Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

19 Novemba 2022

16:09:09
1324627

Russia na China zapinga azimio la Bodi ya Magavana ya Wakala wa IAEA dhidi ya Iran

Azimio jipya la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani limepasishwa ambapo limetuma ujumbe ulio wazi kufuatia kupungua kwa kura za nchi zilizoliunga mkono licha ya mashinikizo mapya ya kisiasa ya Marekani na Troika ya Ulaya dhidi ya Iran.

Katika kura zilizopigwa juzi Alhamisi,  nchi 26 zilipiga kura ya ndio zikiunga mkono azimio dhidi ya Iran, nchi 5 hazikupiga kura na nchi mbili yaani Russia na China zilipiga kura ya hapana. Hata hivyo ukichunguza matokeo baada ya upigaji kura ukilinganisha na azimio kama hilo la mwezi Juni mwaka huu tunashuhudia uhakika mwingine wa mambo. Katika azimio lililopita, mbali na Russia na China ambazo zilipinga, nchi 30 zilipiga kura ya ndio na 3 hazikupiga kura. Katika uga huo, kwa mujibu wa weledi wa mambo kura za ndio zilizopigiwa azimio hilo jipya ambazo zinatambuliwa kama zisizo za dharura na zisizo na sababu zimepungua kwa asilimia 11. 

Mikhail Ulyanov Mwakilishi wa Russia katika wakala wa IAEA ameitaja hatua  hiyo ya Troika ya Ulaya na Marekani dhidi ya Iran kuwa isiyojenga na isiyofaa na kueleza kuwa: bila ya kuzingatia msukumo wa pande zilizoandaa azimio hilo, limesababisha kuwa ngumu zaidi hali ya mambo kuhusu masuala ya usalama na mazungumzo ya Vienna kuhusu mapatano ya JCPOA na ndio maana Russia ikapiga kura ya kulipinga azimio hilo.  

Mjadala wa kuwasilisha azimio dhidi ya Iran ulianza kujadiliwa katika kikao cha Bodi ya Magavana wa IAEA tangu wiki jana; ambapo Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo alitoa madai ya kutopatiwa ufumbuzi hitilafu zilizopo kati ya wakala huo na Iran kuhusu masuala ya usalama. Marekani na Troika ya Ulaya ndizo zilizosambaza rasimu ya azimio hilo kwa nchi wanachama wa Bodi ya Magavana wa IAEA. 

Azimio hilo limekariri madai mazito kuhusu kupatikana mada za nyuklia katika maeneo matatu ya Iran na kubainisha kuwa ni jambo la dharura kwa Iran kushirikiana na wakala wa IAEA. Azimio hilo aidha limeitaka Iran itoe maelezo ya kiufundi yenye mashiko bila kuchelewa kuhusu madai yaliyotolewa na pia  iandae mazingira ya  kufikiwa taasisi na zana hizo tajwa kwa ajili ya kukusanya sampuli. 

Hatua hii dhidi ya Iran imechukuliwa huku Tehran ikiwa tayari imekubali wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kufanya safari mwezi huu hapa nchini ili kutembelea taasisi zake za nyuklia na kuchunguza madai ya kupatikana mada za urani katika maeneo matatu ya nyuklia hapa nchini. 

Grossi amekuwa akitoa madai tokea miaka mitatu iliyopita kuhusu kile alichokiita shughuli za nyuklia ambazo hazijatangazwa katika maeneo mbalimbali nchini Iran. Madai hayo kwa mara ya kwanza yalitolewa na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na kisha yakavaliwa njuga na kuchochewa na vyombo vya habari na wapatanishi wa Magharibi. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wake imepinga madai hayo na kusisitiza kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki haupasi kutoa hukumu kwa kutegemea nyaraka za uzushi za utawala wa Kizayuni ambazo hupatiwa taasisi hiyo kwa malengo maalumu ya kisiasa.  

Chombo hicho hakipaswi kutoa hukumu na maoni kwa kutegemea nyaraka za uzushi za utawala wa Kizayuni ambazo hupewa taasisi hiyo kwa malengo maalum ya kisiasa.

Kwa utaratibu huo, licha ya nia njema ya Iran na jitihada zake za kutatua hitilafu kati yake na IAEA, lakini Wamagharibi pia wameendelea kufanya juhudi ambapo majuzi wamewasilisha azimio katika Bodi ya Magavana ya IAEA ili kutumia suala hilo kama wenzo wa mashinikizo dhidi ya Tehran. 

Mohsen Naziri-Asl Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao yake huko Vienna ameeleza kuvunjwa moyo kwamba: Bodi ya Magavana inachunguza kadhia ya uwongo badala ya kutoa mchango katika kudhamini usalama na amani duniani kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya utendaji wa chombo hicho. Amesema, Troika ya Ulaya na Marekani zimetumia vibaya vikao vitatu vya karibuni vya bodi hiyo kwa maslahi yao duni ya kisiasa.  

Hatua ya Marekani na Troika ya ulaya ya kupasisha azimio jipya katika Bodi ya Magavana ni ishara ya wazi ya hatua hasi za nchi za Magharibi ambazo zinadhani kwamba kufuatia ghasia na machafuko ya karibuni nchini Iran kwa upande mmoja, na kwa upande wa pili mkwamo wa sasa katika mchakato wa mazungumzo ya Vienna sambamba na Marekani kung'ang'ania kutoafiki matakwa halali ya Iran ili kuiondolea nchi hii vikwazo na kuhitimisha masuala ya usalama yaliyosalia, zitaweza kuilazimisha Tehran kukubali matakwa yao yasiyo ya kimantiki kupitia mashinikizo ya kisiasa au kuipigisha Iran magoti ili itupilie mbali matakwa yake halali. 


342/