Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

17 Novemba 2022

18:17:48
1324052

Iran yaitaka Marekani iache unafiki katika mazungumzo ya JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani ipo mbioni kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kwa msingi huo amewaasa viongozi wa nchi hiyo na timu ya wapatanishi wa Washington katika mazungumzo hayo kuweka pembeni unafiki.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumatano katika kikao na waandishi wa habari na kueleza kuwa, ubadilishanaji wa jumbe baina ya Iran na Marekani kuhusu kuhuishwa mapatano hayo ya nyuklia ya mwaka 2015 umekuwa ukiendelea siku zote.

Amir-Abdollahian ameeleza bayana kuwa, "Mara ya mwisho Iran na Marekani kubadilishana jumbe juu ya kuifufua JCPOA ni saa 72 zilizopita." 

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amefafanua kuwa, Marekani imeitumia Iran jumbe kadhaa kupitia mawaziri wa mambo ya nje wa nchi ajinabi na kwamba ina haraka ya kujiunga tena na JCPOA, lakini maafisa wa Washington wanaviambia vyombo vya habari kuwa mapatano hayo si jambo la dharura kwa sasa kwa Marekani, huku nchi hiyo ikiendelea kuunga mkono ghasia hapa nchini.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewahutubu maafisa wa Washington kwa kusema: Hatufanyi mazungumzo kwa ajili ya kuzungumza tu, lakini kwa sababu tunataka matokeo. Namshauri Bwana Robert Malley (mkuu wa timu ya mazungumzo ya Marekani) na maafisa wengine wa Marekani waache unafiki.

Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, katu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaruhusu mistari yake myekundu ikiukwe kutokana na mashinikizo ya Marekani. 

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa mara nyingine tena amezionya baadhi ya nchi za Magharibi, kwa kushinikiza kufanyika kikao maalumu cha kuijadili Jamhuri ya Kiislamu katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. 

342/