Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

17 Novemba 2022

18:19:15
1324055

Kivuli cha ufashisti kwenye bunge na baraza jipya la mawaziri la utawala wa Israel

Siku ya Jumanne Novemba 15, kilifanyika kikao cha kwanza cha Bunge la Kizayuni (Knesset) ambapo wawakilishi 120 wa bunge hilo walikula kiapo mbele ya Isaac Herzog, rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kati ya wabunge 120 wa Knesset, wanachama 23 pekee ndio wapya na waliosalia ni wabunge wa zamani ambao walibaki kwenye nafasi zao katika uchaguzi wa hivi majuzi. Ikilinganishwa na bunge lililopita, idadi ya wawakilishi wanawake imepungua kutoka 36 hadi 29, na idadi ya wabunge wa Kiarabu imepungua kutoka 15 hadi 9.

Licha ya kuwa mielekeo ya kivita, ubaguzi na kupenda kujitanua imekuwepo katika serikali na mabunge yote ya utawala wa Kizayuni wa Israel, na hata miradi mikubwa zaidi ya kujitanua na ujenzi wa vitongoji vya walowezi kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas Mashariki imetekelezwa katika kipindi cha vyama vya mrengo wa kushoto na vile vinavyoitwa eti vya wapenda amani, lakini bunge jipya na baraza la mawaziri lililoundwa kutokana na bunge hilo vimetajwa kuwa bunge na baraza la mawaziri la kifashisti zaidi.

Miongoni mwa matakwa ya wawakilishi wengi wa bunge jipya la utawala wa Kizayuni wa Israel ni kufukuzwa Waarabu wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu hususan wakazi wa Baitul Muqaddas Mashariki, ruhusa ya kuwafyatulia risasi waandamanaji kwa kutumia silaha za moto na kufanya sherehe za kidini za Mayahudi huko Baitul Muqaddas. Kupunguzwa mamlaka ya mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni pia ni moja ya mipango ya mrengo ulioshinda uchaguzi wa bunge jipya la Knesset, na Chama cha Kidini cha Kizayuni (Religious Zionist Party) kimetaka kufutwa kwa kesi ya ufisadi inayomkabili Benjamin Netanyahu. Itamar Ben-Gvir kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha "Otzma Yehudit" pia ametaka kuidhinishwa sheria ya kinga kwa mawaziri wakuu dhidi ya kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Baraza jipya la mawaziri la utawala wa Kizayuni linaoongozwa na chama cha Likud linajumuisha vyama vya mrengo wa kulia ukiwemo muungano wa Otzma Yehudit- Religious Zionist Party na vilevile vyama vya United Torah Judaism (Yahadut HaTorah – UTJ).

Bezalel Smutrich, kiongozi wa chama cha Religious Zionist Party anafanya kampeni ya kuongoza wizara ya vita ya Israel huku Itamar Ben-Gvi kiongozi wa chama cha Otzma Yehudit akifanya juhudi za kuongoza wizara ya usalama wa ndani. Kundi la marabi wenye ushawishi mkubwa pia limetoa taarifa likitaka kuteuliwa Bezalel Smutrich kama Waziri wa Vita ili kuzuia kuundwa serikali ya Palestina na kuandaa mazingira ya kuendelezwa ujenzi wa vitongoni vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi.

Kwa mujibu wa Al-Monitor, serikali ya mrengo wa kulia ambayo Netanyahu aliahidi kuunda itakuwa serikali ya kisoshalisti ya kihafidhina na ya kurudi nyuma zaidi kati ya serikali zilizowahi kutawala Israel katika historia ya utawala huo.

Sifa kuu ya uchaguzi uliofanyika majuzi huko Israel ni ushindi wa Itamar Ben-Gvir mwenye itikadi kali za mrengo wa kulia, na chama chake cha Otzma Yehudit, ambacho ni kambi ya tatu ya vyama vingine vya mrengo wa kulia kwenye Knesset.

Ben-Gvir ni mkazi wa kitongoji cha Wazayuni cha Kiryat Arba katika mji wa Al Khalil kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi. Ni mmoja wa wafuasi wa "Meir Kahane", rabi wa Kizayuni mwenye misimamo ya kufurutu mipaka na kiongozi wa harakati ya Kach. Harakati hii inasisitiza sana suala la kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao na kuwahamishia katika nchi nyingine na inaamini kuwa, Palestina inapaswa kuwa mali ya Wazayuni tu.

Harakati ya Kach inalitambua suala la ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu za Palestina kuwa ni kitu ambacho hakiwezi kufumbiwa macho au kujadiliwa. Mwanzoni mwa kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina kundi hili lenye misimamo mikali kupindukia lilikuwa miongoni mwa wahusika wakuu wa mauaji na kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao, na bado wanasiasa wa genge hilo kama vile Itamar Ben-Gvir, wana ushawishi mkubwa katika muundo wa kisiasa wa utawala wa Kizayuni. Ben-Gvir amekuwa na uhusiano wa karibu sana na Baruch Kopel Goldstein, daktari Mzayuni raia wa Israel na Marekani. Miaka 28 iliyopita Baruch Goldstein alifanya mauaji ya halaiki na ya kinyama ndani ya Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim huko Al Khalili kwa kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya alfajiri. Wapalestina 30 waliuawa shahidi katika hujuma hiyo ya kigaidi. Ben-Gvir anamtambua Baruch Goldstein kuwa ndiye shujaa wake na alitundika picha ya katili huyo Mzayuni chumbani kwake kwa miaka mingi.

Kutokana na imani yake kubwa kwamba Mayahudi ndio watu bora zaidi ya wengine, Itamar Ben-Gvir ni mmoja wa wanasiasa wa Israel ambao wana chuki kubwa si dhidi ya Wapalestina pekee, bali dhidi ya watu wote wasio Wayahudi, na anataka kulipiza kisasi kwao. Hawa ndio wanaotarajiwa kuongoza serikali mpya ya utawala wa Kizayuni wa Israel!

Kulingana na gazeti la Los Angeles Times, asilimia 62 ya Wayahudi wa Israeli sasa wanajitambua kuwa wafuasi wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu mipaka, wakati mwaka 2019 idadi hiyo ilikuwa asilimia 46. Vuguvugu la mrengo wa kulia pia ndilo lenye mizizi zaidi miongoni mwa vijana wa Israel na linajumuisha takriban 70 miongoni mwao.

Hata hivyo kwa mujibu wa weledi wa mambo, kuundwa bunge na baraza la mawaziri la mrengo wa kulia wenye siasa na misimamo mikali zaidi katika historia ya Israel kunaweza kuibua changamoto za ndani na nje kwa utawala huo na kuzidisha migawanyiko na tofauti za ndani. Serikali hiyo inatazamiwa kukabiliana na changamoto katika mahusiano yake ya kigeni na nchi za Magharibi hususan katika kipindi hiki cha serikali ya Joe Biden huko Marekani.

Katika upande mwingine, kuundwa serikali hiyo yenye misimamo mikali na ya kibaguzi kunaweza kuwa fursa kwa Wapalestina kwa ajili ya kuharakisha mchakato wa mazungumzo ya ndani ili kuunda kambi moja dhidi ya adui Mzayuni.