Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya serikali ya Gaza, Iyad Al-Bazm, amethibitisha, katika taarifa yake, kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha "kuwapo kwa petroli iliyokuwa imehifadhiwa ndani ya nyumba hiyo, ambayo ilisababisha mlipuko mkubwa wa moto na kuua idadi hiyo ya watu."
Al-Bazm amesema kamati maalumu imeundwa ili kuchunguza pande zote kuhusu moto huo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa magari ya kubebea wagonjwa katika Hospitali ya Indonesia iliyopo Jabalia, Salah Abu Laila amesema miili 20 iliyoungua imepelekwa hospitalini hapo baada ya kuungua kwa jengo la familia ya Abu Raya mjini Jabalia na kueleza kuwa watoto wasiopungua 7 ni miongoni mwa waliofariki dunia katika tukio hilo.
Mwandishi wa televisheni ya Al-Jazeera katika Ukanda wa Gaza amenukuu chanzo cha matibabu kikisema kuwa watu 21 wa familia moja wamefariki dunia katika moto huo uliozuka jana Alhamisi katika jengo la makazi kwenye eneo la Tel Zaatar katika kambi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa walisikia kelele za watu lakini hawakuweza kuwafikia wahanga ili kutoa msaada kutokana na kukithiri kwa moto huo.
Kufuatia moto huo, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetangaza maombolezo ya umma leo Ijumaa.
342/