Main Title

source : Parstoday
Jumanne

15 Novemba 2022

16:42:46
1323357

Abdollahian: Iraq ina wajibu wa kuzuia vitisho dhidi ya Iran kutokea Kurdistan

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa mwito kwa jirani yake Iraq kuchukua hatua za kuzuia vitisho vinavyopangwa na kutekelezwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kutokea eneo lenye mamlaka ya ndani la Kurdistan, kaskazini mwa Iraq.

Katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Iraq jana jioni, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema usalama ni suala nyeti katika kiwango cha kieneo na katika uhusiano wa pande mbili.

Amir-Abdollahian amemhutubu Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq kwa kusema: Jamhuri ya Kiislamu haitaraji kutishiwa kutoka eneo la Kurdistan ya Iraq, kwa kutilia maanani uhusiano aali wa nchi mbili hizi.

Kwa upande wake, Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema serikali ya Baghdad haitaruhusu majirani zake watishiwe kutoka katika ardhi yake.

Haya yanajiri baada ya Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kushambulia na kuharibu ngome za magaidi katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Kurdistan, kaskazini mwa Iraq.

Kikosi cha Nchi Kavu cha jeshi la IRGC hapo jana kilianzisha wimbi jipya la operesheni hiyo dhidi ya makundi ya kigaidi kwa kutumia makombora, droni na maroketi.

Iran inasisitiza kuwa, oparesheni hizo zitaendelezwa kwa nguvu zote hadi vitisho vilivyopo vitakapozimwa kikamilifu na ngome za magenge ya kigaidi zitakapoondolewa; na hadi pale viongozi wa Erbil watakapochukua hatua dhidi ya magaidi hao wanaotishia amani na usalama wa Iran.

342/