Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

24 Novemba 2022

18:45:27
1325940

Moscow yajibu mpango wa CIA wa kuwasajili raia wa Russia

Ubalozi wa Russia mjini Washington umesema azma ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ya kutaka kuwasajili raia wa Russia katika taasisi hiyo ni ithibati nyingine inayoonesha kuwa Marekani inafanya juu chini ili kuidhalilisha nchi hiyo. Hata hivyo ubalozi huo umesisitiza kuwa njama hizo za Washington hazitafua dafu.

Ubalozi huo wa Russia nchini Marekani umesema hayo leo Alkhamisi, kufuatia ripoti iliyochapishwa na gazeti la Wall Street Journal iliyofichua kuwa, Naibu Mkurugenzi wa Operesheni wa CIA, David Marlowe anapanga kuwasajili raia wa Russia eti walioghadhabishwa na mgogoro wa Ukraine, kwenye taasisi hiyo ya kijasusi ya US.

Taarifa ya Ubalozi wa Russia mjini Washington imeeleza kuwa: Hatukuwa na njozi kuhusu harakati za CIA dhidi ya Russia, kwani ni wazi kuwa vyombo vya intelejensia vya Marekani vinajaribu kuyumbisha uthabiti wa Russia.

Ubalozi huo wa Russia nchini Marekani umebainisha kwenye taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye mtandao wa Telegram kuwa, kauli ya Marlowe yumkini imetokana na uchu wa kutaka Kongresi ya Marekani iongeze bajeti ya CIA.

Haya yanajiri siku chache baada ya David Petraeus, mkuu wa zamani wa CIA kusema kuna uwezekano wa Marekani kujiingiza moja kwa moja katika vita vya Ukraine hata bila ridhaa ya NATO.

Nchi za Magharibi hasa Marekani zinaipatia Ukraine silaha na zana mbalimbali za kijeshi na kuzidisha mashinikizo kwa Russia tangu kuanza vita huko Ukraine Februari mwaka huu, huku vita na mzozo vikishadidi ndani ya Ukraine. 

342/