Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

18 Novemba 2022

19:10:36
1324316

Abdollahian azihutubu Israel, Magharibi: Iran si Libya au Sudan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maadui wameelekeza mashambulizi yao dhidi ya ardhi na utambulisho wa Iran kwa kuunga mkono harakati za ugaidi ndani ya nchi; lakini njama hizo zimegonga mwamba kutokana na kusimama kidete Wairani.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Alkhamisi katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa: Idara za usalama, utawala bandia wa Israel na baadhi ya wanasiasa wa nchi za Magharibi waliopanga njama za kuzusha vita vya ndani nchini Iran ili kuibomoa nchi hii wanapaswa kufahamu kuwa, Iran sio Libya wala Sudan.

Abdollahian amesema taifa la Iran limetoa pigo kwa maadui wanaokula njama za kuwagawa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu, na wanaotaka kubadilisha utambulisho wa taifa hili, mbali na kuhujumu ardhi na mamlaka ya kujitawala nchi hii.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi za Magharibi kwa kuunga mkono kwa hali na mali magenge ya kigaidi yanayolenga kuyumbisha amani na usalama wa Jamhuri ya Kiislamu.

Usiku wa kuamkia jana, watu wasiopungua saba waliuawa shahidi huku wengine zaidi ya kumi wakijeruhiwa, baada ya magaidi wawili waliokuwa juu ya pikipiki kuwashambulia kwa risasi raia na maafisa usalama katika mji wa Izeh mkoani Khuzestan, kusini magharibi mwa Iran.

Vikosi vya usalama vya Iran vimewatia mbaroni watu kadhaa wanaohusishwa na shambulio hilo la kigaidi, na jingine lililotokea pia usiku wa kuamkia jana pia katika mji wa Semirom katika mkoa wa kati wa Esfahan, na kusababisha vifo vya watu watatu huku maafisa usalama wanane wakijeruhiwa.

Aidha maafisa usalama wawili waliuawa shahidi huku wengine wawili wakijeruhiwa katika shambulio jingine lililotokea katika mji wa Malekshahr mkoani Esfahan.

Wimbi hili la mashambulio limejiri chini ya mwezi mmoja baada ya gaidi aliyekuwa na silaha nzito kuvamia Haram Takatifu ya Shah Cheragh mnamo Oktoba 26 katika mji wa Shiraz, mkoa wa kusini wa Fars kabla ya Swala ya Magharibi na kuua wafanyaziara 15 akiwamo mwanamke na watoto wawili na kuwajeruhi wengine 40.

342/