wakaguzi wa wakala wa IAEA kutembelea taasisi zake za nyuklia katika safari yao nchini Iran mwezi huu ili kufanya uchunguzi kuhusu tetesi za karibuni za wanachama 35 wa taasisi hiyo ya kimataifa kuhusu madai ya urani iliyopatikana katika maeneo matatu ya nyuklia hapa nchini. Kwa utaratibu huo, licha ya Iran kuonyesha nia njema kwa kufanya juhudi za kutatua hitilafu zilizopo kati yake na IAEA, lakini Wamagharibi wanaendelea kutumia vibaya suala hilo kama wenzo wa kutoa mashinikizo dhidi ya Tehran. 

Amir Saeid Iravani Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa anasema:"Hakuna tatizo lolote kuhusu Iran kutekeleza makubaliano ya hatua za tahadhari; na hili lilithibitishwa pia katika ripoti ya karibuni ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).  

Katika jitihada nyingine, Uingereza imeanzisha vita vipya vya kisaikolojia dhidi ya Iran kwa kumuita balozi mdogo wa Iran mjini London na kumlalamikia masuala kadhaa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza Ijumaa ilitangaza kuwa imemuita kujieleza mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Iran kwa sababu ya kile ilichokitaja kuwa "vitisho dhidi ya baadhi ya waandishi wa habari." Wakati huo huo James Cleverly Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amedai katika taarifa aliyoitoa kwamba, wamechukua hatua hiyo kufuatia vitisho dhidi ya waandishi wa habari wanaofanya kazi nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, huko nyuma pia Balozi wa Uingereza aliitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kutokana na misimamo ya uingiliaji ya Uingereza na pia propaganda zinazoendeshwa na vyombo vya habari vya lugha ya Kifarsi vyenye makao yake huko London. Baada ya kuanza ghasia na fujo hapa nchini mbali na Marekani, viongozi kadhaa wa nchi za Ulaya na Uingereza wamekuwa wakiwaunga mkono wazi wazi wafanya fujo nchini hapa sambamba na kutoa matamshi ya uingiliaji na kuchochea moto wa ghasia. Nchi hizo si tu hazijatosheka na mkondo huo wa uharibifu bali zimewawekea pia vikwazo viongozi na mashirika kadhaa ya Iran. Vikwazo ambavyo vimekabiliwa na jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo Iran pia imewawekea vikwazo baadhi ya shakhsia na taasisi za Ulaya na za Uingereza. Hujjatul Islam Sayyid Ismail Khateeb Waziri wa Usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anasema: "katika matukio yaliyoshuhudiwa hivi karibuni hapa nchini kumebainika wazi mkono wa utawala wa Kizayuni katika utekelezaji, mkono wa Uingereza katika kuendesha propaganda na wa utawala wa Saudia katika kufadhili ghasia na fujo."

Katika hatua nyingine, nchi za Ulaya zikishirikiana na Marekani zina mpango wa kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Iran kwa kisingizio cha kuunga mkono wafanya fujo wakitaraji kuwa kwa kufanya hivyo zitafanikiwa kuendeleza machafuko nchini. "Annalena Baerbock Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Jumatano iliyopita aliashiria katika ukurasa wake wa twitter kuhusu vikwazo vya sasa vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran na kudai kuwa:" tunafanyia kazi kifurushi cha vikwazo kinachofuata." 

Nchi za Ulaya na Marekani, vyombo vyao vya habari na pia vyombo vya habari vinavyotangaza kwa lugha ya Kifarsi vinavyopewa himaya ya hali na mali na nchi za Magharibi zimehusika pakubwa katika machafuko na ghasia za karibuni hapa nchini kwa kueneza nara na shaari za uwongo eti za kuwaunga mkono wananchi wa Iran huku lengo lao kuu likiwa ni kuunga mkono wafanya fujo na kuvuruga usalama wa taifa. Hata hivyo nchi hizo zimepuuza kushiriki pakubwa wananchi wa Iran katika maandamano ya kuunga mkono mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu na kudhihirisha upinzani wao mkali kwa ghasia na machafuko nchini. Hivi sasa pia licha ya kushindwa na kugonga mwamba mtawalia njama zao, nchi za Magharibi zimejiekeleza katika kustafidi na wenzo na propaganda mpya za pande kadhaa dhidi ya Iran ambazo lengo lake ni kuudhofisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia kuzidisha mashinikizo ya pande zote dhidi ya nchi hii.  


342/