Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

19 Novemba 2022

16:06:44
1324623

Kiongozi wa Korea Kaskazini: Tutatumia silaha za atomiki kujibu vitisho vya atomiki

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un ameionya Marekani kuwa nchi yake itajibu vitisho vya atomiki kwa silaha za atomiki na makabiliano kwa makabiliano dhidi yake.

Kim ametoa indhari hiyo wakati akisimamia jaribio la ufyatuaji wa kombora linalovuka bara moja kuelekea jengine aina ya Hwasong-17 na kusisitiza kuwa kitisho chochote cha kijeshi dhidi ya Pyongyang kitakabiliwa na jibu kali la silaha za atomiki.

Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini vimeripoti mapema leo kuwa Kim amesema hayo alipokuwa akisimamia uzinduzi wa kombora la masafa marefu la Hwasong-17 akiwa na binti yake mwenye umri wa miaka tisa. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la Yonhap, kombora hilo lililorushwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pyongyang, lilipaa umbali wa kilomita 999.2 angani katika mwinuko wa kilomita 6,000.

Ripoti ya Yonhap imeongezea kwa kusema: "ufyatuaji huu wa majaribio umeonyesha jinsi mitambo mipya na ya kistratejia ya silaha za Korea Kaskazini na utendaji wake wenye nguvu wa kivita inavyoweza kuaminika. Ufyatuaji huo umefanyika katika hali isiyostahamilika iliyosababishwa na hatua za kuanzisha makabiliano ya kijeshi za Marekani na vikosi vya maadui wengine".

Wakati akifuatilia uzinduzi wa kombora hilo la Hwasong-17 Kiongozi wa Korea Kaskazini amebainisha kuwa, kurushwa kombora la balestiki linalovuka mabara kunaonyesha kuwepo uwezo wa kuaminika na madhubuti katika nchi yake wa kukabiliana na aina yoyote ya kitisho cha nyuklia.

Kim ametahadharisha kwa kusema: "ikiwa maadui wataendelea kutoa vitisho dhidi ya Korea Kaskazini kwa kutangaza zana zao za kushambulia za nyuklia, serikali na chama chetu, nazo pia zitatoa jibu kali kwa vitisho vya nyuklia kwa silaha na makabiliano kwa makabiliano".../

342/