Main Title

source : Parstoday
Jumapili

20 Novemba 2022

19:57:59
1324951

Hamas: Mpango wa wavamizi wa Kizayuni huko al Khalil utashindwa

Sambamba na kupongeza muqawama na mapambano ya wananchi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, msemaji wa harakati ya Hamas amesisitiza kuwa, juhudi za utawala wa Kizayuni za kuimarisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi huko al Khalil hazitafanikiwa.

Hali ya sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hususan katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni tata mno, ambapo wapiganaji wa Kipalestina wanajibu jinai zisizo na idadi za Wazayuni kwa njia yoyote ile, na jambo hilo limeweka mazingira magumu kwa Wazayuni maghasibu.

Abdul Latif al-Qanou, Msemaji wa Harakati ya Mupambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema: "Mashambulio ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina katika mji wa al Khalil, kuvunjiwa heshima misikiti na jaribio la kutaka kuuyahudisha mji huo vitakabiliwa na muqawama na mapambano ya Wapalestina."

Al-Qanou amesisitiza kuwa, mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya hujuma za walowezi huko al Khalil yanafanyika katika fremu ya mapambano yasiyo na kikomo dhidi ya wavamizi hao kwa ajili ya kulinda ardhi na maeneo matakatifu.

Msemaji wa Hamas amepongeza muqawama wa wananchi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al Khalil katika kutetea mji na maeneo yao matakatifu.

Awali Wazayuni walikuwa wakipigana tu na Wapalestina wa kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na katika eneo la Gaza, lakini sasa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ulioko mashariki mwa Palestina umekuwa kaa la moto linalowakosesha usingizi Wazayuni kutokana na mapambano ya silaha ya vijana wa eneo hilo.


342/