Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

12 Desemba 2022

16:40:19
1330410

Don DeBar: Marekani ingali inadhibiti matukio ya Libya

Mwandishi wa habari na mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa wa Marekani amesema kufufuliwa kwa faili la shambulio la bomu la Lockerbie la mwaka 1986 kunaonesha wazi kuwa Washington ingali inadhibiti na kuingilia masuala ya ndani ya Libya.

Don DeBar, mtangazaji wa radio mjini New York na pia mwanaharakati wa kupinga vita amesema hayo baada ya raia mmoja wa Libya anayeshukiwa kuunda bomu lililouwa watu 270 waliokuwa katika ndege ya shirika la Pan Am huko Scotland mwaka 1988 kutiwa nguvuni nchini Marekani.

DeBar ameiambia kanali ya Press TV ya Iran kuwa, kulibebesha dhima taifa zima la Libya kutokana na kadhia ya Lockerbie kulipelekea taifa hilo la Kiarabu la kaskazini mwa Afrika likabiliwe na vikwazo shadidi vya kuumiza, licha ya Tripoli kukanusha madai dhidi yake.

Kwa mujibu wa mwanahabari huyo wa Marekani, kuhuishwa kesi ya Lockerbie kunapaswa kutazamwa katika muktadha wa matukio yanayojiri hivi sasa nchini Libya, na ukweli kwamba Marekani inajaribu kuathiri matukio hayo kwa maslahi ya mchezo wake wa kijiopolitiki.

Waendesha mashitaka wa Scotland wamesema familia za wale waliouawa kwenye shambulio hilo zimefahamishwa kwamba Abu Agila Muhammad al-Marimi,  anayeshukiwa kuunda bomu lililotumika kwenye shambulio la Lockerbie sasa yuko kizuizini.

Awali mshukiwa huyo alikuwa anashikiliwa nchini Libya akituhumiwa kushiriki kwenye mashambulizi dhidi ya klabu moja ya usiku mjini Berlin mwaka 1986. Wizara ya Sheria ya Marekani imethibitisha kumshikilia mshukiwa huyo, ikisema kuwa anatazamiwa kufikishwa mahakamani karibuni mjini Washington.

Al-Marimi ni afisa wa tatu wa ujasusi wa Libya kufikishwa mahakamani nchini Marekani kwa mashambulizi dhidi ya ndege hiyo ya shirika la Pan Am iliyokuwa ikiruka kutoka London kwenda New York tarehe 21 Disemba 1988. Ndege hiyo, Boeing 747, iliripuka ikiwa juu ya mji mdogo wa Lockerbie, Scotland, na kuwauwa watu 259 waliokuwemo ndani yake na wengine 11 mahala ilipoangukia.


342/