Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

24 Desemba 2022

19:57:24
1333226

Al-Azhar yasema Taliban imekiuka sheria za Kiislamu kwa kuzuia wanawake kusoma vyuo vikuu

Sheikhe Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri ameutaka utawala wa Taliban kuondoa marufuku ya elimu ya juu kwa wanawake nchini Afghanistan.

Sheikhe Mkuu wa Al-Azhar, Sheikh Ahmed El-Tayeb Al-Azhar amesema amesikitishwa sana na uamuzi wa Taliban wa kuwapiga marufuku wanawake wa Afghanistan kuendelea na masomo ya chuo kikuu.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Sheikh El-Tayeb alisema marufuku iliyowekwa na Taliban kwa masomo ya chuo kikuu ya wanawake inakinzana na wito wa Sharia ya Kiislamu kwa wanaume na wanawake kutafuta elimu "kutoka utotoni hadi kaburini".

Aidha Sheikh El-Tayeb amebainisha zaidi kuhusu idadi kubwa ya Hadithi za Mtume Mohammad SAW kuhusiana na suala hili na kuongeza kuwa kuna wanawake wengi wa Kiislamu ambao wamefanikiwa na kuweza kuongoza katika nyanja za sayansi, elimu na siasa.

"Uamuzi huu wa kushtua kwa dhamiri za Waislamu na wasio Waislamu haukupaswa kutolewa na Mwislamu yeyote," Sheikh Mkuu wa Al Azhar amesema.

Sheikh EL-Tayeb ametoa wito kwa wale walio madarakani nchini Afghanistan kupitia upya uamuzi huo, na kuwakumbusha kuhusu siku ya kiyama  wakati pesa, mamlaka, hadhi na siasa hazitakuwa na manufaa

Mapema wiki hii, Taliban ilitangaza kupiga marufuku mahudhurio ya wanawake katika vyuo vikuu nchini Afghanistan, uamuzi ambao umelaaniwa vikali duniani kote.

Waziri wa Elimu ya Juu wa Taliban Neda Mohammad Nadeem amesema marufuku hiyo imekuja kwa kuwa wanawake hawajatii kanuni za mavazi na kwa kuwa baadhi ya masomo ya shule hayakuwafaa.

342/