Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

18 Novemba 2022

19:04:05
1324308

UN: Operesheni za misaada ya kibinadamu Somalia bado ni changamoto

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa, ukame wa muda mrefu nchini Somalia tayari umewakosesha makazi zaidi ya watu milioni moja

Taarifa ya jana Alkhamisi ya shirika hilo imesema kuwa, mazingira ya utendaji kazi nchini Somalia mwezi uliopita wa Oktoba yaliendelea kuwa magumu kutokana na ukame mkubwa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema, hali ya usalama nchini humo inaendelea kuzorota kutokana na kuongezeka mgogoro wa vita kati ya genge la kigaidi la al Shabaab na askari wa Somalia kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi.

Vita baina ya jeshi la Somalia linaloshirikiana na wapiganaji wa kieneo dhidi ya genge la kigaidi la al Shabaab vinaendelea katika majimbo ya katikati ya nchi hiyo. Katika matukio ya hivi karibuni, genge la al Shabaab limetimuliwa kwenye vijiji vya vingi vya kiistratijia lilivyokuwa linavidhibiti, katikati ya Somalia. 

Somalia ina migogoro mingi. Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa, mbali na vita, ukame uliopo hivi sasa umewakosesha makazi zaidi ya watu milioni moja mwaka 2022 pekee, huku njaa ikikumba maeneo ya kusini na katikati mwa Somalia.

Somalia ndiyo nchi iliyoathiriwa zaidi na ukame katika eneo hilo huku zaidi ya milioni 7 - nusu ya wakazi wa nchi hiyo - wakihitaji msaada wa kibinadamu huku mamilioni ya wengine wakikabiliwa na njaa kali.Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema jana Alkhamisi kwamba sehemu kubwa ya eneo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na ukame mbaya zaidi katika miaka 40 iliyopita. Watu wapatao milioni 46 wanakabiliwa na njaa kali katika eneo hilo. 

342/