Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

18 Novemba 2022

19:03:23
1324307

Matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula na mkwamo wa kisiasa nchini Marekani

Hatimaye, baada ya siku 9 za uchaguzi wa Marekani wa katikati ya muhula, kulingana na matokeo yaliyotangazwa ya uchaguzi wa Bunge la Kongresi, chama cha upinzani cha Republican kimepata wingi wa viti katika Baraza la Wawakilishi, nacho chama tawala cha Democratic kikapata wingi wa viti katika Baraza la Seneti.

Kwa kushinda angalau viti 218 katika Baraza la Wawakilishi, Warepublican walifikia wingi unaohitajika katika awamu katika Bunge la Kongresi ambalo litaanza duru mpya Januari 3, 2023. Hivyo, katika Bunge lijalo, Warepublican watakuwa ni wengi katika Baraza la Wawakilishi na Wanademokrat watakuwa wengi katika Seneti kwa kushinda viti 50.

Kinyume na utabiri wa kushindwa kwa kihistoria kwa Wanademokrat, lakini Warepublican hawakuweza kuanzisha wimbi lao jekundu na kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa bunge.

Kampeni za uchaguzi wa katikati ya muhula Marekani zilishuhudia mijadala ya kisiasa na ushindani wa vyombo vya habari, na kwa sababu hiyo, Warepublican walipata faida ndogo katika mabunge yote mawili, kinyume na utabiri kuhusu wimbi lao jekundu. "Lindsey Cormack" mtafiti wa masuala ya bunge katika Taasisi ya Stevens, anasema: Tulisikia mengi kuhusu kusubiri wimbi jekundu, lakini hatukuona kitu kama hicho. Warepublican walishinda viti vipya katika Baraza la Wawakilishi, lakini bila shaka, matarajio ya viongozi wa Republican hayakutimia. Kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula, kura za maoni zilionyesha kushindwa kwa kihistoria kwa Chama cha Democratic katika Bunge la Kongresi lakini matokeo yaliyotangazwa yalionyesha ushindani wa karibu kati ya vyama viwili, ambayo ina maana kwamba mgawanyiko wa kisiasa nchini Marekani utaendelea kuongezeka.

Wachambuzi wanaamini kuwa udhibiti wa chama cha Republican katika Baraza la Wawakilishi utapelekea mkwamo wa kisiasa nchini Marekani na kurejea kwa mzozo kati ya Kongresi na White House. Kwa kuzingatia utawala wa kila moja ya vyama viwili vikuu katika Mabaraza ya Wawakilishi na Baraza la Seneti, Rais wa chama cha Democratic Joe Biden anatarajiwa kukabiliwa na changamoto kubwa katika Bunge la Marekani katika kipindi cha miaka miwili ijayo ya uongozi wake ili kupitisha miswada anayoitaka bungeni hasa katika Baraza la Wawakilishi. Aidha, licha ya wingi wa Wademokrat katika Seneti, Biden atakabiliwa na vikwazo vizito kupitisha miswada inayohitaji kura za zaidi ya maseneta 60. "Mike Wagner" mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, anasema: "Pengine tutaona mgawanyiko katika Kongresi, ambao utalazimisha makubaliano ya kisiasa kati ya mabunge mawili ya Wawakilishi na Seneti, au kuzidishwa mkwamo katika uhusiano kati ya pande hizo mbili na rais."

Suala jingine ni tangazo rasmi la rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, kuwa ana nia ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2024, jambo ambalo litapelekea kuongezeka migawanyiko ndani ya Chama cha Republican kati ya kundi linalomuunga mkono Trump na lile la upinzani ambalo lina mielekeo ya wastani zaidi.

Kwa hakika, matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani yamedhihirisha tofauti za kimtazamo ndani ya chama cha Republican, na madhara yake, hasa kushindwa kwa wimbi jekundu, ambalo kwa kiasi kikubwa lilisababishwa na kura za wapiga kura kwa wagombea wa Democratic ili wafuasi sugu wa Trump waingie bungeni, kumehatarisha juhudi za Donald Trump za kutambulishwa kama mgombea pekee wa Chama cha Republican katika uchaguzi wa urais wa 2024.

Sasa Trump anakabiliwa na mpinzani mkubwa, Ron DeSantis,gavana wa jimbo la Florida, Ingawa Trump alimsaidia kupata kura zinazohitajika ili kuendelea na uongozi wake kama gavana wa Florida, sasa gavana huyo ni mshindani mkuu wa Trump katika kuwania uteuzi wa Chama cha Republican katika uchaguzi wa urais wa 2024.

Televisheni ya Fox News ya Marekani iliyo karibu na chama cha Republican ilitangaza katika ripoti kuwa: Mshindi mkubwa zaidi wa uchaguzi wa katikati ya muhula bila shaka ni "Ron DeSantis", gavana wa Florida, na mshindwa mkubwa wa uchaguzi huu ni Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani.